Friday, August 17, 2012

VIONGOZI WA DINI SINGIDA WAHIMIZA WAUMINI KUSHIRIKI SENSA 2012


Na. Elisante John na Everista Lucas
Singida

WAUMINI wa madhehebu mbalimbali yab dini Mkoani Singida wameaswa kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa ya watu na makazi, mwishoni mwa mwezi huu, ili kuiwezesha serikali kupanga na kutekeleza vyema mipango ya maendeleo.

Viongozi hao mashekhe, wachungaji na wawakilishi wa madhehebu ya dini mbalimbali walitoa rai hiyo juzi, kwenye mkutano wao na mkuu wa Mkuu Mkoa Singida, Dk. Parseko Kone, uliofanyika ukumbi wa mikutano, jengo la ofisi ya mkuu wa Mkoa.

Walikemea tabia ya baadhi yao kupinga zoezi hilo kwa madai kuwa linakwenda kinyume na imani za dini zao, jambo ambalo ni uongo,lenye lengo kupotosha na kukwamisha jamii kushiriki sensa ya watu na makazi.

Mwenyekiti wa BAKWATA Wilaya Singida mjini Hamisi Kisuke na mchungaji Amos Maghas kutoka kanisa la FPCT, walitoa wito kwa waumini wao kushiriki zoezi hilo, ili kufanikisha upatikanaji takwimu sahihi, kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Kwa upande wake mkuu wa Mkoa Dk. Kone alishukuru msimamo wa viongozi hao katika kushirikiana na Serikali, lakini akawataka kukemea na kufichua wote wenye nia mbaya kukwamisha zoezi hilo.

Aliwataka wale wanaotumia kigezo cha udini kugomea zoezi hilo waache mara moja, badala yake washiriki kikamilifu kwenye zoezi hilo lenye lengo la kupata takwimu sahihi zitakazosaidia kupanga mipango ya maendeleo.

Dk. Kone alisema zipo dalili kwa baadhi ya viongozi kuhimiza waumini wao wasishiriki sense, jambo linalohatarisha zoezi hilo.

Alisema ni vyema viongozi hao wakaweka mkazo na kuwaelimisha waumini wao ili washiriki vyema zoezi hilo, badala ya kuvuruga kwa lengo la kuleta mtafaruku na kuvunja umoja na mshikamano uliopo baina ya Watanzania.

Alisema Watanzania wasikubali kudanganywa au kukubali imani potofu na kukataa kuhesabiwa kwani zoezi hilo ni kwa faida yao na kwamba kutakuwa na madodoso ikiwemo la jamii, wasafiri, waliolala nyumba za kulala wageni, waliolazwa hospitalini na wasio na makazi maalumu.

No comments: