Sunday, November 11, 2012

TANZANIA HAITAPIGANA NA MALAWI-KIKWETE

Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete amesema Tanzania haina mpango wowote wa kuingia vitani na nchi ya Malawi kugombea mpaka wake katika ziwa Nyasa ambalo Malawi huliita ziwa Malawi


Na. Prosper Kwigize
Dodoma
Kauli hiyo  ameitoa jumapili November 11, 2012 katika mkutano mkuu wa nane wa Chama cha Mapinduzi CCM mjini Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine chama hicho kitafanya uchaguzi wa viongozi wa chama hicho

Rais Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa taifa wa chama cha mapinduzi amekiri kuwepo kwa mgogoro wa kimpaka baina ya Tanzania na Malawi ambapo Tanzania inatoa hoja kuwa mpaka huo uko katikati ya ziwa huku Malawi wao wakidai kuwa mpaka uko ufukweni upande wa Tanzania eneo la mbambabay

Hata hivyo rais Kikwete amebainisha kuwa pamoja na kutokuwepo na nia ya kuingia vitani na Malawi, Tanzania inaendelea kuimarisha uwezo wa majeshi yake kwa kutoa mafunzo na kuongeza zana za kivita ili kuwaweka tayari wapiganaji kulinda mipaka na usalama wa watanzania

Aidha ameonya kuwepo kwa watu wanaoichafua nchi kuwa serikali imepeleka vikosi mpakani kwa nia ya kujiandaa kupigana na Malawi na ametaja kuwa huo ni uongo na Tanzania haina mpango huo na wanaoeneza uvumi huo hawana nia njema na taifa la Tanzania.

Wakati huo huo Dr. Kikwete ametoa wito kwa watanzania kuacha malumbano na chuki za kutafuta vyeo badala yake wasimamie utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM na pale penye mafanikio watembee kifua mbele na wasitishwe na washindani wa CCM ambao wamekuwa wakidai kuwa CCM hakijafanya kitu

Rais Kikwete ameinadi miradi mikubwa ua jenzi wa barabara, elimu, Nishati na utaratibu wa kutumia mapato ya ndani kupitia makusanyo ya kodi kuwa ni kiashiria cha CCM kufanya vema katika kuleta maendeleo kwa watanzania

WAKATI HUO HUO kamati kuu ya CCM imempendekeza Dr. Muhamed Ally Shein na Philp Mangula kuwa wagombea wa nafasi ya makamu mwenyekiti baada ya Tamko la kustaafu kwa Aman Karume wa Zanzibar na Pius Msekwa wa Bara.

1 comment:

Anonymous said...

HONGERA RAIS WETU KWA KAULI HIYO, VITA SI TIBA YA UKOROFI WA JIRANI YETU MALAWI BALI ELIMU NA MAZUNGUMZO YATATUWEZESHA KUSHINDA.

ASANTE STANDARD KWA KUTUPA HABARI HII HARAKA IWEZEKANAVYO, NAJUA MAGAZETI YATALETA HABARI ZA DODOMA KESHO