Na Halima Jamal
MKUU wa wilaya ya Iramba mkoani Singida,Yahaya Nawanda,ameagiza kila mkazi wa wilaya hiyo kuwa mlinzi wa misitu, ili kuh mafadhi maliasili hiyo inayokabiliwa na tishio la kutoweka.
Nawanda ametoa agizo hilo wakati akizungumza kwenye kilele cha siku ya upandaji miti wilayani humo uliofanyika katika kijiji cha Mbelekese kata ya Ndago jimbo la Iramba magharibi.
Amesema uvunaji ovyo wa miti katika wilaya hiyo,umesababisha madhara mengi ikiwemo ukame mkali,uhaba wa mvua na unatishia wilaya hiyo kugeuka kuwa jangwa.
Alisema kila mkazi wa wilaya hiyo ni shahidi mzuri wa madhara makubwa yatokanayo na uvunaji huo usikuwa na uwiano na upandaji miti.
“Kwa hiyo mimi kama mkuu wa wilaya hii,sikubaliani kabisa na uvunaji huu.Kuanzia sasa ni marufuku mtu kukata mti.Kama mtu anataka kuni,akate matawi na si kuagusha mti mzima.Kwa hiyo,naagiza kuanzia sasa kila mtu awe ni mlinzi wa miti na akimwona mtu anakata,amzomee”,alisema Nawanda.
Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa wilaya,ameagiza pia kuwa suala la kuchangia maendeleo katika wilaya hiyo, ni la kufa na kupona.Mtu ambaye hataki kuchangia maendeleo ahame haraka wilayani humo na kwenda kuishi mahali watu hawachangii maendeleo yao.
“Niseme tu kwamba hata mtu akifariki dunia kama anadaiwa michango ya maendeleo yakiwemo ya sekta ya elimu,asizikwe hadi hapo michango anayodaiwa iwe imelipwa ndio azikwe.We mtu anafariki dunia huku akiwa ameaacha watoto wanne nani awagharamie”,alihoji.
Kuhusu ujenzi wa maabara,Dc Nawanda alisema kuwa kila shule ya sekondari ihakikishe inakamilisha ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara kabla ya juni 30 mwaka huu.
Kwa mujibu wa afisa maliasili na utalli wilayani Iramba,jumla ya vijiji 75 vinetenga maeneo kwa ajili ya hifadhi ya misitu ya asili yenye ukubwa wa hekta 25,652,shule 167 zimepanda miti kwenye maeneo yao yenye hekta 757.8,vijiji 28 vina mashamba ya miti yenye hakta 481.5 na taasisi 17 zina mashamba ya misitu hekta 30.
No comments:
Post a Comment