Wednesday, September 19, 2012

WANAFUNZI WATAHADHARISHWA DHIDI YA UKIMWI


Na. Jumbe ismail na Everister Lucas

Singida

 

KATIBU wa Idara ya Utumishi wa Walimu Mkoa wa Singida amewaasa vijana wanaomaliza masomo ya elimu ya kidato cha nne nchini kujiepusha na maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukimwi kutokana na kile alichodai kwamba dawa ya kutibu bado haijapatikana.

Katibu huyo,Bwana Samwel Olesaitabahu ametoa tahadhari hiyo wakati wa sherehe za mahafali ya 11 ya kidato cha nne katika shule ya sekondari Singida,iliyopo kwenye Manispaa ya Singida.

Amefafanua Bwana Olesaitabahu kuwa idadi kubwa ya vijana wanaomaliza elimu ya sekondari ya kidato cha nne na hata kabla ya kumaliza masomo yao huanza kujingiza kwenye vitendo vya uasherati,jambo ambalo amesema linachangia kwa kiasi kikubwa kupoteza nguvukazi ya taifa.

Aidha afisa huyo mwenye dhamana ya kusimamia idara ya utumishi ameweka wazi kuwa malevi kwa vijana ni jukumu la wote kati ya wazazi na walimu,na kwamba ni dhana potofu kuwa walimu ndio wenye majukumu ya kuwasimamia wanafunzi hao.

Hata hivyo afisa huyo amebainisha kwamba ili kufanikisha kupata vijana wenye malezi mema ni vyema wazazi kwa kushirikiana na walimu kuwalea kwa uangalifu wanafunzi na kwamba haitakuwa vizuri kazi hiyo ikaachwa kwa walimu peke yao.

Kuhusu suala la nidhamu kwa wanafunzi,Bwana Olesaitabahu amesema suala la nidhamu katika shule yeyote ile ni la utatu kwa maana kwamba walimu,wanafunzi pamoja na uongozi wa shule,hauna budi kuwa na nidhamu ya pamoja kwa lengo la kuleta ufanisi kwenye taaluma.

Hata hivyo akijibu risala ya wanafunzi waliomaliza kidato cha nne katika shule hiyo,katibu huyo amesisitiza kwamba uongozi wa shule hiyo hauna budi kuweka kipaumbele kulingana na changamoto zinazowakabili wanafunzi wa shule hiyo.

Amefafanua huku akitoa mfano wa vipaumbele katibu huyo wa idara ya utumishi aliutaja ujenzi wa uzio wa kutenganisha chuo na shule hiyo ya sekondari.

Hata hivyo hakusita kuushauri uongozi wa shule hiyo kuanza mara moja kuweka mikakati ya kuendeleza shule hiyo,hususani ujenzi wa uzio huo na alitumia fursa hiyo kuwapongeza walimu wanaofundisha shule binafsi licha ya walimu hao kufundishwa na serikali.

Awali katika risala yake,Mkuu wa shule hiyo,Bwana Francis Ibabila amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika shule hiyo,lakini bado shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni kukosekana kwa maabara,maktaba pamoja na uzio unaotenganisha kati ya chuo na shule ya sekondari hiyo.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa shule kukosekana kwa uzio huo unachangia kwa namna moja au nyingine ukosefu wa nidhamu kwa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo.

Changamoto zingine kwa mujibu wa Bwana Ibabila ni upungufu wa maji ya kutosheleza mahitaji ya wanafunzi pamoja na utoro wa wanafunzi unaosababishwa na ushirikiano mdogo kati ya walimu na wazazi.

Katika mahafali hayo ya 11 jumla ya vijana 56 wakiwemo wavulana 26 na wasichana 30 wamehitimu kidato cha nne katika shule ya sekondari Singida,iliyopo katika Manispaa ya Singida.

No comments: