Monday, February 11, 2013

TAARIFA YA HABARI YA SAA NNE USIKU FEB 11, 2013


Source:SR/Chami

Ed: BM

Date: Feb 11/02/2013

SINGIDA

Wito umetolewa  kwa wananchi wa mkoa wa Singida kufuata utii wa sheria bila shuruti na kuwa makini na fedha bandia zinazoingia ndani ya mkoa huo

Kamanda wa polisi mkoa wa singida ACP Linus Sinzumwa ametoa wito huo leo, wakati akitoa taarifa za matukio ya wiki kwa  waandishi wa habari ofisini kwake.  Ametaja ukio la mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Hassan Kisuwa kukamatwa na fedha bandia katika maeneo ya Singida Motel mkoani Singida

Kamanda Sinzumwa amesema kuwa mshtakiwa alikutwa na noti mbili za shilingi elfu tano kila moja, zikiwa na namba B 40012036 na nyingine ikiwa na namba DT 1547949 na kusema kuwa mtuhumiwa anatarajiwa kifikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika

Kamanda Sinzumwa amelitaja tukio jingine ni la mtu mmoja aliyetajwa kwa jina la Juma Husein mwenye umri wa miaka 50, kujeruhiwa kwa kukatwa mapanga na mtu aitwae John Shayo katika maeneo ya mwenge, na kwamba chanzo cha tukio hilo hakijajulikana na mshtakiwa amekamatwa kwa mahojiano zaidi

Aidha ameendelea kwa kutaja tukio jingine lililotokea tarehe 8 ambapo watu watatu ambao ni John Lewala, Eliasi George,  na Mateo Leornad walijeruhiwa kwa kukatwa mapanga katika eneo la Unyamikumi kwa kile kilichotajwa kuwa ni mgogoro wa ardhi na kwamba watu watano wamekamatwa kwa kuhusikana tukio hilo ambao ni Christopher Kimoteo, Emanueli Edward, Hamisi Joseph, Agustino Daniel,  na Edward Simbu

Kamanda amesema  jumla ya matukio mawili yameripotiwa kwa wiki iliyopita na moja la siku ya leo. Amesema ni vyema uhalifu unapotokea kutoa taarifa mapema kwa vyombo vya sheria na si kujichukulia sheria mkononi


 

 

Source:SR/

Ed: BM

Date: Feb 11/02/2013

 

SINGIDA

Wafanyabiashara ndogo ndogo wa soko kuu la manispaa ya Singida wameiomba serikali kuwapatia mikopo isiyokuwa na riba ili kufikia malengo wanayoyahitaji.

Baadhi ya wafanyabiashara wa soko hilo wakati wakizungumza na Standard radio.

Akizungumza kwa niaba ya wafanya biashara wenzake, Bw. Omari shabani amesema chanzo hasa cha kuzorota kwa biashara zao ni kutokana na kudaiwa riba, pindi wanapochukua mikopo kitu kinachopelekea kupata hasara siku hadi siku.

 Vilevile ameendelea kusema Serikali iangalie suala la ushuru kwani hakuna kiwango  maalum  cha kulipia ushuru, badala yake wamekuwa wakipandishiwa ushuru mara kwa mara.

Naye Bw Shabani Saidi ambaye pia ni mfanyabiashara wa soko hilo ameiomba serikali kuongeza kiwango cha mikopo  ili kukuza biashara  zao

Sambamba na hayo wamesema wafanyabiashara washirikiane na kuunda kamati maalum ya kusimamia biashara zao ili kuhakikisha wanapata haki zao.


 

Source:SR/

Ed: BM

Date: Feb 11/02/2013

SUMBAWANGA

Mwanamke mmoja mkazi wa kijiji cha Mkoe kata ya Nyangalua ambaye ni mlemavu wa ngozi Albino, amevamiwa nyumbani kwake na kukatwa mkono na watu wasiojulikana alfajiri ya leo na kutoweka nao kusikojulikana.

Akizungumza mapema leo, Daktari anayemuhudumia mama huyo hosipitali ya Rukwa Dk, Rashidi Lugisha, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema majeruhi huyo alifikishwa hospitalini hapo akiwa amepoteza fahamu kutokana na kuvuja damu nyingi.

Aidha, Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Rukwa, Jacob Maluwanda amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema tayari wameshafika kwenye eneo la tukio,  umbali wa kilomita sitini kutoka Sumbawanga mjini.

Amesema upelelezi unaendelea ili kuwabaini watu waliotenda unyama huo na kuahidi kutoa taarifa endapo uchunguzi ukikamilika.

 


 

Source:SR/

Ed: BM

Date: Feb 11/02/2013

MWANZA

Mwanachuo wa chuo kikuu cha SAUT kilichopo Nyegezi Malimbe mkoani Mwanza amevamiwa na watu wanne waodhaniwa kuwa ni majambazi na kumpora baadhi ya vitu vyake.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Ernest  Mangu amesema kuwa tukio hilo limetokea jana majira ya saa 9 usiku eneo la Nyegezi Malimbe Kata ya Mkolani wilaya ya Nyamagana.

Amemtaja mwanachuo aliyeporwa vitu vyake kuwa ni Catherine Antony  ambapo  majambazi hao wakiwa na mapanga, na kupora kompyuta  Laptop aina ya HP na simu mbili aina ya Samsung Galaxy  vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni moja  na laki moja na elfu tisini.

Kamanda huyo amesema, jeshi la polisi mkoani Mwanza linaendelea kuwasaka watu waliohusika na tukio hilo.

Wakati  huo huo mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Zacharia Stephano  anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 20 na 25  makazi yake hayakujulikana,  ameuawa na wananchi baada ya kutuhumiwa kuiba betri ya gari.

Kamanda  Mangu amesema  tukio hilo limetokea jana majira ya saa kumi na moja alfajiri maeneo ya Furahisha kata ya Kirumba mkoani Mwanza.

Amesema kuwa marehemu ameuawa baada ya kutuhumiwa na wananchi kuwa  alikuwa akiiba  betri ya gari yenye namba za usajili T.265 AUD aina ya Scania. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya mkoa Sekou Toure kwa uchunguzi zaidi.

Jeshi la polisi linamshikilia Slaji Ismail mwenye umri wa miaka (38) mkazi wa Bunda kwa mahojiano kuhusiana na tukio hilo.


 

Source:SR/Hawa

Ed: BM

Date: Feb 11/02/2013

SINGIDA

Wazazi wametakiwa kutowaficha watoto wao wenye ulemavu badala yake wawapeleke wapate elimu itakayowasaidia katika maisha yao.

Hayo yamesemwa na  mratibu wa  mafunzo ya elimu ya ujasiriamali mkoani Singida Bi  Amina Abubakari Msaghaa wakati akizungumza na standard Redio leo  ofisini kwake.

Mratibu  huyo amesema walemavu wakipatiwa elimu  watajua jinsi gani waendeshe biashara zao, vilevile njia za kujikinga na maambuzi ya VVU na kuzuia mimba za utotoni.

Bi Amina pia ametoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano kwa walemavu kuhusu suala  la kupata elimu ya nadharia na vitendo.


 

 

Source:SR/

Ed: BM

Date: Feb 11/02/2013.

MUSOMA

Watu wasiojulikana wamemuua kwa kumnyonga shingo mwanamke mmoja kwa kutumia kanga yake katika eneo la mgarajabo manispaa musoma mkoani Mara

Kamanda wa polisi wa mkoa wa mara Absalom Mwakyoma amesema tukio hilo limetokea hivi karibuni jirani na eneo ambalo miaka mitatu iliyopita watu 17 familia moja waliuwawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana

 

Mwakyoma amesema kando ya mwili wake zimekutwa nguo za ndani zikiwa zimechanwa na dumu la kuchotea maji likiwa mita 20 tokea mwili ulipokuwa, nywele zake zilikutwa zimefungwa  kwenye kijiti kichakani huku khanga  ikiwa shingoni  ulimi wake ukiwa nje  na kinyesi  pembeni.

 

Aidha amesema kuwa  jeshi la polisi  linaendelea na uchunguzi, sambamba na kuwasaka watu waliohusika na kitendo hicho cha kikatili. Ametoa wito kwa wananchi wataokuwa na taarifa  za watu  waliohusika na mauaji  hayo,  wazitoe kwa siri  kwa vyombo vya ulinzi  na usalama ili sheria ichukue mkondo wake.


 

Source:SR/Chami

Ed: BM

Date: Feb 11/02/2013

 

SINGIDA

Wanawake wawili wakazi wa majengo tarafa ya Itigi wilayani Manyoni mkoani Singida, wameachiwa huru na mahakama kwa miezi kumi na mbili kwa sharti la kutotenda kosa lolote.

Mahakama kuu kanda ya kati, imewaachia huru wanawake hao waliokuwa wakikabiliwa na shtaka la kumtorosha mtoto wa miaka mitano na kumtupa kwenye kisima cha maji.

Akisoma shtaka hilo, wakili wa serikali Bw. Hemed Seif amesema washtakiwa walitenda kosa hilo tarehe kumi na saba mwezi Machi mwaka 2005 katika eneo la majengo, tarafa ya Itigi.

Walioachiwa huru na mahakama hiyo ni Bi. Chiku Mlowezi na Mwadawa Hamis, ambao wanadaiwa siku ya tukio walikwenda nyumbani kwa Hawa Hamis na kumkuta mtoto akicheza na watoto wenzake na kumchukua wakidai kumpeleka kwa kinyozi kunyoa nywele, na kwenda kumtumbukiza kisimani.

Mtoto huyo aliokolewa na wasamaria wema waliompeleka hospitali kupata matibabu na alipopona aliwataja watu walitenda kosa hilo. Washtakiwa wamekiri kutenda kosa hilo na Jaji Laurent Kaduri ametoa hukumu ya kesi hiyo.


 

Source:AFP

Ed: BM

Date: 11 February 2013.

 

KHARTOUM

Mtaalam wa haki za binadamu wa Umoja wa mataifa amesema idara ya usalama nchini Sudan, inawashikilia viongozi wa upinzani bila kuwafungulia mashtaka na kutowapatia huduma za afya wanazohitaji.

Mtaalam huyo wa haki za binadamu wa  Umoja wa mataifa Mashood Adebayo Baderin, ameeleza kusikitishwa kutokana na kukamatwa kwa viongozi wa upinzani na watu wengine, ingawa hakutoa maelezo zaidi.

Ameitaka serikali ya Sudan kuwaachia huru au kuwafungulia mashtaka kwa kufuata vifungu vya sheria za nchi hiyo na kuwafikisha mahakamani.

Taarifa iliyotolewa na Umoja wa mataifa, imeitaka serikali ya Sudan kukomesha unyanyasaji unaofanywa na idara ya usalama, ambayo imekuwa ikizuia maandamano na kutovipa uhuru vyombo vya habari.

Sudan imekuwa ikikumbwa na maandamano ya mara kwa mara yanayotekelezwa na watetezi wa demokrasia,  wanaotaka kufanyika mapinduzi dhidi ya rais Omar al-Bashir ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1989. Mapinduzi kwa njia ya maandamano yamewaondoa madarakani viongozi wa nchi za Misri, Libya na Tunisia.


 

Source:AFP

Ed: BM

Date: 11 February 2013.

 

DAMASCUS

Mwakilishi maalum wa Umoja wa mataifa katika nchi za Kiarabu amemtaka kiongozi wa waasi nchini Syria kufanya mazungumzo na serikali ya nchi hiyo, kufuatia mapigano makali kutokea jana kati ya waasi na vikosi vya serikali.

 

Mwakilishi huyo maalum wa Umoja wa mataifa Bw. Lakhdar Brahimi amekutana na kiongozi wa upinzani  Ahmed Moaz al-Khatib katika mji mkuu wa Misri, Cairo na kumtaka afanye mazungumzo na serikali ya nchi hiyo.

 

Shirika la kutetea haki za binadamu nchini Syria, limekuwa likikusanya taarifa kutoka hospitali za kiraia na kijeshi, limesema watu hamsini wamekufa jana katika ghasia zilizotokea katika nchi nzima. 

 

No comments: