Monday, July 29, 2013

CHF YAKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 377 IRAMBA


Na:Mwandishi wetu
Wilaya ya Iramba mkoani Singida, imekusanya zaidi ya shilingi milioni 377  zikiwa ni makusanyo ya ada za uanachama wa mfuko wa afya ya jamii (CHF), tangu mfuko huo uanzishwe juni mwaka 1998 hadi sasa.

 
Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na mkuu wa wilaya hiyo, Yahaya Nawanda, wakati akizungumza na  waandishi wa habari ofisini kwake juu ya maendeleo ya mfuko huo, ambao umekuwa mkombozi mkubwa kiafya kwa wakazi wa wilaya hiyo.

 
Amesema kiasi hicho cha fedha, ni ada za wakazi wa kaya 37,710 wa wilaya hiyo  zilizojiunga na mfuko huo ambayo ni sawa na zaidi ya aslimia 50 za kaya 78,000 za wilaya ya Iramba.

 
Mkuu huyo wa wilaya, amesema licha ya fedha hizo kugharamia matibabu kwa wanachama, pia zimetumika katika kukarabati majengo ya vituo vya huduma za afya na nyumba za kuishi watumishi.

VYOMBO VYA DOLA KUSAIDIA WATOTO WAISHIO MAZINGIRA HATARISHI


Na:Mussa Mbeho
Wakazi wa mkoa wa singida wameshauriwa  kutoa taarifa kwenye  vyombo vya dola pindi wanapobaini kuwa kuna watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ili kuwasaidia.

Hayo yamesemwa na Afisa ustawi wa jamii wa mkoa wa singida Bi. Zuhura Karya  wakati akikabidhi watoto  waliogundulika wakiishi katika mazingira magumu kwa uongozi wa shule ya msingi St.Vicent  iliyopo Itigi wilayani Manyoni.

Bi. Karya amesema kuwa wananchi washirikiane na viongozi wa serikali ili kufichua watoto ambao wanaishi katika mazingira hatarishi ili kuwawezesha watoto kupata haki zao za msingi na si kuwaacha waendeleee kuteseka.

 

Aidha amesema kuwa wataendelea  kuwasaidia watoto ambao wanaoteseka kwa kuwalea na kuwasomesha ili kuondokana na tatizo la ongezeko la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Bi. Karya amewataja watoto waliopatikana katika mazingira hatarishi kuwa ni Juma Masunga mwenye umri wa miaka 13, Swalehe Masunga mwenye umri wa miaka 11, Rajabu Masunga mwenye umri wa miaka 8, na Tabu Masunga mwenye umri wa miaka 6 ambao walikuwa wakiishi na baba yao aliyekuwa akijulikana kama mganga wa jadi kumbe ana matatizo ya akili.

 

MADIWANI 16 WA CHADEMA WASUSIA MKUTANO HANANG


Na:Mwandishi wetu
Madiwani 16 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wa halmashauri ya wilaya ya Hanang, mkoani Manyara juzi walisusia mkutano wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo na kuamua kutoka nje ya ukumbi wakidai kanuni za mkutano huo zimekiukwa.

Akizungumza na Waandishi wa habari nje ya ukumbi wa mkutano huo, Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Manyara kupitia tiketi ya CHADEMA, Bi.  Rose Kamili amesema madiwani hao waligoma kujiandikisha kwenye orodha ya wajumbe baada ya kutokubaliana na dondoo zilizokuwepo kwenye mkutano huo, ikiwemo ya uchaguzi wa makamu mwenyekiti wa Halmashauri hiyo na kupitisha kamati za kudumu.

Aidha mbunge huyo amesisitiza pia kwamba licha ya madiwani wa chama hicho kudai mabadiliko ya maamuzi hayo kabla ya kusoma muhtasari wa kikao, mwenyekiti alitumia ubabe kulazimisha kikao hicho kuendela na kwamba hakuwa tayari kusikiliza wazo la mtu ambaye hajajiandikisha kwenye mahudhurio ya mkutano huo.

Akihalalisha kufanyika kwa mkutano huo, Mwanasheria wa TAMISEMI,Bw. Eustad Atanas Ngatale amesisitiza kuwa taratibu za mikutano ya halmashauri zinaongozwa na kanuni za uendeshaji wa mikutano ya halmashauri ambazo zinatungwa na halmashauri yenyewe lakini uwezo huo umetolewa na Waziri mwenye dhamana ya serikali za mitaa.

HASSAN MWINYI AWATAKA WANACHI KUZINGATIA MAFUNDISHO YA DINI ILI KUDUMISHA AMANI


Na:Mwandishi wetu
 
Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, amewataka Watanzania kuzingatia mafundisho ya dini zao ili kudumisha amani na utulivu nchini.

Rais Mwinyi ametoa rai hiyo jana wakati akihutubia katika hafla ya kuhitimisha shindano la kusoma Kurani iliyofanyika katika ukumbi wa viwanja vya Sabasaba, Dar es Salam, ambako alikuwa mgeni rasmi.

Shindano hilo liliandaliwa na taasisi ya Al-Hikma Education Centre ya jijini Dar es salaam na kuwashirikisha vijana wa Kiislamu kutoka katika nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Rais Mwinyi amesema ili kudumisha amani, utulivu na mshikamano wa taifa ni muhimu kwa vijana na wananchi kwa ujumla kusoma na kuzingatia mafundisho ya dini zao, na kwamba kwenda kinyume na mafundisho ya dini kunaweza kusababisha uvunjifu wa amani kama ilivyo katika nchi nyingine za Afrika.

Katika shindano hilo mshindi wa jumla ni Suleiman Omar Ally (10), kutoka taasisi ya Al-Hikma ambaye amewashinda wenzake tisa na kundi la waliohifadhi juzuu 30, na amezawadiwa shilingi milioni 10 na zawadi nyingine.

Washindi wengine ni Abdallah Juma katika kundi la waliohifadhi juzuu 20, na Anwari Yahya amekuwa mshindi katika kundi la waliohifadhi juzuu 10.

SERIKALI NA DINI ZINAFANYA KAZI MOJA KATIKA HUDUMA ZA JAMII


Na;Mwandishi wetu
Mkuu wa mkoa wa Singida Dk. Parseko Kone amesema serikali na dini zinafanya kazi moja ya kumhudumia mwananchi katika nyanja mbali mbali za huduma za jamii.

 
Dk. Kone amesema hayo mwishoni mwa wiki katika sherehe za kuwekwa wakfu askofu Benjamin Yared Wellya wa Kanisa la Tanganyika African Church TAC zilizofanyika katika kijiji cha Chikuyu wilayani Manyoni.

 
Amesema serikali mkoani Singida mikakati ya kanisa la TAC katika kupambana na umaskini, kulinda amani na kuwa na mipango ya kuanzisha taasisi za elimu na afya katika eneo la Chikuyu.

 
Aidha, amewataka waumini kufanya kazi kwa juhudi na maarifa kwa kuzingatia utaalam wa washauri wa kilimo. Dk. Kone ametoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Singida kutumia fursa nyingi zilizopo ili kuondokana na umaskini.

 
Awali Askofu Benjamin Yared Wellya, ameahidi kushirikiana na waumini wote, serikali na taasisi nyingine katika kulinda amani, upendo na mshikamano katika jamii.

Tuesday, July 23, 2013

WAHAMIAJI HARAMU WAFIKA KWA WINGI KATIKA WILAYA YA SIMANJIRO MKOANI MANYARA


Na:Mwandishi wetu
 
Wilaya ya Simanjiro iliyoko mkoani Manyara, inaongoza kwa kufikiwa na kukaliwa na wahamiaji haramu ikilinganishwa na wilaya nyiingine za mkoa huo.

Katibu Tarafa wa Moipo, Bw. Joseph Mtataiko, amesema hayo wakati akifungua warsha iliyoandaliwa na Idara ya Uhamiaji Mkoa, kuhusu ulinzi shirikishi kwa kuwatambua na kuwafichua wahamiaji haramu.

Amesema wilaya hiyo ni maficho ya wahamiaji haramu kutokana na mgodi wa machimbo ya madini wa Mererani, kwani kila siku wageni wapya wanaingia kutoka sehemu mbalimbali nchini hasa mikoani.

Aidha, amesema wilaya hiyo ni mapito ya wageni haramu waendao nchi za jirani za kusini mwa Tanzania. Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji mkoani Manyara, Ebros Mwanguku, amewataka wananchi wa wilaya hiyo kuwa makini kwa wageni wanaoingia kwa kutoa taarifa katika kituo cha polisi, ili wafanyiwe uchunguzi kuhusu uingiaji wao wilayani humo.

Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Manyara imeendesha warsha ya uhamiaji shirikishi ikishirikisha kamati za ulinzi na usalama, katika wilaya za Babati, Mbulu na Simanjiro na kumalizia na wilaya za Kiteto na Hanang’ ili kuimarisha ulinzi na hali ya usalama na amani mkoani humo.


 

UTAMADUNI WA KITANZANIA HUENDANA NA MAADILI MAZURI


 
Na:mussa mbeho
 
Vijana katika Manispaa ya Singida wameshauriwa kufuata maadili mazuri ili kuendeleza utamaduni wa  makabila yao.

 
Kauli hiyo imetolewa  leo  na Afisa utamaduni wa manispaa ya singida Bw. Anacletus Mkuki wakati akizugumza na  Standard Radio.  Amesema endapo vijana watafuata utamaduni wa makabila yao itasaidia kupunguza  tatizo la mmomonyoko wa maadili uliopo hivi sasa.

 
Bw.  Mkuki amesema kuwa  vijana wengi wamesahau maadili ya makabila yao kitendo ambacho  kinasababisha wengi wao kutokuwa na  maadili mema.

 
Aidha, Bw. Mkuki amewaasa vijana wote kuzingatia mila na desturi zao ili kuepukana na mmomonyoko wa maadili uliopo mkoani Singida.

 

 

Monday, July 22, 2013

BASI LA MOHAMED TRANS LAPATA AJALI MJINI SINGIDA


 
Na:Edson Raymond
Abiria arobaini na watano wamenusurika kifo baada ya basi mali ya Kampuni ya Mohamed Trans lenye namba za usajili T 210 APG walilokuwa wakisafiria kutoka Dodoma kwenda Mwanza  kupasuka tairi la upande wa kulia na kuhama barabarani kwenye njia panda karibu na viwanja vya People’s Manispaa ya Singida.

 

Wakizungumza leo na standard radio mara baada ya ajali hiyo,  baadhi ya abiria wamesema imetokea muda mfupi baada ya kutoka katika stand mpya ya mabasi ya Singida ambapo walipofika eneo la round about basi hilo lilipasuka tairi na kuhama kutoka barabarani na kuingia kwenye mtaro ulioko jirani na eneo hilo.

 

Wamesema kuwa kabla ya ajali hiyo, alipita mwendesha pikipiki ambaye alikatisha ghafla mbele ya basi hilo na mara baada ya hapo basi hilo lilianza kuyumba na kuingia mtaroni.

 

Aidha kwa upande wa kondakta wa basi hilo ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake kwa madai kuwa si msemaji wa kampuni, amesema ajali hiyo imetokea kama ajali nyingine na kwamba basi hilo halikuwa katika mwendo kasi na kuongeza kuwa abiria wote wametoka salama bali kuna baadhi wamepata michubuko midogo midogo katika sehemu mbali mbali za miili yao.

 

TOZO YA SHILINGI ELFU MOJA YA SIMU KUSAIDIA KUENEZA UMEME VIJIJINI


Na Mwandishi wetu
Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, amesema tozo ya shilingi elfu moja  iliyopitishwa na Bunge kwa matumizi ya simu za mikononi hailengi kuwaumiza wananchi, bali mapato yake yatakwenda moja kwa moja kusaidia kueneza umeme vijijini.

 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari juzi na Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri Pinda ametoa kauli hiyowakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mjini Songea ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya wiki moja katika Mkoa wa Ruvuma, baada ya kuutembelea Mkoa mpya wa Njombe.

 
Amesema wanaopinga tozo hiyo, hawaitakii mema nchi kwani imepitishwa na bunge lililomalizika mwezi uliopita, ili fedha zitakazopatikana zisaidie katika mpango mkubwa wa kueneza umeme vijijini unaoendeshwa na Wakala wa Umeme Vijijini, REA. Kwa Mkoa wa Ruvuma pekee, vijiji vipatavyo 150 vitapatiwa umeme chini ya mpango huo.

 
Kabla ya mkutano wa hadhara, Waziri Mkuu alizindua Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi, VETA, cha Songea kinachodahili zaidi ya wanafunzi 500 na kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa ufundi stadi mbalimbali.

VIKUNDI VYA UJASIRIAMALI NI UKOMBOZI WA UCHUMI


 
Na:Edilitruda Chami
Wakazi wa mkoa wa Singida wameaswa kutotegemea ajira kutoka mashirika binafsi na serikalini badala yake kujiunga  na kuanzisha vikundi mbalimbali vya kijasiriamali ili kujikomboa kiuchumi.

Wito huo umetolewa na mwenyekiti wa mradi wa mafunzo woman society  mkoani singida bi. Amina Abubakari   wakati akizungumza na standard radio juu ya umuhimu wa kuunda makundi ya kijasiriamali kwa wanawake katika kujiendeleza kibiashara.

Bi. Amina amesema  lengo la mradi huo ni kuhakikisha  maambukizi ya virusi vya ukimwi hayaenei kwa kuwawezesha   wanawake kuwajibikaji na shughuli za kiuchumi, kuzuia ongezeko la  mimba za utotoni, pamoja na  kuwaweka walemavu na watoto wanaoishi katika mazingira magumu  katika hali nzuri ya maisha kwa kuwajengea uwezo wa kujiajiri wenyewe.

Amesema  kila mwananchi atambue umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu kwa kuwashirikisha wananchi wengine katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo, bila kubaguana kwa misingi ya dini, siasa au kabila.  Mradi wa mafunzo woman society  umeanziasha vikundi vya wajasiriamali wadogo wadogo 15 wanaoshughulika na kilimo, ufugaji na usindikaji wa vyakula, na wameweza kutoa mafunzo kwa vijana 273.

MAABARA SHULENI ZINAONGEZA WASOMI


Na:Prisca Rojin
Wakazi wa  kata ya Mandewa mkoani Singida wameombwa kushiriki vyema katika ujenzi wa maabara ili kuongeza idadi ya wasomi nchini.

 
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa kitongoji kata ya Mandewa, Bw. Juma Assi wakati akizungumzia hatua iliyofikiwa sasa katika ujenzi huo wa maabara.

 
Bw. Assi amewaomba watu wote wenye uwezo wa kufanya kazi kushiriki pamoja ili kupanua wigo wa elimu kwa vizazi vilivyopo na vijavyo ili kupunguza idadi ya watu wasiojua kusoma wala kuandika.

 
Aidha, amewashukuru baadhi ya wakazi ambao wanaonesha kujitoa kwa hali na mali na kuwataka wengine kuiga mfano huo ili kuendeleza kata ya Mandewa katika sekta ya elimu.  

 
 
 

Wakazi wa  kata ya Mandewa mkoani Singida wameombwa kushiriki vyema katika ujenzi wa maabara ili kuongeza idadi ya wasomi nchini.

 
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa kitongoji kata ya Mandewa, Bw. Juma Assi wakati akizungumzia hatua iliyofikiwa sasa katika ujenzi huo wa maabara.

 
Bw. Assi amewaomba watu wote wenye uwezo wa kufanya kazi kushiriki pamoja ili kupanua wigo wa elimu kwa vizazi vilivyopo na vijavyo ili kupunguza idadi ya watu wasiojua kusoma wala kuandika.

 

Aidha, amewashukuru baadhi ya wakazi ambao wanaonesha kujitoa kwa hali na mali na kuwataka wengine kuiga mfano huo ili kuendeleza kata ya Mandewa katika sekta ya elimu.  

 
 
 

TANZANIA NA CHINA KUENDELEZA USHIRIKIANO



Na:mwandishi wetu
Rais Jakaya Kikwete amekutana na ujumbe wa China unaoongozwa na mkurugenzi wa Idara ya ukaguzi wa mahesabu ya China Bw. Liu Jiayi.

Katika mazungumzo na uju mbe huo,  rais Kikwete amesema katika miaka ya hivi karibuni, mawasiliano ya ngazi ya juu na ya umma kati ya pande hizo mbili yamekuwa yakiimarishwa.

Viongozi wa China wametembelea Tanzania, na kusaini makubaliano ya ushirikiano na kutoa msaada na uungaji mkono mkubwa kwa Tanzania. Rais Kikwete ametoa shukurani kwa uungaji mkono unaotolewa na China kwa kazi ya idara ya ukaguzi wa mahesabu ya Tanzania, na kuelezea matumaini yake kuwa,  Idara ya ukaguzi wa mahesabu ya China itatoa uungaji mkono na msaada kwa wingi zaidi katika kutoa mafunzo kwa wataalamu, na kubadilishana uzoefu.

 
Bw. Liu Jiayi amesema Idara ya ukaguzi wa mahesabu ya China itafanya juhudi kadri iwezavyo kuhimiza ushirikiano wa fedha na miradi kati ya nchi hizo mbili.

Wednesday, July 17, 2013

RAIS ABDELAZIZ BOUTEFLIKA AREJEA NCHINI KWAKEWA ALGERIA BAADA YA KUPATA MATIBABU NCHINI UFARANSA


 
 
Na:Iran Radio
Habari kutoka Ufaransa zinasema, Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria amerejea nchini kwake baada ya kupata matibabu nchini Ufaransa.

 

Habari zinasema kuwa, Rais Bouteflika ameondoka nchini Ufaransa jana kuelekea nchini kwake. Rais huyo mwenye umri wa miaka 76 alipelekwa nchini Ufaransa baada ya kukumbwa na ugonjwa wa kiharusi mwishoni wa mwezi Februari ambapo awali alilazwa katika hospitali ya kijeshi ya Valde Grace na kupelekwa katika hospitali nyingine ya mjini Paris, Ufaransa.

 

Kutokuwepo kwake kisiasa nchini Algeria, kuliibua maswali mengi hasa kuhusiana na nafasi ya uraisi nchini humo. Hali hiyo ilivifanya vyama na makundi ya kisiasa yanayoipinga serikali inayoongozwa na Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria, vilitaka kufanyika uchaguzi kabla ya wakati kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, kutokana na kuugua rais huyo.

 

AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KOSA LA KUKUTWA NA NYARA ZA SERIKALI MKOANI SINGIDA


Na;Fatma Munah
 
Mkazi  mmoja wa kijiji cha Misughaa mkoani Singida amefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi wilaya  kwa kosa la kukutwa na nyara za serikali  kinyume cha sheria ya wanyama pori.

 
Akisomewa  mashtaka,   mshtakiwa  Bw Andrea Patric,  mwendesha mashtaka wa serikali sajent Lawrence mbele ya hakimu Bi Terrysoph Tesha  amesema  mshtakiwa  alikutwa na nyara za serikali tarehe 09 mwezi July mwaka 2012 majira ya saa kumi na nusu jioni katika kijiji cha Misughaa wilaya na mkoa wa Singida

 
Aidha sajent Lawrence amesema mshtakiwa alikutwa na kilo moja na nusu ya nyama ya digidigi ambayo thamani yake ni shilingi laki nne na elfu ishirini na tano ikiwa ni mali ya serikali.  

 
Mshtakiwa amekiri kosa na mahakama imemtia hatiani na kumhukumu kwenda jela kwa miezi mitatu au kulipa faini ya shilingi elfu hamsini, kama onyo kwa kuwa mshtakiwa ni mara yake ya kwanza kutenda kosa hilo.

MADIWANI WAGOMA KUSHIRIKI UCHAGUZI WILAYANI BUHIGWE MKOANI KIGOMA


 
 Na:Mwandishi wetu
 Madiwani watano wa Chama Cha Mapinduzi wilayani Buhigwe Mkoani Kigoma, wamesema hawatoshiriki uchaguzi wa kumpata mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, kutokana na ukiukwaji wa sheria uliofanyika.

Madiwani hao wametoa kauli hiyo kufuatia uchaguzi wa jina la atakaekuwa mgombea wa kiti hicho uliofanyika juzi wilayani humo kupitia chama hicho kudaiwa kufanyika kinyume na utaratibu.

Madiwani hao wamesema katika uchaguzi wa nafasi hiyo kupitia CCM zilitangazwa nafasi nne pamoja na kutakiwa kuwa na majina matatu ya wagombea lakini yalitangazwa majina mawili pamoja na nafasi 2 kitu ambacho ni kinyume na  kanuni za chama hicho

Mmoja wa madiwani hao Bw Alois Edward diwani wa kata ya Biharu amesema baada ya tukio hilo baadhi ya madiwani walihoji na hawakupata majibu kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi huo zaidi ya kutishiwa kupokonywa nafasi zao pamoja na kadi za uanachama ambapo wamesusia uchaguzi huo
.
Standard Radio imemtafuta katibu wa chama hicho mkoa wa kigoma Bw Mohammed  Nyawenga msimamizi wa uchaguzi huo, ili kuzungumzia tukio hilo na kudai kuwa hayupo tayari kuzungumza lolote na hata alipotafutwa kwa njia ya simu haikupokelewa.

MUUNGANO WA KAMPUNI ZA ULINZI NA JESHI LA POLISI KUTAIMARISHA UFANISI KATIKA KAZI


Na:Jonhson Soah
 
Kampuni binafsi za ulinzi mkoani singida zimeshauriwa kuimarisha ushirikiano na jeshi la polisi ili kuleta ufanisi.

 
Hayo yamesemwa leo na kamanda wa polisi mkoa wa Singida, ACP Geoffrey Kamwela wakati wa kikao na kampuni binafsi za ulinzi ofisini kwake, kwa lengo la kubadilishana taarifa juu ya usalama mkoani hapa.

 
Kamanda kamwela ameyataja mambo waliyokubaliana kuwa ni utaratibu wa kuendesha mafunzo ya darasani pamoja na ukakamavu kwa walinzi binafsi yatatolewa na jeshi la polisi.

 
Aidha Bw. Kamwela amezitaka kampuni binafsi kuajiri watu kulingana na uadilifu, na umri unaostahili na kuzishauri kampuni hizo zipitie jeshi la polisi ili kuhakikishiwa taarifa sahihi za waajiriwa.

 
Mkoa wa Sngida una kampuni za ulizni binafsi zipatazo 18 zilizosajiliwa kisheia.

KUUZA NYARA ZA SERIKALI KWA MASLAHI BINAFSI NI KOSA KISHERIA


 
Na;Prisca Rojin
 
Afisa mhifadhi wa wanyamapori halmashauri ya wilaya ya Singida Bw. Augustino Lorry,  amewataka wananchi kutoa taarifa pale inapogundulika mtu ameuza nyara za serikali kwa maslahi yake binafsi,  ili achukuliwe hatua za kisheria.

 
Kauli hiyo inafuatia mtu mmoja anayefahamika kwa jina la Hassan Jumannne mkazi wa mtaa wa Mamtanda Mandewa, anayetuhumiwa na wakazi wenzake kuhamisha maji kutoka  kwenye bwawa linalotumiwa na wakazi wa eneo hilo na kuuza vyura.

 
Afisa mhifadhi wa wanyamapori Bw. Lorry, amesema  kuwa mtu huyo amevunja sheria ya uhifadhi wa wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 ya kuuza nyara za serikali bila kibali.

 
Aidha Bw Lorry ametoa tahadhali kwa jamii nzima kulinda na kutunza wanyama pia kutouza nyara za serikali bila kibali kutoka kwa maafisa wa wanyamapori.

 

 

Tuesday, July 16, 2013

UMASKINI NI CHANGAMOTO KWA MAENDELEO YA BURUNDI




Na Iran Radio


Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa  kuisaidia nchi hiyo katika juhudi za kupunguza umasikini na changamoto zinazoikabili.

Wito huo ametolewa jana katika ufunguzi wa mkutano wa ufuatiliaji wa wafadhili wa Burundi ambao unafanyika kwa siku mbili mjini Geneva, Uswisi.

Aidha Rais huyo amewapongeza washirika kwa uungaji mkono na kusema kuwa tangu mwaka 2005 nchi ya Burundi  imepata maendeleo makubwa katika sekta mbalimbali, zikiwemo utawala bora, amani na usalama, masuala ya hali ya hewa, elimu, afya na miundo mbinu.

Ametaja changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi hiyo kuwa ni pamoja na  migogoro ya ardhi, ukuaji mdogo wa uchumi, utapiamlo, kilimo cha kisasa, ongezeko la kasi la idadi ya watu, ukosefu wa nishati pamoja  na mabadiliko kwenye sekta ya elimu.

Amesema nchi hiyo inahitaji kusaidiwa kuandaa uchaguzi ulio huru na  wa haki na utakaoshirikisha watu.

MGOGORO WA MPAKA WA ZIWA NYASA BADO UZI NI ULEULE KWA RAIS JOYCE BANDA



Na:Iran radio


Rais Joyce Banda wa Malawi amesema kuwa nchi yake haina nia ya kulegeza kamba katika mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa na Tanzania.

 
Kiongozi huyo ametoa msimamo huo baada ya kukutana na marais wa zamani Bw. Joachim Chissano wa Msumbiji na Bw. Thabo Mbeki wa Afrika Kusini ambao ni wajumbe maalum wa jumuiya ya SADC katika mgogoro huo.

 
Rais Joyce Banda amesema madai ya Tanzania kwamba inamiliki sehemu fulani ya Ziwa Nyasa si ya kweli na kwamba mpaka uko ufukweni mwa ziwa hilo.

 
Amesema nchi yake inafuatilia kwa karibu upatanishi wa SADC na kwamba isiporidhishwa na maamuzi ya jumuiya hiyo italiwasilisha suala hilo mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu ICJ.

 
Joachim Chissano na Thabo Mbeki wanatarajiwa kuelekea Tanzania na kukutana na Rais Jakaya Kikwete ili kujadili mgogoro. Tanzania inasisitiza kwamba mpaka wake na Malawi uko ndani kabisa ya Ziwa Nyasa. 

NCHI YA KENYA NA NIGERIA ZIMEONYESHA USHIRIKIANO WA KUPANUA WIGO WA KIBIASHARA


Na:Iran Radio
Serikali za Kenya na Nigeria zimekubaliana kupanua wigo wa ushirikiano katika sekta mbalimbali hususan biashara.

Hayo yamebainika kwenye mkutano kati ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na mwenzake Goodluck Jonathan wa Nigeria mjini Abuja. Viongozi hao wamesisitiza umuhimu  wa kuimarishwa biashara miongoni mwa nchi za Afrika huku Rais Kenyatta akisema sera za nje za serikali yake zitazingatia zaidi biashara na nchi za Kiafrika.

Rais Jonathan kwa upande wake amesema bunge la nchi yake litajadili njia za kupunguza urasimu ili kurahisisha biashara na Kenya. Rais Kenyatta yuko nchini Nigeria kuhudhuria mkutano maalum wa Umoja wa Afrika wa kujadili jinsi ya kupunguza maambukizi ya virusi vya HIV na ugonjwa wa Kifua Kikuu barani Afrika.

Mikataba ya ushirikiano kati ya nchi na nchi, inatarajiwa kusainiwa wakati marais wa nchi mbalimbali watakapokutana baada ya mkutano huo.

 

VIJANA WAMEONYESHA CHANGAMOTO KUBWA YA MAENDELEO ENDAPO WATAGOMBEA NAFASI MBALIMBALI ZA UONGOZI NCHINI


Na;Muss Mbeho
Vijana wa manispaa ya singida  wametakiwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi,  hasa kwa kipindi kijacho cha uchaguzi mkuu  ili kuleta changamoto za maendeleo kwa taifa.

Hayo yamesemwa leo na mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Singida Bw. Ibrahimu Kijanga wakati  akizungumza  na Standard Radio ofisini kwake kuhusu uwajibikaji wa vijana katika suala la uongozi.

 
Bw.  Kijanga amesema vijana wamepewa nafasi mbalimbali za uongozi katika jumuiya zao, kwa  lengo la kuwaandaa vijana kuwa viongozi wachapa kazi kwa sasa na kwa wakati ujao, katika sekta za serikali na sekta binafsi.

 
Aidha, Bw.  Kijanga amewataka vijana kutojiunga na makundi mabaya na kuepuka kutumika vibaya kama vile kushiriki maandamano ambayo si halali kisheria,  na badala yake wafanye kazi kwa bidii ili kupiga vita umasikini.

 

 

 

TANZANIA IMEONYESHA NIA YA KUOMBA MAMLAKA MAKUBWA ZAIDI KWA UMOJA WA MATAIFA ILI KULINDA AMANI HUKO DARFUR


Na;Iran radio
Tanzania imetangaza kuwa itauomba Umoja wa Mataifa ukipe mamlaka makubwa zaidi kikosi cha kimataifa cha kulinda amani huko Darfur (UNAMID) baada ya mauaji ya askari wa wanauhudumu katika kikosi hicho.

Msemaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kanali Kapambala Mgawe amesema kuwa Tanzania inafanya mazungumzo na Umoja wa Mataifa kuhusu uwezekano wa kikosi cha UNAMID,  kupewa mamlaka makubwa zaidi ya kujilinda dhidi ya makundi yenye silaha huko Darfur, magharibi mwa Sudan.

Wakati huo huo,  kamanda wa kikosi cha UNAMID Mohammed Bin Shampas amesema watu waliofanya shambulizi la Jumamosi iliyopita dhidi ya askari wa kikosi hicho huko Darfur walikuwa wamejizatiti kwa silaha na ametoa wito wa kuangaliwa upya uwezo na zana za kikosi hicho.

Askari saba wa Tanzania katika kikosi cha UNAMID waliuawa Jumamosi iliyopita na wengine 17 kujeruhiwa katika shambulizi la kushtukiza lililofanywa na watu waliokuwa na silaha dhidi ya kikosi hicho.  

 

WANANCHI MKOANI SINGIDA WAHIMIZWA KUHIFADHI CHAKULA




Na. Edilitruda chami

Wananchi mkoani singida wametakiwa kujifunza mbinu mbadala za  kusindika vyakula ili kuvihifadhi kwa matumizi ya baadae na kuepukana na njaa ambayo inaweza kujitokeza.

Akizungumza na standard radio meneja wa viwanda vidogovidogo SIDO mkoani Singida  Bi. Shoma Kibende amesema  endapo  wananchi watatumia mbinu za kuhifadhi vyakula na hata kufungasha kwa njia ambayo ni salama hapatakuwepo na upungufu wa vyakula.  

Amesema mkoa wa Singida unazalisha vyakula vingi kama vile  nyanya, matunda, mbogamboga, karanga  lakini vinaharibika mapema kutokana na watu kutojua njia sahihi za kuhifadhi vyakula kwa matumizi ya baadaye.

Aidha, amesema Sido ina mpango wa kuhakikisha mwananchi anajikita katika shughuli za kijasiriamali  kwa kutoa mafunzo mbalimbali ili kuongeza kipato chao  binafsi na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali pamoja na kujifunza mbinu za usindikaji. 

Jumla ya viwanda 76 vimefikiwa na SIDO katika kutoa mafunzo ya ujasiriamali na usindikaji bora wa vyakula na matunda, kama njia pekee ya kutokomeza njaa kwa siku za baadae

MAHAKAMA MKOANI SINGIDA YAFUTA KESI YA UTAPELI


Na MAZIKU MOTTO

 

Kesi iliyokuwa inamkabili Bw. Abdallah Ramadhani mkazi wa Puma manispaa ya Singida imefutwa na mahakama ya mwanzo Utemini kutokana na mlalamikaji Rajabu Ramadhan pamoja na mshtakiwa kushindwa kufika mahakamani.

 

Hukumu hiyo imetolewa na hakimu wa mahakama hiyo Bw Simon Njau, ambapo amesema mnamo tarehe 24 june mwaka huu, mshitakiwa Bw Ramadhan alikaidi wito uliotolewa na mahakama uliomtaka afike mahakamani hapo.

 

Bw Njau amesema kwa kitendo cha kukaidi wito wa mahakama ni kosa na ni kinyume cha sheria za nchi.

 

Mahakama hiyo imeamua kuondoa shauri hilo kutokana na mlalamikaji kushindwa kufika mahakamani ili atoe ushahidi juu ya tuhuma zinazomkabili Bw Ramadhan.