Ni miaka 13 sasa tangu mwalimu Julius Kambarage Nyerere aage Dunia baada ya kuugua na kulazwa katika hospitali ya St. Joseph jijini London
Katika kuadhimisha kumbukumbu ya Mwl. Nyerere mambo mengi hufanyika; miongoni mwa mambo hayo ni matembezi ya vijana, kuzima mwenge wa Uhuru pamoja na hotuba mbalimbali za viongozi wa kitaifa kuhusu Umoja na mshikamano wa watanzania
Ni dhahiri kuwa kila mtanzania analo neno la kusema kuhusu Nyerere, Wapo wanaosema kuwa Nyerere ni Baba wa Taifa, wapo wanaotamka kuwa Nyerere alikuwa mbabe na mkorofi, wapo wanaoeleza kuwa Nyerere alipenda usawa na haki kwa kila mtanzania
Standard Radio imefanya mahojiano na watu mbalimbali ili kujua nini hisia zao kuhusu mwalimu Nyerere, maoni ni mengi lakini Khadija Mahamba ambaye ni mwanachuo wa chuo cha taaluma ya Habari cha DSJ (Dar es Salaam School of Journalism) anasema kuwa Nyerere aliacha pengo kubwa nchini Tanzania
“Enzi za Mwalimu kila kitu kilikuwa kinaenda kwa usawa bila ubaguzi; lakini katika miaka 13 tangu afariki UKABILA na UDINI umeshamiri miongoni mwa watanzania
Tunapotafakari na kuadhimisha miaka hiyo ya kifo cha Nyerere ni vema basi Serikali, wanasiasa na wananchi wengine tukafikiria njia mbadala wa kutimiza malengo yetu bila kuchochea ubaguzi, udini na kuacha ubinafsi ambao ni chanzo cha ufisadi na migogro miongoni mwa jamii yetu.” Khadija Mhamba DSJ
Standard Radio tunaunga mkono maoni haya.
1 comment:
Mwalimu Nyerere ni miongoni mwa viongozi nguli ambao misimamo yao iliweza kujulikana bayana katika anga za kitaifa na kimataifa. Hakupenda kujipendekeza kwa matajiri kama viongozi wetu wa sasa. Alikuwa muwazi na msema ukweli hata mbele ya mataifa makubwa kama Marekani na Uingereza na kutokana na hali hiyo ilimfanya aonekane kama kiongozi pekee duniani. Wakati tunatafakali kifo chake ni bora tujisahihishe kila mmoja wetu utu wetu usinunuliwe na mtu ili tuweze kutumia haki yetu ya kikatiba ya kuwa na uhuru wa kuamua mambo yetu kama nchi. Mwl.aliwatetea sana wakulima wadogowadogo na alipambana dhidi ya dhuluma ndio maana akaja na azimio la arusha na miiko ya uongozi.
Post a Comment