Wednesday, January 2, 2013

MILIONI 92 ZAJENGA MAABARA SINGIDA


Zaidi ya shilingi milioni 92.3 zimetumika kugharamia ujenzi wa maabara mbili katika shule ya sekondari ya Ipembe katika manispaa ya Singida mjini hapa.

Mkurugenzi wa manispaa hiyo,Mathias Mwangu aliyasema hayo juzi wakati akizungumzia zoezi la ujenzi wa maabara katika halmashauri hiyo.

Alisema kuwa kati ya fedha hizo, serikali kuu imechangia shilingi 80 milioni na nguvu kazi ya wananchi,imechangia shilingi 12,385,000.

Mwangu alisema wamejenga maabara hizo za biolojia na kemia,ili kuwasaidia wanafunzi kujifunza kwa vitendo masomo ya sayansi.

“Lengo kuu la kujenga maabara haya,ni kuwasaidia wanafunzi kujifunza kwa vitendo masomo ya sayansi,pia kuwafanya wanafunzi kuyapenda masomo ya sayansi na kuongeza kiwango cha ufaulu wao”,alifafanua.

Aidha,mkurugenzi huyo,alisema kuwa maabara hayo yatasaidia pia wanafunzi wa shule jirani zisizo na maabara kufika na kujifunza kwa vitendo masomo ya sayansi hususani kemia na biolojia.

Mwangu alitaja changamoto inayowakabili hivi sasa,ni kuendelea kununua vifaa muhimu vya maabara na pia kuanza ujenzi wa maabara ya fizikia.

Mkuu wa wilaya ya Singida,mwalimu Queen Mlozi,ameagiza kila sekondari ya kata,zihakikishe zinajenga vyumba vitatu vya maabara kwa kasi ile ile iliyotumika kujenga shule za sekondari za kata.

Hata hivyo uchunguzi wa blog hii umebaini kuwa, pamoja na jitihada hizo za serikali bado shule nyingi za serikali zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu wenye uwezo wa kufundisha masomo ya sayansi

No comments: