SHIRIKA lisilo la kiserikali la
Singida Non – Governmental Organizations Network (SINGONET), limetumia zaidi ya
shilingi 149.8 milioni kugharamia utekelezaji wa mradi wa kuimarisha mahusiano
kati ya wananchi na wabunge, madiwani na watendaji wa serikali.
Hayo yameelezwa juzi na mratibu wa
SINGONET, Maendeleo Makoye, wakati akitoa taarifa yake kwenye mdahalo mkubwa kwa
kuimarisha mahusiano ya wananchi na wabunge,madiwani na watendaji wa
serikali.
Alisema fedha hizo zilizotolewa na
shirika la The Foundation For Civil Society kugharamia mradi huo, ambao
umetekelezwa katika awamu nne kuanzia Septemba mwaka jana hadi Septemba mwaka
huu.
Makoye alisema kuwa mradi huo
ulilenga kuamsha ari ya ushiriki na ushirikiashwaji wa wananchi katika
kuchambua, kujadili na kutoa mapendekezo yao juu ya mchakato wa uandikaji wa
Katiba mpya ya Tanzania.
Aidha alitaja malengo mengine kuwa ni
kujenga na kudumisha uhusiano na ushirikiano kati ya asasi za kiraia na wananchi
na kushughulikia changamoto zinazoikabili jamii hasa katika upatikanajii wa
huduma za elimu, afya, upatikanaji wa maji na nishati.
Katika hatua nyingine, Makoye alisema
baadhi ya wabunge na Madiwani nchini, wameshindwa kuonyesha uwajibikaji wao kwa
umma kama inavyotarajiwa.
Akifafanua zaidi,Makoye alisema
wawakilishi hao wameshindwa kushiriki pamoja na kushirikisha jamii katika
kubuni, kupanga, kutekeleza na kusimamia mipango mbalimbali ya
maendeleo.
“Hakuna utaratibu ulio wazi juu ya
mijadala ya pamoja kati ya wananchi na wawakilishi wao. Kwa maana hiyo, wananchi
hawashiriki kuchangia maoni na mawazo ambayo Mbunge au Diwani anapaswa
awawakilishe katika taasisi za maamuzi”,alisema Makoye.
Mratibu huyo,
alisema
mapungufu hayo ya kimawasiliano, jamii imeshindwa kuwakilishwa
vilivyo na matokeo yake, serikali imeshindwa kutimiza ipasavyo mahitaji halisi
na matarajio ya wananchi wake.
No comments:
Post a Comment