Thursday, August 23, 2012

WAPINZANI WAMTETEA LOWASA


MWENYEKITI wa Chama cha United Peoples Democratic (UPDP), Fahmi Dovutwa, amemfananisha Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na Waziri Mkuu Mstaafu, marehemu Rashid Kawawa.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Dovutwa alisema Lowassa hana tofauti na Kawawa, ambaye katika uhai wake akiwa waziri mkuu alibeba lawama za Serikali katika utawala wa awamu ya kwanza.

Dovutwa ambaye mwaka 2010 aligombea urais, alisema Lowassa hakuhusika katika kashfa ya rushwa iliyotokana na mkataba tata wa Richmond na kwamba alijiuzulu uwaziri mkuu ili kulinda heshima ya Serikali na si vinginevyo.

“Mwalimu Nyerere alipata kutoa hotuba siku moja akisema kwamba: ‘Namshukuru sana mzee Rashidi Mfaume Kawawa, amenisaidia sana.
‘Mambo yote ambayo amekuwa akilaumiwa Kawawa niliyafanya mimi na yeye (Kawawa) alibeba tuhuma hizo kwa ajili yangu’, haya ni maneno ya Baba wa Taifa na hotuba zake hizi zipo,” alisema Dovutwa akimnukuu Mwalimu.

Dovutwa aliongeza: “Kwa kauli hiyo ya Baba wa Taifa ni wazi Lowassa hakuhusika na kashfa ya Richmond. Kwa sababu maamuzi ya kiutendaji wa Serikali yako mikononi mwa Baraza la Mawaziri ambalo mwenyekiti wake ni Rais.

“Waziri yeyote hana uwezo wala mamlaka ya kuamua jambo bila ridhaa ya Rais. Lowassa aliwajibika ili kuilinda Serikali ya CCM chini ya Rais Kikwete isianguke na kupisha uchaguzi mwingine,” alisema.

“Mwalimu Nyerere alielewa vizuri dhana ya uwajibikaji na Watanzania wengi hawakumwelewa Mwalimu Nyerere alipokuwa akiwarudisha baadhi ya watumishi ambao awali waliwajibika kwa tuhuma za kiutumishi.

“Kimsingi tuhuma alizokuwa amelaumiwa kiongozi mwandamizi wa Serikali zilikuwa ni tuhuma za kiongozi mkuu wa Serikali ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kuamua kufanya jambo au kulikataa.

“Ili kuilinda Serikali na kiongozi mkuu wa Serikali ndipo hutokea mtumishi mmoja wa Serikali kubeba lawama na tuhuma za wizara yake kwa manufaa ya Serikali yenyewe.

Hivyo dhana ya kuwajibika ilieleweka vizuri kwa Mwalimu Nyerere kuliko wasomi walio wengi wa ndani na nje ya CCM,” alisema Dovutwa.

Dovutwa alisema Lowassa ni kiongozi makini mwenye ujasiri ambaye aliweza kufanya mambo akiwa waziri mkuu, huku akiwatahadharisha wananchi kuwa makini na baadhi ya viongozi.

“Watanzania tusikumbuke kufanya mabadiliko ambayo huenda tukaondoa wala rushwa wadogo na kuingiza wala rushwa wakubwa zaidi,” alisema.

Dovutwa aliwataka Watanzania kutafakari juu ya mwenendo wa vyama vilivyoko bungeni, hasa kutokana na Bunge kuchafuka kutokana na kashfa ya rushwa inayowahusisha wabunge.

No comments: