Na Daud Nkuki
Singida
Viongozi wa Kata na Vijiji wametakiwa kutambua umuhimu wa uwepo wa mabaraza ya Jadi kama yalivyo ainishwa katika sera ya ulinzi ya Taifa.
Mkuu wa kituo cha Polisi Mtinko Inspekta Ildefonce Bernard Kagaruki, alikuwa akizungumza na wazee wa Baraza la jadi la Kata ya Makuro, katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida, kuhusu wajibu wa kazi zao.
Inspekta huyo ambaye alikuwa akizindua baraza hilo, aliwaambia mabaraza ya aina hiyo, hayana budi kuwa na mtandao na Viongozi wa serikali, dini, vyama vya siasa na taasisi mbalimbali ili kuondoa migongano kati yao na viongozi hao.
“Awali mabaraza hayo yalidaiwa kuingilia kazi za wengine. Kufanya hivyo ni kuvuruga sera ya ulinzi katika mgongano wa kimaslahi” alisisitiza mkuu huyo.
Alisema nchi hii inaongozwa na utawala wa kisheria, kila lifanywalo liwe chini ya sheria na sio kuzingatia mambo ya kijadi yanayovunja sheria za nchi.
Inspekta Kagaruki hakusita kuzungumzia swala la unywaji pombe ambao ni kichocheo cha uhalifu usio na udhibiti kama vile ubakaji, utoroshwaji, ugomvi, wizi, kutishiana maisha na wanawake kushindwa kutunza ndoa zao.
Aidha Baraza lazima lipige vita mila zilizopitwa na wakati; ukeketaji,mimba kwa wanafunzi, utoro mashuleni na kadhalika. Linalotakiwa ni jinsi ya kudhibiti mimba mashuleni na sio kwanini ana mimba.
Uzinduzi wa Baraza hilo, ulihudhuriwa na wazee 44 kati yao 36 wanaume na wanane wanawake, ambao wametakiwa kuanzisha ulinzi shirikishi katika maeneo yao.
No comments:
Post a Comment