Wengi tumekuwa tukijiuliza maana halisi ya neno mazingira,
ila tafsiri zimekuwa ni nyingi wengine husema ni kitu chochote kinachomzunguka
binadamu, wengine husema ni sawa na usafi huku wengine wakihusisha pia uoto wa
asili yaani nyasi na miti, vyanzo vya maji, mito na milima.
Katika eneo la mnadani mkoani Singida hali inaendelea kuwa
mbaya zaidi siku hadi siku kutokana na mazingira kuwa machafu huku maji ya kusafishia
vyombo na mazingira yakizidi kuadimika
siku hadi siku.
Ulevi ,uchafu, uhaba wa maji, huku omba omba wakiwa
wametanda kila upande, yote haya yamo katika soko la mnadani njia panda ya kwenda
Arusha-Makyungu mkoani Singida. Biashara ya pombe za kienyeji imechukua eneo
kubwa la soko tofauti na bidhaa nyingine, omba omba nao kila jumamosi wanahamia
katika soko hilo kwa lengo la kutafuta ridhiki ili kujikimu na hali ngumu ya
maisha, wengi wao wakiwa ni wazee pamoja na watoto wadogo. Bi. Edilitulda Chami, Mwandishi wa habari
Mazingira ya soko hilo yamekuwa kero kutokana na uchafu na
harufu mbaya ya pombe za kienyeji maarufu kama Mtukuru ( lugha ya Kinyaturu )
ambazo zimekuwa zikinyweka katika hali ya uchafu wa hali ya juu. Pombe hiyo ya
kienyeji imekuwa ikitumika kama maji ya kunywa kwani hata watoto wadogo hununua
maandazi na pombe hiyo kwa lengo la kupunguza kiu na njaa. Ni vyema sana kulinda tamaduni zetu kama
matumizi ya vyakula, vinywaji na mengineyo, lakini usafi uzingatiwe!
Hali hii si kwamba imeonekana kwa mwandishi wa habari tu, eneo
la mnadani Singida kutokana na umaarufu wake pia hutembelewa na maafisa wa
ngazi mbali mbali wa serikali ambao kila jumamosi huhudhuria hapo kunywa pombe
na kula nyama choma na supu. Wengine wanashiriki hata katika mlo wa mchana
katika eneo hilo, najiuliza je hawaoni hali hii?
Waswahili walisema, usipoziba ufa basi jiandae kujenga
ukuta. Endapo utatokea ugonjwa wowote wa mlipuko huenda ukagharimu maisha ya
watu ambayo hayalinganishwi au kuthamanishwa na chochote hapa duniani.
No comments:
Post a Comment