Tuesday, July 16, 2013

TANZANIA IMEONYESHA NIA YA KUOMBA MAMLAKA MAKUBWA ZAIDI KWA UMOJA WA MATAIFA ILI KULINDA AMANI HUKO DARFUR


Na;Iran radio
Tanzania imetangaza kuwa itauomba Umoja wa Mataifa ukipe mamlaka makubwa zaidi kikosi cha kimataifa cha kulinda amani huko Darfur (UNAMID) baada ya mauaji ya askari wa wanauhudumu katika kikosi hicho.

Msemaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kanali Kapambala Mgawe amesema kuwa Tanzania inafanya mazungumzo na Umoja wa Mataifa kuhusu uwezekano wa kikosi cha UNAMID,  kupewa mamlaka makubwa zaidi ya kujilinda dhidi ya makundi yenye silaha huko Darfur, magharibi mwa Sudan.

Wakati huo huo,  kamanda wa kikosi cha UNAMID Mohammed Bin Shampas amesema watu waliofanya shambulizi la Jumamosi iliyopita dhidi ya askari wa kikosi hicho huko Darfur walikuwa wamejizatiti kwa silaha na ametoa wito wa kuangaliwa upya uwezo na zana za kikosi hicho.

Askari saba wa Tanzania katika kikosi cha UNAMID waliuawa Jumamosi iliyopita na wengine 17 kujeruhiwa katika shambulizi la kushtukiza lililofanywa na watu waliokuwa na silaha dhidi ya kikosi hicho.  

 

No comments: