Saturday, February 9, 2013

TAARIFA YA HABARI SR FM FEB 9, 2013 17:00


SINGIDA

Wito umetolewa kwa wakazi wa Singida kushirikiana na serikali pamoja na asasi zisizo za kiserikali katika kupambana na kupunguza ongezeko la watoto wa mitaani au wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Wito huo umetolewa leo na mwalimu mkuu msaidizi wa kituo cha asasi ya The Agape Chriatian Orphans Children Care Support  ACOCAS, kilichopo katika kata ya Mandewa Manispaa ya Singida, Bw. Joel Manase wakati akizungumza na Standard redio kituoni hapo.

Bw. Manase amesema, ni jukumu la kila mtu katika jamii kuhakikisha anatumia kila njia kwa hali na mali ili kupunguza ongezeko la watoto wa mitaani ama waishio katika mazingira magumu.

Amesema kuwa, kituo hicho chenye zaidi ya watoto mia moja kinachojishughulisha na kutoa msaada wa elimu kuanzia ngazi ya chekechea na wengine shule za msingi pamoja na wale hawakufanikiwa kujiunga na shule. 

Amesema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto kama upungufu wa majengo, mahudhurio mabaya kwa baadhi ya watoto kutokana na walezi au wazazi kuwatumia katika shughuli za uzalishaji mali. Changamoto nyingine ni kukosa ufadhili kwani kwa sasa kinaendeshwa na kanisa la TAG.


Source:SR

Ed:BM

Date: 9 February 2013.

 

BIHARAMULO

Jeshi la Polisi wilayani Biharamulo Mkoani Kagera limefanikiwa kuzima tukio la uharifu kwa kuwapiga risasi na kuwaua majambazi wawili wakati wakiwa katika harakati za kuvamia wafanyabiashara na kuwapora

Tukio hilo limetokea Februari 8 mwaka huu katika kijiji cha Nyabusozi, ambapo kundi la watu wanaosadikiwa kuwa majambazi wakijiandaa kuvamia, wanachi walitoa taarifa kwa jeshi la polisi ambao waliwazingira na kufanikisha kuua wawili huku wengine wakikimbia

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera Phillip Kalangi ameiambia Standard Radio kuwa katika tukio hilo majambazi hao wameacha Bunduki aina ya SMG na risasi 20, na kwamba jeshi la polisi linaendelea kuwasaka wengine

Aidha,  kamanda Kalangi amesema mafanikio hayo yametokana na ziara ya mkuu wa wilaya hiyo Bw. Richard Mbeho na Kamati yake ya ulinzi na usalama hivi karibuni katika kata ya Runazi, ambapo waliendesha zoezi la kupiga kura kuwabaini wahalifu na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi

Hata hivyo, kamanda huyo amewataka wananchi kutoa taarifa kwa viongozi husika pale wanapoona raia wanaowatilia mashaka ili kuepusha madhara ya uhalifu.          EndS

Source:SR

Ed:BM

Date: 9 February 2013.

 

ZANZIBAR

Zanzibar, nchi yenye wakazi zaidi ya milioni moja, na wenye kufuata utamaduni wa Kiislam ni miongoni mwa nchi zilizokuwa na idadi kubwa ya wasichana wanaolazimishwa kuolewa wakiwa na umri mdogo.

Utafiti uliyofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) umeonesha kuwepo kwa tatizo la kuwalazimisha wanafunzi kuolewa mapema visiwani Zanzibar, mjini na vijijini.

Hata hivyo, ripoti ya utafiti huo imebaini kuwa takwimu zilizopatikana ni chache kulinganisha na hali halisi kutokana na kuwa ndoa nyingi za kulazimishwa hazifikishwi katika vyombo vya sheria.

Kwa jumla takwimu za Wizara ya Elimu, ni kesi 32 za kulazimishwa kuolewa zilirekodiwa mwaka 2011, na kwamba kesi nyingi hazifikishwi polisi isipokuwa wanafamilia husuluhishana wenyewe kwa wenyewe na kwa wale wanaokataa suluhu ndiyo wanaofikishana polisi na mahakamani.

Aidha kwa mujibu wa shirika la kimaitaifa la kuchangia maendeleo ya watoto (PLAN) wasichana zaidi ya millioni 14 wanaolewa wakiwa na umri chini ya miaka 18 katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Inakisiwa kuwa katika kila dakika moja, watoto wa kike 19 wenye umri chini ya miaka 18 wanaolewa kwa nguvu duniani huku nchi za Chad, Niger, na Mali zikiongoza.

Source:SR

Ed:BM

Date: 9 February 2013.

 

 

DODOMA

Serikali imewasilisha bungeni muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali na kuomba kuzifanyia marekebisho sheria nane ikiwamo ya udhibiti wa fedha haramu.


Akiwasilisha muswada huo bungeni mjini Dodoma, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, amesema sheria hiyo sura ya 423 kwa kuongeza aya C kwenye tafsiri ya neno kufadhili ugaidi.


Amesema sehemu hiyo imefanyiwa marekebisho kwa kuzingatia ushauri wa Kamati ya Bunge na kwamba marekebisho yanayopendekezwa yanalenga kuongeza kwenye tafsiri ya kosa la kufadhili ugaidi.


Amesema tafsri ya neno hilo kama ilivyo sasa haijumuishi matendo hayo na kusababisha kuacha mwanya kwa wahalifu kutumia fursa hiyo kukamilisha malengo yao.


Jaji Werema amesema serikali inapenda kufanya marekebisho kwenye sheria ya kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu, kwa lengo la kutoa ufafanuzi kwa mahakama ziwe na uwezo wa kusikiliza mashauri chini ya sheria hii kuwa ni mahakama ya hakimu mkazi au mahakama ya wilaya

No comments: