Saturday, January 26, 2013

BIASHARA YA MKAA MKOANI SINGIDA NA MSTAKABALI WA MAZINGIRA


 

WANANCHI mkoani Singida, wameshauriwa kuacha biashara ya uchomaji mkaa, na badala yake waelekeze nguvu zao katika ufugaji wa nyuki, kwa madai kwamba una faida zaidi kuliko biashara ya mkaa.

Wito huo umetolewa juzi na Meneja wakala wa huduma za misitu Tanzania (T.F.S) wilaya ya Singida, Hashimu Kavito, wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya mikakati inayochukuliwa na wakala huo, kufanikisha malengo ya upandaji miti, mkoani hapa.

Alisema ufugaji wa nyuki gharama yake ni ndogo mno ukilinganisha na ile ya uchomaji mkaa.

“Pia ufugaji wa nyuki licha ya kuwa hauna gharama kubwa, unayo faida nyingi. Ufugaji wa nyuki unasaidia misitu isikatwe ovyo, bei ya asali na nta, kwa sasa ipo juu mno",alifafanua Hashimu.

Meneja huyo, alisema kutokana na ukweli huo, mfugaji wa nyuki anayo nafasi kubwa ya kuboresha uchumi wake, wilaya, mkoa na hata taifa tofauti na muuza mkaa.

Katika hatua nyingine, aliwataka wananchi wabadilike na kuanza kutambua kuwa miti ni sawa na mazao mengine yaliyozoeleka.

No comments: