Sunday, October 21, 2012

MINADA MKOANI SINGIDA NA HATAARI KWA MAZINGIRA NA AFYA

Na Edilitruda Chami
 
Wengi tumekuwa tukijiuliza maana halisi ya neno mazingira, ila tafsiri zimekuwa ni nyingi wengine husema ni kitu chochote kinachomzunguka binadamu, wengine husema ni sawa na usafi huku wengine wakihusisha pia uoto wa asili yaani nyasi na miti, vyanzo vya maji, mito na milima.
 
Katika eneo la mnadani mkoani Singida hali inaendelea kuwa mbaya zaidi siku hadi siku kutokana na mazingira kuwa machafu huku maji ya kusafishia vyombo na  mazingira yakizidi kuadimika siku hadi siku.  
 
Ulevi ,uchafu, uhaba wa maji, huku omba omba wakiwa wametanda kila upande, yote haya yamo katika soko la mnadani njia panda ya kwenda Arusha-Makyungu mkoani Singida. Biashara ya pombe za kienyeji imechukua eneo kubwa la soko tofauti na bidhaa nyingine, omba omba nao kila jumamosi wanahamia katika soko hilo kwa lengo la kutafuta ridhiki ili kujikimu na hali ngumu ya maisha, wengi wao wakiwa ni wazee pamoja na watoto wadogo.           Bi. Edilitulda Chami, Mwandishi wa habari
 
Mazingira ya soko hilo yamekuwa kero kutokana na uchafu na harufu mbaya ya pombe za kienyeji maarufu kama Mtukuru ( lugha ya Kinyaturu ) ambazo zimekuwa zikinyweka katika hali ya uchafu wa hali ya juu. Pombe hiyo ya kienyeji imekuwa ikitumika kama maji ya kunywa kwani hata watoto wadogo hununua maandazi na pombe hiyo kwa lengo la kupunguza kiu na njaa.  Ni vyema sana kulinda tamaduni zetu kama matumizi ya vyakula, vinywaji na mengineyo, lakini usafi uzingatiwe!
 
 
Hali hii si kwamba imeonekana kwa mwandishi wa habari tu, eneo la mnadani Singida kutokana na umaarufu wake pia hutembelewa na maafisa wa ngazi mbali mbali wa serikali ambao kila jumamosi huhudhuria hapo kunywa pombe na kula nyama choma na supu. Wengine wanashiriki hata katika mlo wa mchana katika eneo hilo, najiuliza je hawaoni hali hii?
 
Waswahili walisema, usipoziba ufa basi jiandae kujenga ukuta. Endapo utatokea ugonjwa wowote wa mlipuko huenda ukagharimu maisha ya watu ambayo hayalinganishwi au kuthamanishwa na chochote hapa duniani.
 
 

No comments: