Tuesday, October 2, 2012

WANAFUNZI WAPONGEZWA UTUNZAJI WA MAZINGIRA SINGIDA

Na Daud Nkuki
Singida

Shule ya Sekondari Mtinko katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida imepongezwa kwa jitihada za utunzaji wa mazingira.

Pongezi hizo zimetolewa na Afisa Tarafa wa Mtinko Rajabu Njiku, alipokuwa akikabidhi vyeti kwa wanafunzi 114 wanaohitimu elimu ya kidato cha nne, katika sherehe za mahafali ya shule hiyo, yaliyofanyika hivi karibuni.

Katika juhudi za kuboresha mazingira kwa kushirikiana na wazazi shule inaonekana yenye madhari nzuri ya kupendeza kwa upandaji miti katika kipindi cha miaka saba tangu ianzishwe mwaka 2006.

Shule imefanikiwa kujenga matundu ya vyoo 26 yanayokidhi haja ya wanafunzi na waalimu. Pia inayo nyumba mbili za walimu na vyumba kadhaa vya madarasa.

Pamoja na mafanikio hayo, bado inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo upungufu wa waalimu wa sayansi na hisabati, vifaa vya maabara, vitabu vya kujifunzia na kufundishia, na ukosefu wa umeme shuleni hapo.

Katika risala yao wahitimu hao wamependekeza shule hiyo ipatiwe umeme, maabara, nyumba za walimu ziongezwe na ukomeshwaji utoro wa wanafunzi udhibitiwe.

Mkuu wa shule hiyo Honorata Mbiaji, amewaonya wahitimu hao kutojichanganya na vitu vitakavyotia aibu shule ilaumiwe. Wala wasilete aibu kwa jamii, huko wanaporudi vijijini na mitani.

Kwa mara ya kwanza katika sherehe hizo wazazi waliweza kuchanga papo hapo jumla ya shs. 65,000/= kwa ajili ya kuwapongeza wahitimu hao.

No comments: