Monday, October 15, 2012

CHF YATOA SOMO KWA MADIWANI SINGIDA

 
Na. Elisante John, Singida.
 
MADIWANI wa wametakiwa kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF), ili wanufaike na huduma bora za tiba, wakati wanapougua.
Changamoto hiyo imetolewa na afisa operesheni, bima ya afya (NHIF) mkoa wa Singida, Isaya Shekifu, wakati akijitambulisha kwa madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Singida.
Aidha Shekifu amewaomba madiwani kujiunga na mfuko huo, ili wao na familia zao waweze kunufaika na huduma zinazotolewa na CHF.
Amesema kutokana na ukweli kuwa wananchi wengi hawana uwezo mkubwa kifedha, njia nzuri na ya uhakika kupatiwa tiba sahihi wanapougua, ni kujiunga na mfuko huo.
Shekifu amesema ili kaya ijiunge na mfuko huo, inapaswa kulipa Sh. 5,000, kisha baba, mke na watoto wanne walio na umri chini ya miaka 18, watatibiwa kwa muda wa mwaka mmoja, bila ya kutozwa gharama zingine.
Amezitaja baadhi ya huduma zinazotolewa na mfuko huo kuwa ni pamoja na ada ya kujiandikisha na kumuona daktari, gharama ya uchunguzi wa afya, vipimo 143 na gharama za upasuaji mkubwa na mdogo.
Huduma zingine ni gharama ya dawa zote zilizoidhinishwa na wizara ya afya na ustawi wa jamii, mafao ya vifaa saidizi na huduma ya matibabu ya macho, ikiwemo pia upasuaji  husika.   

No comments: