Monday, July 22, 2013

BASI LA MOHAMED TRANS LAPATA AJALI MJINI SINGIDA


 
Na:Edson Raymond
Abiria arobaini na watano wamenusurika kifo baada ya basi mali ya Kampuni ya Mohamed Trans lenye namba za usajili T 210 APG walilokuwa wakisafiria kutoka Dodoma kwenda Mwanza  kupasuka tairi la upande wa kulia na kuhama barabarani kwenye njia panda karibu na viwanja vya People’s Manispaa ya Singida.

 

Wakizungumza leo na standard radio mara baada ya ajali hiyo,  baadhi ya abiria wamesema imetokea muda mfupi baada ya kutoka katika stand mpya ya mabasi ya Singida ambapo walipofika eneo la round about basi hilo lilipasuka tairi na kuhama kutoka barabarani na kuingia kwenye mtaro ulioko jirani na eneo hilo.

 

Wamesema kuwa kabla ya ajali hiyo, alipita mwendesha pikipiki ambaye alikatisha ghafla mbele ya basi hilo na mara baada ya hapo basi hilo lilianza kuyumba na kuingia mtaroni.

 

Aidha kwa upande wa kondakta wa basi hilo ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake kwa madai kuwa si msemaji wa kampuni, amesema ajali hiyo imetokea kama ajali nyingine na kwamba basi hilo halikuwa katika mwendo kasi na kuongeza kuwa abiria wote wametoka salama bali kuna baadhi wamepata michubuko midogo midogo katika sehemu mbali mbali za miili yao.

 

No comments: