Friday, August 24, 2012

WAHADZABE KUGAWIWA KITOWEO ILI KUFANIKISHA SENSA



Na. Halma Jamal
Singida

SERIKALI ya wilaya mpya  Mkalama mkoani Singida, imeahidi kutoa nyama pori ya kutosha kwa Wahadzabe wa kitongoji cha Kipamba kata ya Mwangeza, ili waweze kushiriki sensa ya kitaifa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika nchini kote agosti 26 mwaka huu.

Mkuu wa wilaya hiyo Edward Ole Lenga,amesema msaada wa nyama ya wanyama pori hiyo, utasaidia jamii ya Wahdzabe kubaki kwenye kaya zao kipindi chote cha sensa.

Akizungumza muda mfupi kabla ya kumkaribisha mkuu wa mkoa wa SIngida, Dk. Parseko Kone, awahamasishe  Wadzabe na wakazi wengine wa kata ya Munguli, kushiriki sensa,Lenga alisema msaada huo wa  nyama pori, unatokana na ombi liliotolewa na jamii hiyo ambayo chakula chake kikuu ni,nyamapori,mizizi,matunda pori na asali.

Akifafanua, alisema Wahdzabe hao wanaokadiriwa kufikia 227, wametoa ombi hilo ili wakati wote wa sensa wasiende porini kuwinda na badala yake wabaki kwenye kaya zao wakisubiri kuhesabiwa.

“Mheshimiwa mkuu wa mkoa, ndugu zetu hawa Wahdzabe, waliomba wapatiwe nyamapori ambayo ndiyo chakula chao kikuu, ili siku ya sensa wasiende kuwinda porini, kwa kweli endapo watapatiwa nyama hiyo, wamenihakikishia watabaki majumbani kusubiri makarani wa sensa”,alisema.

Mkuu huyo wa wilaya,alisema ombi hilo tayari limeishakubaliwa na maandalizi yote muhimu ya kuwinda wanyama pori siku moja kabla ya siku ya sensa, yamekwisha kamilika.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa Dk. Kone, yeyey alitoa msaada wa chakula chenye uzito wa zaidi ya tani moja, ambacho kitakidhi mahitaji kuanzia sasa hadi zoezi la sensa litakapokamilika.

“nimewaletea hiki chakula amacho ni mchele uliochangwa na vyakula mbali mbali ikiwemo pia mboga mboga ,kutoka shirika lisilo la kiserikali la International  Africa Outreach la nchini  Marekani. Chakula hiki  ni kizuri mno, kina virutubisho vingi”alifafanua Dk.Kone. 

Alisema kwa hali hiyo, kipindi chote cha sensa, hapatakuwepo na haja kwenda porini kutafuta wanyama pori, asali, matunda pori au mizizi.

Katika hatua nyingine,aliwataka wahakikishe kila mmoja anahesabiwa mara moja tu, kwa madai kuwa wakishafahamika idadi yao na hali zao za  maisha, itasaidia serikali kujipanga namna bora  ya kuwahudumia na kuwaletea maendeleo.

Wakati huo huo Dk. Kone, alisema pamoja na kunid la wawindaji, pia makundi mengine ya wavuvi, wachungaji wanaohama hama hama, watafutaji madini na baadhi ya wakulima ambao wana mashamba yaliyo mbali na makazi au makambi yoa ya kawaida, warejee kwenye kaya na makambi yao,ili waweze kuhesabiwa siku ya sensa.

No comments: