Monday, October 8, 2012

CCM WALALAMIKIA WANACHAMA KUTOLIPA ADA ZA UANACHAMA


Baadhi CCM wakicheza ngoma ya Kinyaturu kufurahia jambo wakati wa sherehe ya kumuaga kiongozi wao wa tawi la Mandewa mnjini Singida
Na Boniface Mpagape na
Edilitruda Chami.

Aliyekuwa Katibu wa CCM tawi la Mandewa kwa kipindi cha miaka kumi na mbili Bw.  Juma Mandi ameagwa rasmi tarehe 6 Oktoba 2012, baada ya kushinda katika uchaguzi wa ndani wa Chama uliofanyika tarehe 27 Julai 2012, na kupata wadhifa wa Katbu wa CCM Kata ya Mandewa iliyopo mjini Singida.
Risala iliyosomwa katika hafla fupi ya kumuaga iliyofanyika katika ofisi ya CCM tawi la Mandewa, ilimpongeza Bw. Mandi kwa kuchaguliwa kushika wadhifa huo mpya na kumtakia kila la kheri katika majukumu yake mapya.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Katibu wa itikadi, siasa na uenezi wa CCM wilaya ya Singida mjini Bw. Jumanne Hussein Rajab ambaye aliutumia sherehe hizo kuwakumbusha wanachama wa chama hicho kulipia ada ili waendelee kuwa wanachama hai  pamoja na kuzingatia umuhimu wa kuhudhuria vikao  vyote, sambamba na kuzingatia katiba ya chama chao kwa kuwa ndiyo mwongozo wao.
Akizungumzia shughuli za maendeleo ambazo zimekwishafanyika katika Kata ya Mandewa, Bw. Rajab amesema shule ya sekondari ya kata imejengwa, barabara za mitaa zimechongwa, pamoja na mradi wa maji unaoendelea kujengwa ndani ya kata hiyo, yote hayo yamefanyika ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM.
 Aidha, amewahimiza wakazi wa Kata ya Mandewa kujitokeza kwa wingi ili kushiriki kutoa maoni ya mabadiliko ya Katiba, ambapo tume ya kukusanya maoni  juu ya mabadiliko ya Katiba itafanya mkutano katika kata ya Mandewa tarehe kumi na nane mwezi Oktoba 2012. Amesema mkutano huo utafanyika katika eneo la Ginnery kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa sita mchana.
Katika hafla hiyo pia viongozi mbali mbali wa Kata ya Mandewa akiwemo diwani wa kata hiyo Bw. Shaban Kiranga amesema Kata hiyo inazidi kupata maendeleo hasa kuwepo kwa kituo pekee cha Standard Radio mkoani Singida, kilichopo katika kata hiyo.  Ameikaribisha Standard Radio katika kata yake na kuahidi kutoa ushirikiano wa dhati, ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana katika kata ya Mandewa kwani kutakuwa na vipindi mbali mbali vya kuelimisha umma.  Amesema upatikanaji wa habari utaleta maendeleo katika kata hiyo na mkoa wa Singida kwa ujumla.
Kiongozi mwingine aliyehudhuria katika hafla hiyo, ni Mtendaji wa kata ya Mughangha iliyopo mjini Singida, Bw. Jumanne Athuman Nkii.  Kwa upande wake amewaasa wanachama wote wa CCM kuacha tabia ya kutohudhuria vikao kwani kupitia vikao wanapata maelekezo mbali mbali ikiwa ni pamoja na kukosoana kwa lengo la kukifanya chama kiendelee kuwa hai.  Aidha, amesema ni kosa kutojibu tuhuma zinazotolewa na vyama rafiki (Pinzani) kama zina ukweli au kukanusha.

Akitoa shukurani, aliyekuwa  katibu wa CCM tawi la Mandewa  Bw. Jumanne Mandi  amesema  ushirikiano aliokuwa akipewa katika wadhifa wake wa zamani basi uendelee kutolewa  ndani ya kata  hiyo ambayo ni kubwa  kuliko tawi.  Amewataka viongozi wote washirikiane na kupendana na kuwaomba wakazi wa Mandewa kuitumia  Standard Radio iliyo katika eneo lao.

No comments: