Monday, January 14, 2013

UTEKELEZAJI WA ILANI YA UCHAGUZI-SINGIDA

NA. Halma Jamal
MPANGO wa kilimo (DADPS), halmashauri za Wilaya za Mkoa wa Singida, umechimba malambo sabini, ikilinganishwa na 19 yaliyokuwepo miaka saba iliyopita, kuwezesha mifugo kupata maji.

Malambo hayo yamechimbwa kwa ushirikiano kati ya serikali kuu, halmashauri na wananchi kati ya mwaka 2005 hadi 2012.

Mkuu wa mkoa, Dk. Parseko Kone, alisema hayo wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake, juu ya utekelezaji wa ilani ya CCM mkoa wa Singida, kwa kipindi cha miaka saba iliyopita.

Dk. Kone alisema katika kipindi hicho, kumekuwa na ongezeko la la madume bora ya ng’ombe kutoka 88 mwaka 2005 hadi kufikia 608 mwaka jana.

Alisema mpango wa uhamilishaji mifugo ya asili ulioanza mwaka 2008/2009 umeonyesha mafanikio kwa kuongeza idadi ya ng’ombe waliohamilishwa hadi kufikia 1,267, huku ndama wakiwa 672 hadi kufikia mwaka 2012.

Dk. Kone alisema katika kipindi hicho elimu kupitia mifugo darasa imeongezeka kutoka wafugaji 327 hadi kufikia wafugaji 7,561, hali ambayo pia imeongeza takwimu za wafugaji bora na idadi ya ng’ombe walioboreshwa.

Aidha Dk. Kone alisema mwaka 2005 hapakuwa na kiwanda cha kusindika bidhaa za ngozi na maziwa lakini hadi mwaka jana kuna viwanda vidogo vinne vinavyotengeneza bidhaa zitokanazo na mazao ya ngozi.

Alisema pia wafugaji kuku wa kienyeji wa biashara wenye kufuga kuanzia kuku 100, watu 503 walipatiwa mafunzo hadi kufikia 2010/2011, wakiwa na kuku 50,300, ikilinganishwa na wafugaji saba mwaka 2006/2007.

Mkoa wa Singida una jumla ya mifugo mbalimbali ikiwemo mbuzi, ng'ombe na kondoo 4,145,819, huku kuku pekee wakiwa ni 1,730,031.

No comments: