Friday, January 18, 2013

UHABA WA CHAKULA MKOANI SINGIDA


Na Edilitruda Chami & Abdul Bandola.

Zaidi ya  watu  laki moja na ishirini na tisa elfu  mkoani Singida wanakabiliwa na  tatizo la uhaba wa chakula.

Hayo yamebainishwa na   kaimu mshauri wa idara ya kilimo mkoani  Singida Bw. Lucas Nkuki  wakati wa kikao cha  baraza la madiwani kilichofanyika  jana katika ukumbi wa manispaa  ya Singida.

Bw. Nkuki Amesema kuwa, tathimini iliyofanywa imebaini kuwa  zinahitajika tani 1,292 za chakula mchanganyiko kwa halmashauri ya wilaya ya Ikungi,  tani 1,184 kwa halmashauri ya wilaya ya  Manyoni,  huku tani 711 zikihitajika katika Manispaa ya Singida na tani 1296.2 katika halmashauri ya wilaya ya Singida.

Kutokana na hali hiyo Baraza la Madiwani la halmashauri ya wilaya ya Singida wametoa muda wa siku tano  kwa Mkurugenzi  wa halmashauri iyo kuhakikisha analitafutia ufumbuzi tatizo la upatikanaji wa chakula,  la sivyo wataunda tume kwenda kwa Waziri Mkuu.

Zaidi ya kaya thelathini elfu zinahitaji chakula cha msaada mkoani humo, na hadi sasa wilaya za Iramba na Manyoni zimepata chakula hicho, ingawa hakikutosheleza mahitaji.

Mkoa wa Singida una wilaya sita ambazo ni Singida mjini, Singida vijijini, Mkalama, Iramba, Manyoni  na Ikungi.

    

No comments: