Wednesday, January 2, 2013

MAMILIONI YAIBWA IDARA YA AFYA SINGIDA

Na. Halima JamalSingida KESI inayomkabili mhasibu hospitali ya Mkoa Singida na walinzi watatu wa kampuni binafsi kuhusiana na wizi wa Sh. 15,976,650, imeanza kusikilizwa katika mahakama ya hakimu mkazi mjini hapa, kwa mganga mkuu wa mkoa kutoa ushahidi kuhusiana na tukio hilo.
 

Mhasibu huyo, Rahel Misai na walinzi watatu wa kampuni ya ulinzi ya Yange, Athumani Yohana, Juma Shabani na Rehema Hussein walishitakiwa kwa makosa manne ya wizi wa fedha hizo, zilizohifadhiwa ofisi ya kutunzia fedha, hospitali ya mkoa Singida.

 
Akitoa ushahidi, mganga mkuu mkoa wa Singida, Dk. Dorothy Kijugu aliieleza mahakama kuwa siku hiyo saa moja asubuhi wakati anajiandaa kwenda kazini, alipigiwa simu na mganga mkuu wa kituo kuwa ofisi ya mhasibu imevunjwa na fedha zimeibwa.
Akiongozwa na mwendesha mashitaka mratibu msaidizi wa polisi Shukurani Magafu,Dk. Kijugu alisema baada ya kufika hospitalini aliwakuta askari na katika kukagua walibaini kuvunjwa kwa milango yote minne hadi kufika chumba cha kuhifadhia fedha.
Alisema, baada ya kushuhudia hali hiyo, baadaye ilibidi mkaguzi mkuu wa ndani akague kwa kina, na taarifa yake ilithibitisha kuibwa kwa kiasi hicho cha fedha. Shahidi huyo aliikabidhi mahakama kielelezo cha nakala ya ukaguzi wa tukio hilo.
Hata hivyo katika maswali dhidi ya shahidi, washitakiwa walimuuliza, anadhani tukio hilo lilitokea majira ya saa ngapi, je anawafahamu washitakiwa hao?, muda wa walinzi kubadilishana zamu na wakati wa mhasibu kuingia na kutoka kazini.
Katika majibu yake, shahidi alisema anayepaswa kujua majukumu yao ni mganga mkuu wa kituo, badala ya yeye ambaye anahusika zaidi na utawala wa mkoa mzima, ikiwemo hospitali za wilaya, na juu ya muda wa mhasibu kutoka kazini aliieleza mahakama kuwa ni saa 9:30 jioni.
Kwenye shauri hilo, washitakiwa walifanya kosa hilo julai 13, 2012 usiku, wakihusishwa na mashitaka manne, ikiwemo kula njama kwa nia ya kutenda kosa, kuvunja usiku na kuiba fedha, wizi wa Sh. 15,976,650 mali ya hospitali mkoa na kosa la nne kushindwa kuzuia wizi huo.Shauri hilo limepangwa kuendelea kusikilizwa januari 3, 2013.

No comments: