Friday, January 25, 2013

KATIBA IWATAMBUE WALEMAVU WA NGOZI


Wajumbe wa kamati ya chama cha albino mkoa wa singida TAS, wamefanya semina ya mafunzo ya siku mbili katika ukumbi wa kituo cha walimu nyerere katika manispaa ya Singida yakuwawezesha kutambua haki zao na kutoa maoni kuhusu katiba wanayoitaka.

Akitoa mafunzo hayo Bw. Godwel Mwamakula ambae ni  mwanasheria ofisi ya kazi kwa mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa singida amesema kuwa walemavu wa ngozi ni lazima watambue haki zao za msingi, ili waweze kutoa maoni yao katika katiba itakayoundwa.

Bw. Mwamakula ameongeza kuwa katiba iliyopo haijaweka wazi haki anazohitaji kupata mlemavu wa ngozi hivyo katiba ijayo lazima iundwe tume itakayochunguza na  kuhakikisha viongozi wote wanatambua mahitaji ya makundi maalum wanakuwa waadilifu na mahakama ipewe uhuru wa kusikiliza madai ya haki za walemavu hao.

Akihitimisha semina hiyo, Bw Mwamakula amesema kuwa ulinzi shirikishi na polisi jamii ni kwa ajili ya usalama wa raia na mali zao,  hivyo watumie fursa hiyo kutoa taarifa wakiwa na tatizo lolote ili kuondokana na vitendo vya unyanyasaji katika maeneo wanayoishi na  kufikisha waliyopata kwenye semina kwa wenzao.

Kwa upande wao walemavu wa ngozi wamesema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile, ukosefu wa mafuta ya kulainisha ngozi zao, gharama za elimu, matibabu na kufanya kazi ngumu. Wameiomba serikali kupitia katiba itakayoundwa kuangalia changamoto hizo.

No comments: