Saturday, January 26, 2013

RAIA WA ETHIOPIA WAHUKUMIWA NCHINI TANZANIA


Na Nathaniel Limu

JUMLA ya raia 12 raia wa nchini Ethiopia,wamehukumiwa na mahakama ya wilaya ya Singida,kulipa faini ya shilingi laki moja (100,000) kila mmoja baada ya kukiri makosa mawili ya kuingia na kuishi ndani ya ardhi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kibali halali.

 

Pia mahakama hiyo,imeamuru basi la kampuni ya Mtei ya mjini Arusha T.797 CDZ lililokuwa limebeba Waethiopia hayo,likamatwe na kutaifishwa kuwa mali ya serikali.

 

Raia hao wa Ethiopia ambao ni bado vijana wadogo na wengine ni wanafunzi wa shule na vyuo, ni pamoja na Ahmed Mohammed Mahamud,Tazana Dijamo Walao, Mohammed Abdi Osman, Abraham Nirato Shango, Adinan Abrahim Abdalah na Alamu Ayele Gabresekesie.

 

Weingine ni Muhidini Sufiani Ahmed, Tasfai Sutatu Kidisu, Yassin Mohammed Hassan, Afandi Aden Suleiman, Ayele Liranso Gafuche na Pakala Agore Mancha.

 

Baada ya nwendesha mashitaka mwanasheria wa serikali Ahmed Seif kuwasomea makosa hayo mawili ya kuingia na kuishini nchini bila ya kuwa na kibali,washitakiwa wote kila mmoja kwa nafasi yake, walikiri kutenda makosa hayo.

 

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo,mwanasheria wa serikali,Seif,aliiomba mahakama hiyo kuwa iwape adhabu kali washitakiwa ikiwa ni njia moja wapo ya kukomesha vitendo vya wahamiaji haramu kuingia na kuishi nchini bila ya kuwa na kibali cho chote halali.

 

"Mheshimiwa hakimu vile vile naiomba mahakama yako itaifishe basi la Mtei lililotumika kuwasafirisha wahamiaji hawa haramu ili kuwaogofya wenye magari kuacha kusafirisha raia wa kigeni wasiokuwa na kibali halali cha kuingia na kuishi nchini"alisema Seif.

 

Akitoa hukumu hiyo, hakimu mfawidhi kiongozi wa mahakama ya wilaya ya Singida, Flora Ndale,alisema mahakama yake imezingatia yale yote yaliyoombwa na upande wa mashitaka na utetesi na kufikia uamuzi wa kutoa adhabu ya kulipa faini ya shilingi laki moja kwa kila mshitakiwa.

 

"Mahakama hii inawatia hatiani na kuwapa adhabu ya kulipa faini hiyo ya shilingi laki moja kila moja na atakayeshindwa kulipa faini,atakwenda kutumikia jela kwa kipindi cha miezi mitatu"alisema hakimu Ndale.

 

Hata hivyo,washitakiwa wote 12,kila mmoja wao alilipa faini hiyo ya shilingi laki moja na hivyo kuachiwa huru.

 

Kwa mujibu wa mwanasheria wa serikali Seif, washitakiwa hao wamekamatwa January 17 mwaka huu alasiri katika eneo la kijiji cha Kititimo nje kidogo ya mji wa Singida wakiwa wametokea mkoani Arusha wakielekea nchini Afrika kusini.

No comments: