Wednesday, January 2, 2013

BARABARA KUU YA SINGIDA -MWANZA YAFUNGWA


Baadhi ya madereva wa masafa marefu na wananchi wa Munug'una, Singida vijijini wakiagalia daraja lililokatika na kusababisha msururu wa magari zaidi ya 200 kushindwa kupita mkoani Singida

Meneja wa TANROADS mkoa Singida Yustak Kangole(aliyeinama) akiwaelekeza wakandarasi wa kampuni ya CHICO kutathimini gharama ili walifanyie ukarabati na magari yaanze kupita

Mkuu wilaya Singida mwalimu Queen Mlozi (kushoto)akiteta jambo na RPC Singida Linus Sinzumwa katika eneo la daraja la kijiji cha Mnung'una, Singida vijijini kukatika na kusababisha magari kushindwa kupita

Mwalimu Queen Mlozi mkuu wilaya Singida akiwasiliana eneo lilikokatika daraja

Baada ya daraja Mnung'una kukatika, baadhi ya madereva wamebuni njia ya mzunguko, lakini pia ya hatari

 Dereva na msaidizi wake wakijipumzisha baada ya daraja la kijiji cha Munung'una barabara Singida-Nzega kukatika mkoani Singida, zaidi ya magari 200 ya abiria na mizigo yamekwama mkoani singida yakiwa safarini kuelekea maeneo mbalimbali ya tanzania na nchi jirani

HABARI NA PICHA ZOTE ZIMEPIGWA NA HALMA JAMAL


MVUA kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani Singida,zimeendelea kuleta maadhara makubwa ikiwemo kuvunja daraja na barabara kuu ya Singida – Mwanza

Mvua hizo kubwa zilizoanza kunyesha mwanzoni mwa mwezi wa 12 mwaka jana,jana tar1 zilisababisha daraja la munung’una lililopo katika kijiji cha Msisi wilayani Singida,barabara kuu itokayo Singida kuelekea mikoa ya kanda ya ziwa na nchi jirani za Kongo,Burudi,Rwanda na Uganda, kubomoka na kusabaisha shimo kubwa.

Kubomoka kwa daraja hilo,kumesababisha foleni kubwa ya magari yanayokadiriwa kuwa ni zaidi ya mia tano.Pia mawasiliano kati ya mikoa mbalimbali ikiwemo ya kanda ya ziwa na nchi jirani,yamekatika.

Aidha mmoja wa madereva walioathirika na kubomoka kwa daraja hilo,George Medadi,aliyekuwa akitokea Mwanza akirudi jijini Dar-es-salaam,alisema daraja hilo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na kujengwa chini ya kiwango.

Kutokana na hali hiyo wenyeji wa wa kijiji hicho wamesema kuwa kalvati zilizotumika kujengea daraja hilo,ni zile za zilizowekwa wakati wa uongozi wa Nalaila Kiula alipokuwa waziri wa ujenzi.

Wakifafanua zaidi wananchi hao walisema kuwa Kampuni ya CHICO iliyojenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami,waliyatumia makalivati hayo hayo na walichofanya ni kulundika udogo juu tu.

Naye dereva Iddi Mussa,alisema kuwa barabara nyingi zinazojengwa na kampuni za kichina,zimekuwa hazisimamiwi ipasavyo kitendo kinachochangia kuharibika haraka na kuisababishia serikali kuingia hasara kubwa.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Singida,mwalimu Queen Mlozi,alisema kwa kuanzia,wameimarisha ulinzi katika eneo hilo pamoja na kufungua kituo kidogo cha kutolea huduma ya afya na kuthibiti uwezekano wa kutokea kwa magonjwa ya mlipuko.

“Pia tumefungua barabara ya Singida-Ndago –Misigiri kwa ajili ya kutumiwa na mabasi ya abiria na ale yenye uzito chini ya tani kumi.Vile vile tunaangalia uwezekano wa kuangalia ni namna gani watu waliokwama,wanapata chakula”,alisema.

Meneja wa TANROADS mkoa wa Singida,mhandisi Yustaki Kangole,ambaye alifika na wahandisi wa kampuni ya CHICO,alisema kuwa wamekubaliana na CHICO kwamba wafukie shimo hilo kwa vifusi vya mawe makubwa ili barabara hiyo ianze kutumika mapema iwezekanavyo

“Kwa sasa tunafanya kazi hii ya muda na baada ya eneo hili kukauka,ndio ukarabati mkubwa utafanywa ili kuimarisha barabara hii muhimu kwa uchumi wa taifa”,alisema mhandisi Kangole.

Kwa mujibu wa mhandisi Kangole,barabara hiyo ilijengwa kwa kiwango cha lami na kampuni ya kichina ya CHICO na ilikabidhiwa kwa serikali mwaka 2008.

Wakati huo huo,mkuu wa wilaya ya Mkalama,Edward Ole Lenga,amesema kuwa raia moja wa nchini China,amefariki dunia baada ya gari lake kusombwa na maji ya mto kaka jirani na kijiji cha Gumanga

Alisema mchina huyo ambaye jina lake bado halijatambuliwa hadi sasa,alisombwa na maji ya mto juzi majira ya jioni wakati akikatisha mto wa kijiji cha Gumanga wilaya ya Mkalama.Ndani ya gari hilo mchina huo alikuwa na mtoto wake ambaye alinusurika kufa.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida,Linus Sinzumwa,alikiri kutokea kwa tukio hilo la mchina kusombwa na maji mto.


 

No comments: