Tuesday, July 23, 2013

WAHAMIAJI HARAMU WAFIKA KWA WINGI KATIKA WILAYA YA SIMANJIRO MKOANI MANYARA


Na:Mwandishi wetu
 
Wilaya ya Simanjiro iliyoko mkoani Manyara, inaongoza kwa kufikiwa na kukaliwa na wahamiaji haramu ikilinganishwa na wilaya nyiingine za mkoa huo.

Katibu Tarafa wa Moipo, Bw. Joseph Mtataiko, amesema hayo wakati akifungua warsha iliyoandaliwa na Idara ya Uhamiaji Mkoa, kuhusu ulinzi shirikishi kwa kuwatambua na kuwafichua wahamiaji haramu.

Amesema wilaya hiyo ni maficho ya wahamiaji haramu kutokana na mgodi wa machimbo ya madini wa Mererani, kwani kila siku wageni wapya wanaingia kutoka sehemu mbalimbali nchini hasa mikoani.

Aidha, amesema wilaya hiyo ni mapito ya wageni haramu waendao nchi za jirani za kusini mwa Tanzania. Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji mkoani Manyara, Ebros Mwanguku, amewataka wananchi wa wilaya hiyo kuwa makini kwa wageni wanaoingia kwa kutoa taarifa katika kituo cha polisi, ili wafanyiwe uchunguzi kuhusu uingiaji wao wilayani humo.

Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Manyara imeendesha warsha ya uhamiaji shirikishi ikishirikisha kamati za ulinzi na usalama, katika wilaya za Babati, Mbulu na Simanjiro na kumalizia na wilaya za Kiteto na Hanang’ ili kuimarisha ulinzi na hali ya usalama na amani mkoani humo.


 

No comments: