Wednesday, September 19, 2012

MAKALA MAALUMU TOKA DAR ES SALAAM


Masuala ya Msingi Katika Mwelekeo Mpya wa Hatima ya Taifa Letu

 

Na Gwandumi Gwappo Atufwene Mwakatobe

Septemba 15, 2012, Mwakaleli (Kandete)

 

1. Itikadi na Falsafa ya Taifa

 

Taifa letu linapaswa kuwa na itikadi na falsafa inayotuongoza na inayoweza kurithishwa kutoka vizazi vilivyopo na vijavyo. Itikadi na falsafa ambayo inalinda utamaduni wetu, utu wetu na maisha yetu kwa kuyapa kipaumbele cha kwanza dhidi ya vitu na mali. Itikadi na falsafa nyingi zilizopo na zilizopita zinalenga mifumo ya uchumi badala ya kujikita katika kulinda heshima na hadhi ya utu wa mtu kwanza. Tumepitia vipindi vya ujima, ujamaa, ubepari, ubeberu na mitazamo inayokinzana kimrengo ambayo yote inahusiana na mali au utajiri wa kiuchumi (material wealth), ambayo haijali utu na maisha ya mtu. Tumesahau kuuendeleza utu, heshima na utukufu alionao mtu bila kujali matabaka ya maisha kiuchumi. Bila itikadi na falsafa inayotuongoza tutakosa utamaduni wetu na tutakosa mwelekeo wa jamii na taifa kwa ujumla.

 

Kwa waraka huu natamka kwamba nchi yetu itafuata itikadi na falsafa ifuatayo:

 

Kulinda, Kuheshimu na Kuendeleza Misingi ya Utu wa Mtu na Maisha Yake Kwanza Kuliko Mali na Vitu.

 

Misingi ya Utu ina mihimili mikuu minne: Huruma, Ukarimu, Kujali na Utumishi wa mtu kwa binadamu wenzake, hususan jamii inayomzunguka na taifa lake. Maliasili au rasilimali zozote zile kama wanyamapori, misitu, maji, madini, fedha, nakadhalika, haviwezi kupewa kipaumbele kuliko utu wa mtu na maisha yake.

 

2. Haki ya Msingi ya Raia

 

Raia yeyote nchini anayo haki ya kushiriki kikamilifu katika kuiendeleza jamii na taifa kwa ujumla kwa kutumia kipaji, ujuzi, utaalamu, maarifa na nguvu alizonazo bila kizuizi chochote. Haki ya kuitumikia na kuiendeleza jamii yako ndiyo haki ya msingi na nguzo ya umoja wa kijamii na kitaifa. Ieleweke kuwa hakuna jamii au nchi yoyote duniani iliyoendelezwa na taasisi au chama cha siasa. Nchi inaendelezwa na raia wake wenye uzalendo na uchungu wa kimaendeleo kwa kutumia tunu zao walizojaliwa na Mungu – si chama cha siasa. Mhandisi, fundi, mbunifu, mkulima, msanii, mtaalamu wa tiba, mwalimu, mwanamichezo, mvuvi, mjasiriamali, mwenye kipaji cha uongozi, nakadhalika; hao ndio huiendeleza nchi.

 

Ukiwa mhandisi huhitaji kuwa mwanachama wa chama cha siasa ili kulijenga taifa lako. Ukiwa mkulima stadi huhitaji kibali au tiketi ya chama cha siasa ili uinue kilimo nchini. Vivyo hivyo ukiwa na kipaji cha uongozi huhitaji kuwa mwanachama wa chama cha siasa ili kuiongoza jamii yetu katika ngazi yoyote ile, mathalani uenyekiti wa kijiji, udiwani, ubunge na hata urais.

Haki ya kiraia ya kutumia kipaji chako kuliendeleza taifa letu ni haki ya msingi ambayo haipaswi kuwekewa kizuizi au sharti la aina yoyote ile. Ni ukandamizaji usio mithilika kumtaka raia katika nchi yake apitie chama cha siasa ili awe mkulima, mhandisi, mganga, mwalimu au kiongozi kwa kushika wadhifa au cheo katika ngazi yoyote ile. Na kwa msingi huo hatusemi huyu ni mgombea binafsi bali ni mgombea kupitia haki yake ya kiraia ilmradi amethibitika kuwa ni raia wa Tanganyika, Zanzibar au Tanzania kwa mambo ambayo yanahusu muungano.

 

3. Kukomesha Ubaguzi na Ukiritimba wa Vyama vya Siasa Ili kujenga Umoja

 

Vyama vya siasa vimenyang’anya kwa muda mrefu haki ya uhuru na ushiriki wa wananchi katika kujiletea maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiutamduni. Tumekuwa tukipiga kelele kwamba ukabila, rangi, udini na matabaka ya watu kimaisha yanaleta ubaguzi na hata uhasama. Lakini vyama vya siasa vimekuwa vikifanya ubaguzi na uhasama mkubwa zaidi na hata kuthubutu kudai serikali ni mali ya chama fulani, wakati kiukweli inatokana na wananchi na ni taasisi ya umma – si chama cha siasa. Chama kinapodai serikali ni mali yake wakati inawekwa madarakani na umma huwafanyi watu wa vyama vingine na wasio na vyama wajisikie kwamba si serikali yao. Wanaona hawana serikali, jambo ambalo tunaona wanaojiita  wenye chama tawala wakipandisha mabega na kujiona wana haki zaidi katika nchi kuliko wananchi wenzao. Ni ubaguzi mbaya unaovunja umoja wetu wa kitaifa kudai serikali ni ya chama fulani. Serikali ni taasisi ya umma, si ya chama cha siasa. Chama ni taasisi au asasi ya baadhi ya watu, si ya umma. Vyama vya siasa vinakuja na kuondoka lakini taifa litadumu daima endapo umoja wa kitaifa utalindwa na kuzingatiwa.

 

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Toleo la 2008, Sehemu ya Pili, ibara ya 8, kifungu cha 1(a), ukurasa wa 23, inabainisha wazi kwamba: “Wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na serikali itapata madaraka na mamlaka yake kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii.” Serikali inapata madaraka kutoka kwa umma (wananchi) na si chama cha siasa. Hakuna chama ambacho kiko madarakani isipokuwa kuna serikali ya wananchi iliyoko madarakani. Rais aliyepo ni wa umma si wa chama cha siasa – hakupata madarakani kutokana na chama siasa bali umma uliomchagua kutoka kwa watu wenye vyama na hata wasio na vyama.

 

Tumeona hata bunge linaendeshwa kiubaguzi wakati ni taasisi ya umma ambayo kamwe haipaswi kujinasibisha na vyama vya siasa kwa kuwa hata wabunge/wawakilishi wanatokana na wananchi na si chama cha siasa. Kazi inayofanywa na vyama vya siasa ni kuendesha mchakato tu wa kupata wagombea ambao mwishowe huchaguliwa na wananchi wote kuwa madiwani au wabunge. Tunashuhudia uhasama miongoni mwa wananchi unaotokana na kuegemea chama fulani na kuleta mgawanyiko unaohatarisha au kuvunja kabisa umoja wetu wa kitaifa. Lazima tuwe na masuala tunayokubaliana kitaifa na kuyapa kipaumbele.

 

Ni aibu kuona wanasiasa wakiunganishwa na misiba tu badala ya ajenda na masuala ya kitaifa. Mbaya zaidi ni pale ambapo mbunge akifukuzwa au akikiacha chama chake ananyang’anywa ubunge ambao alipewa na wananchi waliomchagua. Wananchi wananyang’anywa demokrasia yao na mbunge wao. Hii ni dhambi kubwa! Chaguo la wananchi halina budi kulindwa kikatiba na wananchi ndio wanaopaswa kumweka mtu madarakani au kumwondoa. Ipo haja ya kuweka na kuulinda msimamo huu kikatiba.

 

Aidha, chama chochote cha siasa kinachotaka kujijenga kwenye mioyo ya wananchi hakina budi kuacha kujijenga chenyewe bali kishiriki kulijenga taifa na kushughulikia matatizo yanayowakabili wananchi. Si busara kununua gari la kuendeshea kampeni za kisiasa huku zahanati, kituo cha afya au hospitali ikiwa haina gari ya wagonjwa au kuhudumia wajawazito. Chama cha siasa kikiamua kuchimba kisima, kuchonga madawati au kujenga madarasa badala ya kujenga ofisi ya chama kinakuwa kimejiwekea msingi mzuri miongani mwa jamii. Sioni mantiki ya kutumia mabilioni ya pesa kufanya kampeni za kumpata mbunge huku tukishindwa hata kujenga zahanati katika kijiji kimoja. Wala hatuna haja ya kuwa kadi za vyama vya siasa kwa kuwa chama kinapaswa kugusa na kuishawishi mioyo ya watu na matatizo yao hatimaye ndipo hupendwa na kuungwa mkono, na pengine kwa dhati zaidi kuliko wenye kadi. Na kwa kipengele hiki napendekeza Chama Cha Mapinduzi kibadili malengo yake pamoja na jina. CHADEMA kiache kuiga mwenendo wa CCM, na iwe vivyo hivyo kwa vyama vingine.

 

4. Suala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar

 

Awali ya yote, kama alivyowahi kusema Mwalimu Nyerere kuwa ukimwambia mtu mzima ukweli unamheshimu, lakini ukimwambia uongo unamdharau. Ni kuwadharau wananchi kuendelea kuwaambia kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina serikali mbili. Kusema ukweli tuna serikali za aina nne hapa nchini – na si mbili kama ambavyo wengi wameaminishwa. Serikali hizo ni:

 

  1. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ambayo imekuwa wazi sana kiutendaji na kimuundo
  2. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT/URT) ambayo ilianza na masuala 11 wakati wa kuanza muungano mnamo Aprili 26, 1964
  3. Serikali ya Tanganyika ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikijificha kwenye masuala ya muungano au kama ambavyo wengine kimakosa wamebuni jina la Tanzania Bara
  4. Serikali za mitaa ambazo zinatenda kazi katika ngazi ya vitongozi, mitaa, vijiji, wilaya, miji, manispaa na majiji.

 

Na ieleweke kuwa Tanganyika na Zanzibar hazikufuta hadhi ya kuwa nchi isipokuwa tu katika masuala ambayo ni ya muungano, na kwa miezi kadhaa baada ya kuungana, nchi ya muungano iliendelea kuitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hadi pale ambapo mshindi wa kutunga jina moja la muungano alipounganisha TAN kutoka kwenye herufi tatu za kwanza za Tanganyika na ZAN kutoka kwenye herufi tatu za kwanza za Zanzibar, na kumalizia vifupisho vya majina yake mawili vya I na A na kupata TANZANIA. Unapotaja TANZANIA unataja mambo ambayo ni ya muungano, yanayobaki yanakuwa ya nchi ya Zanzibar upande mmoja wa muungano na nchi ya Tanganyika kwa upande mwingine.

 

Hadi leo hakuna mahali popote ambapo jina Tanganyika lilifutwa na kuwekwa jina lingine. Na hadi leo Hati ya Muungano ndio mkataba pekee ulio hai kuhusiana na muungano wa nchi mbili. Wanaoita Tanganyika kuwa ni Tanzania Bara wanakosea sana kwa kuwa hatujawahi kubadili jina la Tanganyika kuwa Tanzania Bara. Hata tungekubaliana kisheria bado tungekosea kuiita Tanganyika Tanzania Bara kwa kuwa pwani yote (Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam na Tanga) haiko bara! Aidha visiwa vya Mafia, Songosongo, Koma, Kwale, Ukerewe na kwignineko haviko bara!

 

Nisisitize kuwa, hali halisi na muundo halisi wa kiutendaji uliopo sasa tangu Aprili 26, 1964 ni wa serikali tatu: Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Tanganyika ambayo kimakosa inajificha kwa kutumia jina la Tanzania au Tanzania Bara. Pia kuna watu walijitungia kienyeji kwa kubdadili jina la Zanzibar na kuita Tanzania Visiwani bila kujua kuwa hata visiwa vya Ukerewe na Mafia ni Tanzania Visiwani lakini haviko Zanzibar! Na waliendelea kutapatapa tena kwa kuiita Zanzibar Tanzania Zanzibar wakati ni Zanzibar na ndiyo jina lililomo kwenye hati ya muungano. Nashukuru kwamba wazanzibar wameendelea kuiita nchi yao kwa jina la Zanzibar.

 

Nisisitize kuwa mambo yote yasiyo ya muungano yanashughulikiwa au yanasimamiwa na Zanzibar au Tanganyika. Kusema masuala yasiyo ya muungano yanashughulikiwa na Tanzania kwa upande wa Tangayika ni makosa kwa kuwa si ya muungano, maana Tanzania ni kwa ajili ya masuala ya muungano tu! Wenzetu Zanzibar wanakwenda sawia na unavyosema mkataba almaarufu Hati ya Muungano na wako wazi sana katika kufuata mkataba huo na kuulinda.

 

Hadi leo hii tuna sikukuu za aina tatu: uhuru wa Tangnyika wa Desemba 9, mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12 na muungano wa Aprili 26. Kimahesabu huwezi kuunganisha vitu viwili ukabakiwa na vitu viwili. Utakuwa na kimoja au zaidi ya viwili! Huwezi kuwaoza mwanamke na mwanaume ukawa na ndoa mbili. Itakuwa ndoa moja tu. Ukiunganisha maumbo mawili yaliyounganika kwa sehemu tu unapata maumbo matatu: kiunganiko (intersection set) na sehemu mbili ambazo hazijaunganika. Kuendelea kusema uongo kwa kudai kuwa Tanzania kuna serikali mbili wakati hali halisi kiutendaji ni serikali tatu ni kuwadharau wananchi.

 

Tanganyika ilikuwa na umri wa miaka miwili na miezi mitano tu ilipoungana na Zanzibar kwa mambo 11 tu (sasa yako 22), tangu ilipopata uhuru Desemba 9, 1961; na Zanzibar ilikuwa na umri wa miezi minne tu na siku kadhaa tangu ilipopata uhuru Desemba 10, 1963, na ilikuwa na umri wa miezi mitatu tu tangu ilipofanya mapinduzi Januari 12, 1964, ambayo ndiyo yanayoenziwa. Leo hii hatuwezi kujigamba kwamba Zanzibar imefaidika na muungano kwa kuwa haikuishi muda mrefu nje ya muungano (miezi mitatu tu) na kuzitumia vizuri fursa za kitaifa na kimataifa. Na Tanganyika pia haikuishi muda mrefu nje ya muungano (miaka miwili tu na miezi mitano). Tanganyika imekuwa ikigharamia mambo mengi ikiwa pamoja na kuwaruhusu Wazanzibar washiriki bungeni kwa mambo yasiyo ya muungano wakati Watanganyika hawashiriki kabisa kwa upande wa Zanzibar.

 

Nihitimishe kwa kusema kuwa suluhisho muafaka na thabiti la kudumisha uhusiano mwema na Wazanzibar ni kuwaachia kabisa wawe taifa huru na dola kamili kitaifa na kimataifa. Tanganyika nayo ibakie kamili ili tuondokane kwa amani na kero nyingi za muungano. Tubakie majirani wema kama ilivyo kwa Zambia, Msumbiji, Rwanda, Kenya na kwingineko. Kuwa na mahusiano mema na jirani ni jambo la msingi na si lazima muunganishe nchi. Kuna nchi nyingi tunahusiana nazo vizuri sana na kwa ukaribu japo haziko jirani. Undugu ni mahusiano mema si kuunganisha nchi.

 

Zanzibar imekosa fursa nyingi za kimataifa kwasababu ya kubanwa na kufinywa na muungano. Kwao muungano ni jinamizi! Si vema kuendelea kuwabana watu ambao ni ndugu zetu kama ilivyo kwa nchi zote jirani. Kuna faida nyingi kwa Tanganyika na Zanzibar kuwa nje ya muungano. Hatuwezi kuendelea na serikali tatu na mifumo tata inayotugharimu fedha nyingi na kero zisizoisha. Mungu ibariki Zanzibar, Mungu ibariki Tanganyika, na bariki uhusiano wetu mzuri na wa kijadi kati ya Zanzibar na Tanganyika na nchi zingine jirani na zilizo mbali.

No comments: