Monday, July 29, 2013

HASSAN MWINYI AWATAKA WANACHI KUZINGATIA MAFUNDISHO YA DINI ILI KUDUMISHA AMANI


Na:Mwandishi wetu
 
Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, amewataka Watanzania kuzingatia mafundisho ya dini zao ili kudumisha amani na utulivu nchini.

Rais Mwinyi ametoa rai hiyo jana wakati akihutubia katika hafla ya kuhitimisha shindano la kusoma Kurani iliyofanyika katika ukumbi wa viwanja vya Sabasaba, Dar es Salam, ambako alikuwa mgeni rasmi.

Shindano hilo liliandaliwa na taasisi ya Al-Hikma Education Centre ya jijini Dar es salaam na kuwashirikisha vijana wa Kiislamu kutoka katika nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Rais Mwinyi amesema ili kudumisha amani, utulivu na mshikamano wa taifa ni muhimu kwa vijana na wananchi kwa ujumla kusoma na kuzingatia mafundisho ya dini zao, na kwamba kwenda kinyume na mafundisho ya dini kunaweza kusababisha uvunjifu wa amani kama ilivyo katika nchi nyingine za Afrika.

Katika shindano hilo mshindi wa jumla ni Suleiman Omar Ally (10), kutoka taasisi ya Al-Hikma ambaye amewashinda wenzake tisa na kundi la waliohifadhi juzuu 30, na amezawadiwa shilingi milioni 10 na zawadi nyingine.

Washindi wengine ni Abdallah Juma katika kundi la waliohifadhi juzuu 20, na Anwari Yahya amekuwa mshindi katika kundi la waliohifadhi juzuu 10.

No comments: