Wednesday, September 12, 2012

WAANDISHI WA HABARI SINGIDA WAANDAMANA




Bi. AWILA- mwakilishi wa gazeti la mwananchi akiwa katika maandamano ya waandishi wa habari Tanzania kupinga mauaji ya mwandishi mwenzetu wa mkoani Iringa Marehemu Mwangosi. STANDARD RADIO FM 90.1 SINGIDA inalaani vitendo vya kikatili dhidi ya waandishi wa habari duniani kote. PICHA na. Prosper Kwigize

Na Evarista Lucas,
Singida
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Singida(SINGPRESS) Bwana Seif Takaza; amewaasa wanahabari wa Mkoa wa Singida kujipanga na kuwa wajasiri zaidi katika utekelezaji wa jukumu lao la uandishi wa Habari.
Takaza alizungumza hayo mapema leo mara baada ya kupokea maandamano ya wanahabari hao wa Mkoa wa Singida katika ofisi ya SINGPRESS iliyopo katika jengo la CDTF mtaa wa Mughanga.
Waandishi wa Habari Mkoani Singida ambao wameungana na waandishi wenzao nchini kwa maandamano ya kimya kimya kulaani na kupinga vikali mauaji ya kikatili dhidi ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten mkoani na Mwenyekiti w Klabu ya Waandishi wa Habari Iringa marehemu Daudi Mwangosi, wakati akiwa kazini.
Maandamano hayo yakisindikizwa na askari polisi yalianzia eneo la Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na kupitia barabara ya Kawawa hadi kituo cha mafuta Esso.
Baadaye yaliingia barabara ya Soko kuu, msikitini, Mghandi, Ipembe, Karume, Kinyeto na hatimae kumalizikia kwenye ofisi ya klabu, ambapo Mwenyekiti wa SINGPRESS, Seif Takaza aliyapokea.
Akizungumza na waandishi 19 wa mkoa Singida walioshiriki maandamano hayo, Takaza alisema kitendo cha polisi kuhusika na mauaji hayo kimedhalilisha chombo hicho, pia ni ukiukwaji wa haki za binadamu, kulingana na mafunzo yao ya kijeshi.
“Mauaji ya mwangosi ni ya makusudi, hasa ikizingatiwa alikuwa mikononi mwa polisi, lakini mwisho wa siku akafia mikononi mwao….jambo hili lazima lipingwe kwa nguvu zote na watetezi wa haki za binadamu,”alisema.
Alisema mauaji hayo ni ya uonevu, kikatili na yanalifedhehesha taifa ambalo tangu lipate uhuru mwaka 1961 limejipatia sifa kubwa ya kudumu katika hali ya amani na utulivu kiasi cha kuitwa jina la kisiwa cha amani.
 
Aidha wanahabari hao wameomba kudumishwa kwa mahusiano kati ya jeshi la polisi na waandishi wa habari ili kuondoa uwezekano wa kutokea mauaji mengine kama hayo.
Hata hivyo wananchi wengi, waliyaunga mkono maandamano hayo huku wakiwapungia mikono sanjari na ‘Poleni’, kila ambapo wanahabari walipita katika barabara mbalimbali za mjini Singida.
Kwa upande upande mwingine baadhi ya wanahabari waliopata fursa ya kutoa maoni yao na dukuduku dhidi ya mauaji hayo ya kikatili walisema kuwa licha ya kuwa marehemu Mwangosi alikufa akiwa kazini; ni wazi kuwa alitaka kuujulisha umma kile kinachoendelea na pia kujitaftia riziki yake.
" Wamiliki waboreshe malipo ya Waandishi wa habari haswa walioko mikoani kwakuwa kipato chao kinategemea zaidi utumaji wa stori na inawezekana kuwa karehemu alipoteza maisha wakati akihangaika kupata stori." Alisisitiza Josephat Isango ambaye anaandikia gazeti la Tanzania Daima.

 

No comments: