Na Boniface Mpagape.
Taarifa ya utekelezaji wa ilani
ya uchaguzi ya tangu mwaka 2005 hadi mwaka 2012, imedhihirisha kuwa mkoa wa
Singida umepiga hatua kubwa katika kutekeleza miradi ya maendeleo katika
kipindi hicho.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa
ilani hiyo jana kwa waandishi wa habari, wakuu wa wilaya za mkoa huo, na
wataalam wa sekretarieti ya mkoa, Mkuu wa mkoa huo Dr. Parseko Ole Kone amebainisha kuwa malengo mbalimbali
yamefikiwa.
Katika sekta ya utawala bora,
ameeleza kuwa mwaka 2005 mkoa ulikuwa na majimbo matano ya uchaguzi na mwaka
2012 kuna jumla ya majimbo manane ya uchaguzi.
Aidha wilaya mpya mbili
zimeanzishwa na kufanyamkoa wa Singida kuwa na jumla ya wilaya tano. Kata
zilikuwa themanini na nane na sasa zipo mia moja ishirini na nne. Kulikuwa na
vijiji mia tatu sitini na sita na sasa vipo mia nne arobaini na mbili.
Kuhusu sekta ya kilimo katika
kipindi hicho mkoa uliweka kipaumbele katika mazao ya chakula kama mtama, uwele, viazi vitamu, muhogo na
maharage mazao ambayo huvumilia ukame.
Mkuu huyo wa mkoa ametaja mazao ya biashara yanayolimwa mkoani humo ni alizeti, vitunguu, ufuta, pamba pamoja na zao la porini la asali. Taarifa hiyo imeonyesha
kuna mafanikio makubwa kutokana na ongezeko la uzalishaji toka mwaka 2005 hadi
2012.
Aidha Bw. Kone amesema mkoani
Singida kuna ongezeko kubwa la viwanda kutoka viwanda hamsini hadi kufikia
tisini, sambamba na idadi ya wafanyabiashara kuongezeka. Katika kipindi hicho pia sekta ya elimu
imeonyesha mafanikio makubwa kwani shule za awali, msingi, sekondari pamoja na
vyuo, imeongezeka.
Taarifa hiyo imetaja sekta ya
afya kuwa imeonyesha mafanikio kutokana na ongezeko la zahanati, vituo vya afya
na kwamba hospitali mpya ya mkoa inajengwa eneo la Mandewa na baadhi ya majengo
yamekamilika. Amesema mafanikio katika
chanjo kwa watoto yametokana na idadi ya watoto waliochanjwa kuongezeka na
kuufanya mkoa wa Singida kuwa wa pili kitaifa.
Mkuu huyo wa mkoa wa Singida
amesema vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano imepungua kutokana
na kusogezwa kwa huduma za afya kwa wananchi.
Amesema vifo vitapungua zaidi kutokana na kuanzishwa kwa chanjo mpya ya
magonjwa yanayosumbua watoto iliyozinduliwa mwishoni mwa mwaka uliopita.
Kuhusu mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI,
miongoni mwa watu elfu tano mia tisa na thelethini na tatu waliopima mwaka
2005, waliokuwa na maambukizi ni watu mia tatu na tatu. Amesema mwaka 2012 jumla ya watu elfu
ishirini na tatu na sabini na wawili walipima na mia nane tisini na tisa
walikuwa wamepata maambukizi ya virusi vya ukimwi, sawa na asilimia tatu nukta
tisa hali ambayo inaonyesha pia kuwa kiwango cha maambukizi kinashuka.
Taarifa hiyo imesema kuwa katika
sekta ya barabara kwa kiwango cha lami, mkoa wa Singida mwaka 2005 ulikuwa na kilomita
moja tu ya lami na sasa zaidi ya kilomita mia tatu sitini na nane, zimejengwa
kwa kiwango cha lami.
Kutokana na mkoa wa Singida
kukabiliwa na tatizo la uhaba wa maji kwa muda mrefu, mkoa umeongeza idadi ya
vyanzo vya maji na kwamba mradi mkubwa wa maji unatekelezwa chini ya udhamini
wa Benki ya kiarabu kwa kushirikiana na serikali. Amesema mradi huo unagharimu
dola za kimarekani milioni kumi na tisa.
Mkuu wa mkoa wa Singida Bw.
Parseko Kone amesema mradi huo utakapokamilika, jumla ya mita za ujazo ishirini na moja elfu
zitazalishwa kwa siku ambazo amesema zitatosheleza mahitaji ya maji kwa wakazi
wa Singida hadi mwaka 2025.
No comments:
Post a Comment