Friday, September 14, 2012

AJALI MBAYA YA GARI SINGIDA


HALIMA JAMAL

SINGIDA

 

Watu 9 wamekufa papohapo na wengine 25 kujeruhiwa baada ya ajali mbili tofauti kutokea mkoani singida leo asubuhi.

 

Taarifa za awali kutoka kwa Kamanda wa polisi mkoani Singida Linus Sinzumwa zimeeleza kuwa gari la kwanza kutokea ajali kuwa ni PT1149 aina ya land rover mali ya Polisi mkoani Morogoro na gari ya pili kuwa ni T126 AU aina ya fuso iliyokuwa ikitokea Singida mjini kuelekea kijiji cha mtavira kwa ajili ya mnada.

 

Alisema ajali ya kwanza iliyohusisha gari ya polisi,ilikuwa ikisafirisha maiti ya askari polisi kutokea Morogoro kwenda Musoma ikiwa imebeba watu kumi na moja.

 

Aidha alisema gari hiyo ilipofika maeneo ya nje kidogo ya mji wa singida ijulikanayo kama kambi ya wachina iliacha njia na kuanza kubiringita na kusababisha vifo vya watu wanne papo hapo.

 

Sinzumwa alisema kuwa baada ya kupata taarifa hiyo baada ya dakika kadhaa aliweza kupata tena taarifa ya kuwa kuna ajali nyingine tena imetokea maeneo ya Minyughe.

 

Alisema baada ya kutuma askari wake kwenye eneo la tukio ndipo walikuta gari aina ya fuso iliyokuwa ikielekea mnadani imepinduka na kukuta maiti za watu watano na majeruhi ndipo walipowachukua na kuwakimbiza hospitali ya mkoa.

 

Aidha Sinzumwa aliwataja waliokufa katika ajali ya gari la polisi kuwa ni Rehema Juma,Regu Kamamo,Rosemary Nyabuzuki pamoja na mmoja aliyefanamika kwa jina moja tu la Juma.

 

Sinzumwa aliwataja waliokufa kwenye ajali ya fuso kuwa ni Sarafina Ally,Mtalika Bilali ,Charles Thomas,Bakari pamoja na Pili Saidi.

 

Maulidi Mohamedi ambaye ni majeruhi wa ajali ya fuso amesema kuwa ajali hiyo imetokana na breki za gari hilo kufeli likiwa linateremsha mlima mkali na dereva wa gari hilo kushindwa kulimudu na kusababisha kuacha njia na kupinduka.

 

''Bado tunaendelea zaidi na uchunguzi wa ajali zote mbili tukikamilisha tutawaita ili muweze kuwa na uhakika nini chanzo zaidi ya ajali hizo''alisema Sinzumwa.

 

Aidha kamanda alisema kuwa majeruhi wa ajali zote wanaendelea kupata matibabu katika hospitali ya mkoa na kuwa hali zao zinaendelea vizuri.

 

Sinzumwa ametoa wito kwa madereva kuwa makini barabarani kwani roho za watu wengi zinapotea kwa uzembe wa watu wachache.

 

No comments: