Wednesday, January 2, 2013

MRADI WA MAHUSIANO SINGIDA WAGHARIMU MIIONI 149

SHIRIKA lisilo la kiserikali la Singida Non – Governmental Organizations Network (SINGONET), limetumia zaidi ya shilingi 149.8 milioni kugharamia utekelezaji wa mradi wa kuimarisha mahusiano kati ya wananchi na wabunge, madiwani na watendaji wa serikali.
Hayo yameelezwa juzi na mratibu wa SINGONET, Maendeleo Makoye, wakati akitoa taarifa yake kwenye mdahalo mkubwa kwa kuimarisha mahusiano ya wananchi na wabunge,madiwani na watendaji wa serikali.
Alisema fedha hizo zilizotolewa na shirika la The Foundation For Civil Society kugharamia mradi huo, ambao umetekelezwa katika awamu nne kuanzia Septemba mwaka jana hadi Septemba mwaka huu.
Makoye alisema kuwa mradi huo ulilenga kuamsha ari ya ushiriki na ushirikiashwaji wa wananchi katika kuchambua, kujadili na kutoa mapendekezo yao juu ya mchakato wa uandikaji wa Katiba mpya ya Tanzania.
Aidha alitaja malengo mengine kuwa ni kujenga na kudumisha uhusiano na ushirikiano kati ya asasi za kiraia na wananchi na kushughulikia changamoto zinazoikabili jamii hasa katika upatikanajii wa huduma za elimu, afya, upatikanaji wa maji na nishati.
Katika hatua nyingine, Makoye alisema baadhi ya wabunge na Madiwani nchini, wameshindwa kuonyesha uwajibikaji wao kwa umma kama inavyotarajiwa.
Akifafanua zaidi,Makoye alisema wawakilishi hao wameshindwa kushiriki pamoja na kushirikisha jamii katika kubuni, kupanga, kutekeleza na kusimamia mipango mbalimbali ya maendeleo.
“Hakuna utaratibu ulio wazi juu ya mijadala ya pamoja kati ya wananchi na wawakilishi wao. Kwa maana hiyo, wananchi hawashiriki kuchangia maoni na mawazo ambayo Mbunge au Diwani anapaswa awawakilishe katika taasisi za maamuzi”,alisema Makoye.
Mratibu huyo, alisema mapungufu hayo ya kimawasiliano, jamii imeshindwa kuwakilishwa vilivyo na matokeo yake, serikali imeshindwa kutimiza ipasavyo mahitaji halisi na matarajio ya wananchi wake.

No comments: