Wednesday, August 15, 2012

MAKALA KUTOKA SINGIDA TANZANIA-SENSA 2012


Na. Everister Lucas

Singida Tanzania



“Hawa nao wanaongea nini? Mie wala hawatanihesabu kabisaaa; tena wakome waishie huko huko kwangu hata wasije. Tena zoezi lenyewe linaanza usiku! Hawapati mtu.” Nilimsikia rafiki yangu akibwabwaja huku kakodolea macho kioo cha Runinga; Nikamuuliza kulikoni mbona alikuwa akiiongea peke yake?



Baadae kidogo nilibaini kuwa katika kipindi cha jambo leo cha TBC 1 ambacho kilikuwa hewani walikuwa wakitoa  mada juu ya zoezi zima la sensa ya watu na makazi na jinsi zoezi hilo litakavyofanyika. Hali hii ilinifanya nimuulize shoga yangu huyo ni nini asichokijua kuhusu sensa. Nae akanambia kuwa haoni umuhimu wa kuhebiwa na kudai kuwa huo ni usumbufu.



Hili likanirudisha nyuma na kunikumbusha kikao cha hivi karibuni kati ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk.Parseko Kone na viongozi wa madhehebu ya dini hapa mkoani Singida juu ya sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika nchini pote usiku wa kuamkia Agosti26 mwaka huu na kudumu kwa muda wa siku sabana, akisisitiza kuwa watakaohesabiwa ni wale wote watakaokuwa wamelala katika kaya yoyote nchini Tanzania usiku wa kuamkia tarehe hiyo.



Tumesikia vyombo mbali mbali vya Habari vikiripoti juu ya changamoto zinazojitokeza katika zoezi zima la sensa kwa imani potofu au kwa kutokujua umuhimu wa zoezi hili.



Kuna baadhi ya watu pia wanasambaza ujumbe kwa njia ya vipeperushi na ujumbe mfupi wa maneno wa simu kuwashawishi wasijitokeze kuhesabiwa.



Na hili lilidhihirishwa na Dk. Kone huku akisoma kivuli cha habari iliyochapishwa na wanaharakati wa dini ya Kiislamu na kutolewa katika gazeti la raia mwema likiwahamasisha waislamu kutoshoiriki katika sensa.



Akiendelea kusoma ujumbe huo ambao unatuhumu kuwa toka enzi za ukoloni idadi ya waislamu ilikuwa ni asilimia sitini lakini kadiri sensa inavyoendelea idadi hiyo inazidi kupungu.



Hata hivyo kutokana na uzito wa suala hili; ilimlazimu Kone kuwataka maafisa wa usalama waliohudhuria kikao hicho kulifuatilia suala hili kwa ukaribu hata kumpata muhusika ili hatua za kisheria zichukuliwe juu yake.



Kwa upande wao viongozi wa dini ya Kiislamu wakionesha wazi kusikitishwa kwao na ujumbe huo, kwa nyakati tofauti tofauti walikemea vikali kitendo hicho na kuahidi kuendelea na hamasa zaidi kwa waumini wao juu ya umuhimu wa sensa.



“Zoezi la kuhesabu lilikuwepo toka enzi za Mtume Mohamad(S.A.W) ambapo viongozi walitakiwa kupata idadi kamili ya Waislamu kwaajili ya kufanya mipango ya maendeleo.” Shekhe Issah Nassor.



Shekhe Issah alizidi kufafanua kuwa haoni tatizo juu ya zoezi hilo kwa vile ni agizo pia kutoka kwa Mungu na pia ni kwa maendeleo ya nchi. Pia alisisitiza kuwa yeye binafsi yuko kwenye ziara za uhamasishaji juu ya sensa ya watu na makazi na kumuahidi Kone kuwa na amani na zoezi litafanikiwa.



Kwa upande wa viongozi wa dini ya Kikristo hawakusita kupongeza viongozi w enzao wad ii ya Kiislamu kwa kitendo cha ujasiri walichokionesha kwa kulikemea wawzi wazi kundi hilo la wanaharakati wanaotaka kuvuruga zoezi la sensa. Mwakilishi kutoka kanisa la sabato pia alisisitiza kuwa sensa ilikuwepo toka enzi za kuzaliwa kwake Yesu Kristo ambapo Yuda aliamuru watu wahesabiwe.



“ Tunachokifanya ni kile ambacho pia kipo katika maandiko matakatifu. Ninyi ni walimu wazuri na mnakubalika katika jamii. Mimi nadhani sijawatwisha mzigo mzito kwakuwa mmesema kuwa sensa ni sheria na ni amri.”Kone

No comments: