Tuesday, October 2, 2012

DALADALA NA MAISHA YETU TANZANIA




Na:
Matinde  Nestory
ARUSHA

Mpenzi msomaji wa makala hii ni wazi kwamba siku zote tunapoongelea vitu muhimu vinavyomsaidia mwanadamu katika maisha yake kamwe huwezi kusita kutaja neno usafiri,usafiri ni nyenzo maalum sana katika kukuza au kuimarisha maisha ya mwanadamu kwani husaidia katika shughuli za hapa na pale.
Ninapozungumzia usafiri ni vitu vyote ambavyo vitakusaidia au kukufikisha mahali unapotaka mfano pikipiki,baiskeli,gari meli na ndege mara nyingi watu wengi wamezoea kutofautisha  vyombo hivi vya usafiri kwa kuvipa majina ya usafiri wa nchi kavu, majini na angani.
Ni wazi kuwa kila mwanadamu anaridhika na uwepo wa kuwa na usafiri katika mazingira anayoishi kwani ni msaada mkubwa kwa kila mwananchi hasa katika nchi masikini kama Tanzania,kwa hiyo basi ni vyema kuvitunza vizuri vyombo hivi ili viendelee kutusaidia katika maisha ya kila siku.
Ukweli ni kwamba usafiri umeendelea kuleta mabadiliko makubwa katika nchi hii na maendeleo yanaendelea kushika hatamu.Pia usafiri umeweza kutuunganisha na mataifa mbalimbali pindi tunapoingiza bidhaa au kupeleka bidhaa nje ya nchi.
Mpenzi msomaji ukweli ni kwamba usafiri umekuwa daraja imara kwa wakulima kwani usafiri huo huo umeweza kuwasaidia katika kilimo watu wengi wamezoea kuona kuwa usafiri kama trekta,ni usafiri wa kawaida lakini kwa wakulima wanachukulia kama nyenzo au pembejeo za kilimo na kuwanufaisha katika sekta ya kilimo.
Tukiangalia hata kwa upande mwingine tunaweza kuona kuwa pato la taifa linaendelea kukua kutokana na kwamba iwapo wakulima wataendelea na kilimo na  kutumia usafiri wa trekta katika kilimo basi ni wazi kuwa wataweza kurahisisha kazi zao za kilimo na hatimaye kutafuta soko mapema.
Ninaweza kuthubutu kusema kuwa kuna baadhi ya watu wanapenda kudharau usafiri wa baiskeli lakini si sahihi kwani kuna baadhi ya mikoa kama shinyanga,tabora hutumia aina ya usafiri wa baiskeli kama vyanzo vya kujipatia fedha kwa kubeba abiria kutoka sehemu moja hadi nyingine ambapo wengi wao hutumia baiskeli kusafirisha mizigo kutoka mashambani.
Hivyo kutokana na hali hiyo imesaidia watu wengi wa ukanda  huo kujiendeleza kimaisha maana usafiri wa baiskeli umeonekana ndio muhimili kwa vijana wengi wasio kuwa na ajira maana ndio kimbilio la watu wengi katika mikoa hiyo ya shinyanga na tabora.
Hata hivyo naweza kuipongeza serikali kutokana na kuruhusu nchi za jirani katika kuingiza au kupokea aina nyingi za usafiri zikiwa zimetengenezwa kwa tecknolojia nzuri na za kisasa kwani zitaweza kuwasaidia wananchi wengi kujiendeleza kiuchumi na kuondokana na umasikini hasa kwa vijana.
Tumekuwa tukishuhudia vijana wengi kujikita katika kuendesha vyombo mbalimbali kama vile pikipiki ambazo zimechukua nafasi kubwa kwani vijana wengi wamepata ajira katika kujikwamua katika janga hili la umasikini pamoja na hayo pikipiki zimesaidia vijana kutokaa vijiweni bila ya kazi yoyote na kuondokana na utegemezi wa familia.
 Nimekuwa nikijiuliza maswali mengi,hivi kungekuwa hakuna usafiri,tungefahamiana vipi na mataifa mengine? Au watu wangeishi vipi pasipo kutembeleana na ndugu zao,na je ingekuwa vipi kwa wagonjwa waishio mbali na zahanati,au hata ukijiuliza mpenzi msomaji ingekuwa vipi kwa serikali endapo viongozi hao wakitaka kutembea majimboni kwao kwa kuangalia hali ya usalama wa raia wao.
Ndugu msomaji kutokana na maswali hayo yanaweza kuleta majibu ya kuwa kusingekuwa na maendeleo yoyote kwani bila usafiri hakuna kitu chochote ambacho kingefanyika katika dunia hii.
Pia serikali inatakiwa iangalie suala hili la miundo mbinu kwa hali na mali ili kusiwepo na dosari yoyote katika usafirishaji wa bidhaa ndani na nje na hata hivyo kushughulikia kwa leseni za watumiaji wa vyombo vya moto ili kuepusha usumbufu kwa watumiaji wake.
Ni vema serikali itambue kwa kina aina ya vyombo vya usafiri vyenye manufaa ili vitusaidie katika maendeleo na kuangalia vyombo vya usafiri ambavyo vimetengenezwa kwa teknolojia ya kisasa na kuepuka kuingiza vifaa vya usafiri ambavyo ni feki kwani vinaweza kurudisha nyuma kimaendeleo  na hata kuleta madhara katika jamii yetu.

No comments: