Thursday, October 4, 2012

JUKWAA LA KATIBA TANZANIA



JUKWAA LA KATIBA TANZANIA
P. O. Box 78466, Plot No. 714/18 Mwenge, Behind TRA Offices, Dar Es Salaam, TANZANIA
Tel: +255 22 2773795   Fax: +255 22 2773764   Cell: 0783 993088

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI



TAARIFA  YA  UFUATILIAJI  WA  MCHAKATO  WA  KUKUSANYA MAONI KWA

AJILI YA UUNDAJI WA KATIBA MPYA TANZANIA KATIKA  MIKOA  YA  KIGOMA, 

LINDI,MWANZA,  MOROGORO, MBEYA, KATAVI NA RUVUMA  KUANZIA

TAREHE 27 AGOSTI HADI 28 SEPTEMBA, 2012 !
KUSUASUA KWA MCHAKATO WA KATIBA: TUJIANDAE VIPI ENDAPO
 HATUTAKUWA NA KATIBA MPYA IFIKAPO 2014?




JUKWAA LA KATIBA TANZANIA tumeendelea kufuatilia na kuchunguza kwa makini awamu ya pili ya Mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya katiba mpya kupitia mikutano ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuanzia tarehe 27 Agosti hadi 28 Septemba  2012 ikihusisha mikoa saba ambayo ni Kigoma, Lindi, Mwanza, Morogoro, Mbeya, Katavi na Ruvuma. Awamu hii haikuhusisha mikoa yoyote ya Tanzania Zanzibar!
Kwa mara nyingine, JUKWAA tunapenda kuipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa  kuweza kuandaa maeneo na vifaa vya kuwezesha wananchi kuendelea kushiriki katika kutoa maoni yao ya mambo ambayo wangependa yaingie katika Katiba mpya. Awamu hii, eneo ambalo Tume imefanya vizuri zaidi ni kwa namna ambavyo wajumbe waliendesha mazungumzo kwa utulivu na ukarimu kwa wananchi walioweza kuhudhuria zoezi la kutoa  maoni yao,hasa kwenye mkoa wa Ruvuma na Mbeya ambako wananchi wengi walisifiaukarimu wa wajumbe wa Tume na kuipongeza. Hili ni jambo jema kwa kuwa inaonesha  jinsi  Tume ilivyojifunza kutokana na mapendekezo yetu mwishoni mwa awamu iliyopita ambapo tuliitaka Tume iache kuhoji watu kwa ukali na maswali kana kwamba wako kituo cha Polisi.
Pamoja na mambo kadhaa mazuri, bado kumeendelea kujitokeza mapungufu kadhaa  ambayo yanahitaji kurekebishwa ili kuweza kuboresha ufanisi wa ukusanywaji wa maoni katika mikoa 15 ambayo imesalia sawa na Asilimia 50 ya mikoa yote ya Tanzania.

1. MAKADIRIO YA KATIBA MPYA KUPATIKANA IFIKAPO APRILI 2014 SI HALISIA.
Kutokana na kusuasua kwa mchakato unaendelea wa ukusanyaji maoni, na hamasa ndogo miongoni mwa wananchi juu ya Mchakato wenyewe wa Katiba Mpya huku sheria ya Mabadiliko ya Katiba, sura ya 83 ya Sheria (2012) ikiipa Tume ya Mabadiliko ya Katiba mamlaka hodhi ya kufanya karibu kila kitu katika Mchakato  huu,  inaanza kujidhihirisha wazi  kuwa ni  jambo  lisilowezekana kukamilisha hatua zote za Mchakato wa Kupata Katiba Mpya ifikapo mwezi Aprili, 2014. Kwa mfano elimu ya uraia inayotolewa ni finyu na haba kutokana na kubanwa na sheria husika. Aidha, Ukusanyaji maoni ambao unafanywa kisheria kuwa kazi ya Tume pekee utachukua muda mrefu sana na tena bila kumfikia kila Mtanzania. Hata taasisi zilizo na utayari, uzoefu na weledi wa ukusanyaji wa maoni kama JUKWAA LA KATIBA TANZANIA zimekwamishwa na sheria ama na vyombo  vinavyotekeleza  sheria hiyo. Katika mwezi wa Oktoba,  kwa  mfano,  JUKWAA  LA  KATIBA  TANZANIA  lilipanga  kuanza kukusanya maoni ya makundi ambayo yanaweza  yasifikiwe na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba kama wafungwa, Mahabusu na watumishi wa magereza lakini Idara ya Magereza imepokea maelekezo toka Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwa kazi hiyo inafanywa na Tume yenyewe. Jambo hili kwa uchunguzi wetu lina utata mkubwa hasa ikizingatiwa kuwa katika mikoa 15 ambako Tume imekwishakusanya maoni, hakuna  wafungwa, mahabusu na watumishi wa magereza  waliopata  fursa  ya  kutoa  maoni  yao.  JUKWAA  LA  KATIBA TANZANIA tunajiuliza Tume itaanza awamu nyingine ya kutembelea magereza baada ya kumaliza ukusanyaji maoni katika wilaya zote? Kama hivyo ndivyo itakavyokuwa, Tume itakamilisha lini ukusanyaji wa maoni?

Hata ukusanyaji wa maoni kwa wananchi wa kawaida katika mikutano ya kata unafanywa kwa kukimbizwa na kurukaruka sana ili kuwahi tarehe ya mwisho ya kupatikana  kwa  Katiba  mpya  ambayo  Tume  ya  Mabadiliko  ya  Katiba imewekewa na Serikali, yaani tarehe 26 Aprili 2014. Kwa makadirio ya haraka, imebaki mwaka mmoja na nusu tu ili kufikia tarehe hiyo ya mwisho ya uzinduzi wa Katiba mpya. Kwa mfano, katika awamu iliyokamilika wiki  iliyopita ya ukusanyaji maoni zipo kata na vijiji vingi havikufikiwa kabisa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika wilaya walikopita. Katika Mkoa wa Kigoma, Wilaya kama Kasulu yenye kata 25 imeshuhudia kata 4 tu zikifikiwa na Tume, huku wilaya ya ya Nachingwea  mkoani Lindi yenye kata 32 ikijionea kata 5 tu zikitembelewa na Tume ya Mabadiliko ya  Katiba. Hali imekuwa hivyo kwa wilaya nyingine nyingi kama Sengerema Mkoani Mwanza yenye kata 34 na Tume imetembelea kata 5 tu au wilaya ya Kilosa, yenye jumla ya Kata 35 ambako Tume imefika katika kata 4 tu. Hali hii inatisha na ni lazima irekebishwe mara moja!

2. MAKUNDI  YENYE  MAHITAJI  MAALUM  HASA  WATU  WENYE ULEMAVU BADO YAMESHINDWA KUSHIRIKI KATIKA KUTOA MAONI
Katika awamu hii pia bado Watu wenye ulemavu wa kuona, kusikia na kuongea hawajaweza kupewa fursa kubwa ya kuweza kushiriki vema kutoa maoni yao. Hii ni kutokana na Tume kuendelea kuitisha mikutano hii mbali na makazi ya wananchi walio wengi. Pia Tume haijaweza kuandaa miundombinu kama vyombo maalum kwa wasioona na wakalimani wa lugha za alama kwa wale wasio na uwezo wa kusikia na kuzungumza. Katika hatua za awali za kupanga  awamu  hii  ya  ukusanyaji  maoni,  Tume  ilijaribu  kuwasiliana  na wataalamu wa lugha za alama lakini kwa mshangao mkubwa Tume ikabadilika ghafla na kusema ingekuwa gharama mno kutumia wataalam hao wa lugha za alama kuongozana nao mikoani na mawilayani. Hii imewanyima wananchi hawa haki yao ya  kikatiba ya kuweza kuchangia maoni yao kwa ufasaha. Hivyo, JUKWAA LA KATIBA TANZANIA bado linaishauri Tume kurekebisha suala hili nyeti kwa haraka iwezekanavyo ili kutoa fursa kwa kundi hili la wananchi kutoa maoni yao kwa ufasaha, kwa kuwa fedha zipo tena kwa kiasi cha bajeti ya shilingi bilioni 34 kwa mwaka huu tu wa Fedha. Hiki ni kiasi kikubwa cha fedha kinacholingana na hata kuzidi baadhi ya wizara za serikali ya Tanzania!


3. MUDA AMBAO MIKUTANO HUITISHWA BADO NI MBAYA !
Ndugu Wanahabari, bado imebainika kwamba mikutano mingi ilifanyika muda wa asubuhi kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 6 mchana na baadaye mchana kuanzia saa 8 hadi 11. Kwa uhalisia mikutano ya asubuhi haijawa muafaka hasa kwa wakazi wa vijijini, ambao wako katika uzalishaji mali. Katika kata ya Mwakaleli mkoani Mbeya JUKWAA LA KATIBA lililalamikiwa kuwa mikutano ya asubuhi iliwanyima fursa wananchi wengi sana waliokuwa katika shughuli za uzalishaji mashambani katika bonde la Mwakaleli. Hii ni kutokana na ukweli kwamba sasa ni msimu wa kuandaa Mashamba, Hivyo wananchi wengi wamekua kwenye shughuli za kuandaa mashamba yao kwa muda huo wa asubuhi.  Kwa  ufananisho  na  mikutano  iliyofanyika  mchana,  kumekua  na mahudhurio makubwa zaidi kutokana na wananchi kuwa tayari wametoka kwenye shughuli za kilimo kwa muda wa mchana hivyo kumudu kuhudhuria mikutano ya  Tume ya Katiba. Hata katika maeneo ya mijini kama vile Manispaa ya Morogoro na wilaya ya Mvomero, watumishi wengi wakiwemo wa umma na serikali walilalamikia  kutokuwepo  utaratibu unaojulikana kuwa siku Tume inapokusanya maoni katika maeneo  yao  basi wawe na ruhusa ya kutofika kazini. Itakuwa vema kwa Tume kuwa wasikivu na  kuacha kukaidi pendekezo la kufanya mkutano mmoja tu wa mchana kwa siku ili muda wa asubuhi utumike kutafakari yaliyojiri siku ya nyuma yake.

4. VITUO VYA KUKUSANYA MAONI KUWA VICHACHE KILA WILAYA
Jambo la tatu ambalo halikwenda sawa katika mwezi wa awamu hii ya pili  ni kuhusu vituo vya ukusanyaji maoni kuwa vichache mno na vilivyoko viko mbali sana kati ya kituo  kimoja na kingine. Waangalizi wetu walipokea malalamiko toka kwa wananchi juu ya Tume kuruka Kata nyingi mno katika kukusanya maoni kama ilivyokwishaelezwa hapo awali. Hii ilichangia sana kwa Wananchi wengi hasa katika vijiji visivyopitiwa na barabara kuu za lami kutojua hata endapo wilaya zao zilikuwa zimeshapitiwa na Tume au bado. Katika moja ya Ziara ambazo JUKWAA LA KATIBA lilifanya katika mikoa ya Singida na Simiyu kupitia iguguno, Mwando, Nduguti, Kamlungu, Maheli, Gumanga, Igunia, Mkalama, Ibaga,  Chemchem,  Bukundi, Itaba hadi Meatu, wanavijiji wengi walionekana kutojua kabisa kama kuna mchakato unaoendelea wa Katiba Mpya na  endapo  mikoa  na  wilaya  zao  zilikuwa  zimekwishafikiwa  au  bado. Tunapendekeza kuwa ratiba ya Tume lazima iwe inatoka  mapema, tena inayohusisha mikoa yote hata itakayofikiwa miezi kadhaa ijayo ikitaja tarehe kamili ili watu wajiandae kwa ajili ya utoaji maoni. Inashangaza kuwa hata wananchi wa Dar es Salaam hivi sasa hawajui hatima ya Mkoa wao ukusanyaji maoni.

5. RATIBA ZA TUME KUBANA UHAMASISHAJI NA MATANGAZO KUHUSU MIKUTANO YA UKUSANYAJI MAONI KABLA YA SIKU.
Eneo la nne lenye mapungufu lilihusu uduni wa uhamasishaji na utoaji taarifa kuhusu ratiba za mikutano ya kupokea maoni. Pamoja na Tume kuchelewa kutoa Ratiba ya awamu ya pili, kwa maeneo mengi Tume ilitoa kwa kuchelewa matangazo ya kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya kutoa maoni hivyo kusababisha wananchi wachache kuhudhuria mikutano hiyo tofauti na ilivyotarajiwa. Katika maeneo mengi ya  Mkoa wa Morogoro, kulikuwa na malalamiko kuwa Tume ilichelewa sana kutangaza kuwa kutakuwa na mikutano na hivyo kusababisha wananchi wengi kukosa fursa ya kutoa maoni yao. Aidha, Katika Mkoa wa Ruvuma, tatizo hili lilipelekea uwiano wa wanawake na wanaume katika kushiriki mchakato wa utoaji maoni kuwa mbovu sana. Kwa mujibu wa takwimu zilizopatikana, idadi ya wanawake walioshiriki mikutano katika mikutano takribani 21  ya wilaya za Tunduru na Namtumbo mkoani Ruvuma ilikuwa ni 1,949 tu kati ya jumla ya wananchi 8,915 sawa na asilimia 22 tu. Aidha, kutokana na makosa hayo ya uhamasishaji duni kwa wanawake,  hata  uchangiaji  katika  kutoa  maoni  ulishuhudia  wanawake wakichangia kwa idadi ndogo sana ya 198 tu kati ya wananchi wote 2,074 waliotoa maoni kwa Tume, sawa na asilimia 9.5 tu, ambayo ni aibu.

6. WAKUU WA WILAYA KUTISHIA WANANCHI KWA UWEPO WAO KATIKA MIKUTANO YA TUME!
Kama inavyojulikana, wakuu wengi wa Wilaya wana mahusiano hasi na wananchi kutokana na wao kuwa na mazoea ya kutumika kwa kamata kamata ya wananchi katika maisha ya kila siku. Kwamba sheria imewapa madaraka ya kuweza kuhusika katika mchakato wa Katiba kwa niaba ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni bahati mbaya sana. Katika maeneo mengi, wakuu wa wilaya walionekana kuweka pingamizi kwa wananchi hata kuandaa midahalo na mijadala ya  Katiba Mpya. Hivyo basi, kuwepo kwao katika mikutano ya kukusanya maoni kuliwakwaza na kuwatisha wananchi wengi sana hasa katika maneo ya vijijini zaidi. Zipo sehemu ambako wakuu wa wilaya husika walipewa fursa ya kufungua mikutano ya  ukusanyaji  maoni. Jambo hili lilileta tafrani kubwa na tungependa kushauri kuwa tabia hii isijirudie tena. Kwa kuwa Tume imejigawa katika makundi imara kwa kila mkoa na  kupatiwa kiongozi wa msafara, hakuna tena haja ya Mkuu wa wilaya yeyote kujiingiza na kuanza kufungua mkutano wa ukusanyaji maoni. Hata katika mikutano na waandishi wa habari  kama iliyofanyika kati ya Tume ya Katiba na wanahabari, ilikuwa si lazima kwa Mkuu wa  Wilaya kuwa mstari wa mbele katika kushiriki kama ilivyotokea mkoani Ruvuma. Katika wilaya kama Meatu, Mkuu wa Wilaya alizuia kabisa mijadala yoyote ya Katiba mpaka kwa ruhusa yake, jambo ambalo hata hata katika sheria ya Mabadiliko ya Katiba haliko vibaya hivyo.
Kutokana na yaliyojitokeza kutokana na ufuatiliaji wetu katika Mikoa saba ya awamu hii  iliyoisha 28 Septemba 2012, JUKWAA LA KATIBA TANZANIA tunapenda kutoa mapendekezo yafuatayo:
(a) Mchakato wa Katiba Tanzania hautazaa Katiba Mpya ifikapo Aprili, 2014 na hivyo ipo haja ya kuanza kujiandaa kwa hilo.
(b) Kwa kuwa sababu kubwa ya kukimbiza mchakato wa katiba Mpya ni haja ya wanasiasa  kupata Katiba Mpya itakayotumika katika uchaguzi wa mwaka 2015, JUKWAA LA  KATIBA tunapendekeza kuwa zipo njia mbadala za kuwezesha uchaguzi ufanyike kwa salama, amani na utulivu hata bila kulazimika kukimbiza mchakato wa Katiba mpya kwa kasi ya ajabu kama inavyoendelea hivi sasa.
(c) Kwa kuwa kikwazo kikubwa katika kufanyika kwa uchaguzi kwa kutumia Katiba ya sasa ni Tume ya sasa ya Taifa ya Uchaguzi ambayo uhuru na ufanisi wake  unatiliwa mashaka, JUKWAA LA KATIBA tunapendekeza kuwa kufanyike marekebisho makubwa kupitia ibara ya 98 ya Katiba ya sasa katika vipengele vinavyohusiana na Tume ya Uchaguzi na usimamizi mzima wa uchaguzi ili ifikapo  April  2014 tuwe tuna ibara za Katiba zinazoweka Tume huru na yenye ufanisi na weledi ili hatimaye ipewe jukumu la kusimamia chaguzi zote zitakazofuata baada ya April, 2014 ikiwemo: Uchaguzi wa serikali za Mitaa, mwishoni mwa 2014; uchaguzi mkuu 2015 na uchaguzi wa wajumbe watakaohitajika katika vyombo vya kujadili na kupitisha Katiba Mpya ya Tanzania. Hiyo itaopunguza sana malalamiko  na  ubishi uliopo hivi sasa bila kulazimika kuharakisha na kukimbiza mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya nchini!
(d) Kuhusu Mchakato wa utungaji wa Katiba Mpya, JUKWAA tunapendekeza kuwa uendelee lakini kwa kasi ya kawaida na kwa umakini mkubwa bila kukimbizakimbiza ili tuweze kupitia hatua zote za uandishi wa Katiba ya Kidemokrasia hata baada ya  uchaguzi Mkuu wa wa 2015. Wataalam zaidi wanakaribishwa kuendelea kushauri namna bora ya kuvuka chaguzi za mwaka 2014 na 2015 kabla ya kupata Katiba Mpya!
Mwisho, tunapenda kuishauri Serikali kupitia Wizara ya Sheria na Katiba kutosahau  ahadi  yake  ya  kupeleka  muswada  wa  sheria  wa  kureebisha mapungufu  yote  katika  Sheria  ya  mabadiliko  ya  Katiba,  2012  haraka iwezekanavyo ili kufungua milango ya  elimu ya uraia, ukusanyaji maoni na kupunguza woga na hofu iliyotanda miongoni mwa wananchi kuhusu mchakato wenyewe wa  Katiba Mpya.
Aidha, ipo haja kwa Tume ya Katiba kupanga ratiba ya mikutano ya ukusanyaji
maoni kwa mikoa 15 iliyobaki kwa umakini mkubwa na kutangaza ratiba hiyo mapema iwezekanavyo ili wananchi waanze Kujiandaa. Zaidi ya yote, Tume ianze  kufikiria  kuandaa  ratiba  ya  asasi  na  makundi  maalum  ambayo hayatafikiwa katika awamu zote za ukusanyaji maoni ili uje ufanywe mpango mahsusi wa kuwahusisha na  kuzungumza  nao hapo baadaye. Kwa Tume imeahidi kukusanya maoni ya wafungwa, mahabusu na watumishi wa Magereza zote, Tume iandae ratiba ya namna  itakavyotembelea  magereza zote na ishirikishe wadau katika upangaji huo wa ratiba.
Hatimaye, tunaitaka Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuhusisha wadau wengine katika kazi yake kuanzia wakati huu wa kukusanya maoni, kuandaa rasimu ya Katiba Mpya, kuandaa  wajumbe wa bunge maalum la katiba, na vyombo vingine vya kimaamuzi na vya habari. Tabia ya Tume kujifungia na kufanya kila kitu wenyewe ni tabia ya uandishi wa Katiba za Kikoloni sio wa Katiba ya Kidemokrasia kwa ajili ya watanzania wote!

Imetolewa na kusainiwa kwa niaba ya JUKWAA LA KATIBA TANZANIA,

Deus M Kibamba

Mwenyekiti

JUKWAA LA KATIBA TANZANIA

03 OKTOBA 2012


No comments: