Monday, July 22, 2013

TOZO YA SHILINGI ELFU MOJA YA SIMU KUSAIDIA KUENEZA UMEME VIJIJINI


Na Mwandishi wetu
Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, amesema tozo ya shilingi elfu moja  iliyopitishwa na Bunge kwa matumizi ya simu za mikononi hailengi kuwaumiza wananchi, bali mapato yake yatakwenda moja kwa moja kusaidia kueneza umeme vijijini.

 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari juzi na Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri Pinda ametoa kauli hiyowakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mjini Songea ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya wiki moja katika Mkoa wa Ruvuma, baada ya kuutembelea Mkoa mpya wa Njombe.

 
Amesema wanaopinga tozo hiyo, hawaitakii mema nchi kwani imepitishwa na bunge lililomalizika mwezi uliopita, ili fedha zitakazopatikana zisaidie katika mpango mkubwa wa kueneza umeme vijijini unaoendeshwa na Wakala wa Umeme Vijijini, REA. Kwa Mkoa wa Ruvuma pekee, vijiji vipatavyo 150 vitapatiwa umeme chini ya mpango huo.

 
Kabla ya mkutano wa hadhara, Waziri Mkuu alizindua Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi, VETA, cha Songea kinachodahili zaidi ya wanafunzi 500 na kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa ufundi stadi mbalimbali.

No comments: