Monday, February 11, 2013

TAARIFA YA HABARI FEBRUARY 11, 2013 SAA 11 JIONI

Source:SR/Bandola

Ed: BM

Date: 11 February 2013.

SINGIDA

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida Bw. Manju Msambya amewataka walimu, viongozi na wananchi Kutokutumia mali za shule kama Viti meza na baadhi ya vitendea kazi shuleni katika mikutano ya hadhara.

Bw. Msambya amesema hayo wakati akikagua shule ya sekondari Mwaru, iliyopo katika kata hiyo kabla ya kuelekea kwenye mkutano wa hadhara uliyofanyika katika kijiji cha Kaugeri  jana  katika kata  ya Mwaru wilayani Ikungu mkoani Singida.

Bw. Msambya amesema kuwa meza na madawati ni michango ya wazazi ili kuweza kuepukana na adha wanazopata wanafunzi na walimu kama vitu hivyo havipo.

Aidha,  Mkuu huyo wa wilaya ya Ikungi ameonya  kuwa matumizi mabaya ya mali za taasisi kama Shule,  yatasababisha  kushuka kwa kiwango cha elimu hapa nchini. 


Source:SR/Limu

Ed: BM

Date: 11 February 2013.


SINGIDA

Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone amemsimamisha kazi afisa ardhi wilaya ya Manyoni pamoja na wasaidizi wake wawili kwa muda usiofahamika, ili kupisha uchunguzi unaofanywa na tume maalum kuchunguza tuhuma mbalimbali zilizotolewa na wananchi dhidi ya maafisa hao.

Afisa wa ardhi aliyesimamishwa kazi wilayani Manyoni ni Bw. Leonard Msafiri na wasaidizi wake ni John Chima na Kenedi Chigulu.

Mkuu huyo wa mkoa wa Singida, amesema ameunda tume ambayo inawajumuisha kamanda wa polisi mkoa wa Singida, mkuu wa mageraza mkoa, mwenyekiti wa baraza la ardhi mkoa, afisa ardhi mkoa, mkuu wa wilaya ya Manyoni, TAKUKURU mkoa  na afisa usalama mkoa.

Dk. Kone amesema tume hiyo itafanya kazi kwa muda wa wiki moja na itatoa mapendekezo ya kuchukua ili kumaliza kabisa malalamiko ya wakazi wa Manyoni mjini wanaowalalamikia maafisa hao wa ardhi.

Hivi karibuni Dk. Kone  alisimamisha kwa muda usiofahamika shughuli zote za ugawaji wa viwanja Manyoni mjini, hadi hapo migogoro ya viwanja iliyopo, itakapopatiwa majawabu yatakayoridhisha wakazi wa mji huo.

Pamoja na kusimamisha shughuli za ugawaji viwanja, pia uendelezaji wa viwanja vyote kwa sasa unasimamishwa kupisha  tume maalum kufanya uchunguzi,  juu ya migogoro ya viwanja.

Maafisa ardhi wa halmashauri ya wilaya ya Manyoni wanadaiwa kusababisha migogoro mikubwa ya ardhi, ikiwa ni pamoja na kupora ardhi za watu na kutolipa fidia.


Source:SR/Eliza

Ed: BM

Date: 11 February 2013.

SINGIDA

Wito umetolewa  kwa watahiniwa mtihani wa Kidato cha Sita wa taifa ulioanza leo katika vituo vyote vilivyosajiliwa Mkoani Singida, kutoshiriki udanganyifu  kwa njia yeyote ile, ili kuepuka kufutiwa matokeo yao.

Wito huo umetolewa na afisa elimu wa mkoa wa Singida Bi. Fatuma Kilimia wakati akizungumza na Standard Radio ofisini kwake.

Amesema  kuwa mkoa huu una vituo 12 vilivyosajiliwa kwa ajili ya mitihani hiyo ya taifa kidato cha sita inayoendelea nchi nzima ambapo watahiniwa 843 wamesajiliwa kufanya mitihani hiyo.

Bi. Kilimia amesema mitihani hiyo iliyoanza leo inatarajiwa kumalizika februari 27 mwaka huu. Amevitaja vituo vilivyosajiliwa kuwa ni Mwenge, Dung’unyi, Kijota, Ilongero, Tumaini, Itigi, Mwanzi, tumaini, Manguanjuki, Ikungi, Palloti, Rurumba na kituo binafsi cha Mwenge.

Aidha amewataka wazazi kutoshiriki katika udanganyifu wa mitihani kwa namna yeyote ile, bali wawaombee watoto wao ili waweze kufanya mitihani kwa utulivu na wasipate vishawishi, kwani kufanya hivyo kutapelekea kufutiwa matokea yao jambo ambalo ni aibu katika jamii na taifa kwa ujumla.

Source:

Ed: BM

Date: 11 February 2013.

 
DAR ES SALAAM

Ofisi ya mkaguzi na mkaguzi wa hesabu za serika imekuwa ya kwanza kuunganishwa na mkongo wa mawasiliano wa taifa.

Jumla ya ofisi kumi na mbili za ofisi ya mkaguzi na mdhibiti wa serikali Rudovic Utto, zimeunganishwa ili kusaidia utendaji kazi mzuri na wenye ufanisi na haraka zaidi

Mdhibiti na mkaguzi huyo amesema mkongo huo uliogharimu kiasi cha bilioni mia nne arobaini na saba utarahisisha mawasiliano tofauti na ilivyokuwa awali,  ikiwa ni pamoja na kufanya mawasiliano yanayojumisha watu wa mataifa na sehemu mbali mbali.

Aidha ameongeza kuwa kiwango hicho cha fedha kimeweza kulipwa kwa awamu na kukamilisha fedha hizo.


 

Source:

Ed: BM

Date: 11 February 2013.

 

MANYARA

Watu watatu wamejeruhiwa kufuatia mapigano yaliyotokea baina ya wafugaji wakigombea maeneo ya malisho na sehemu ya kunyweshea maji.

Mapigano hayo yametokea katika kata ya Elachini ambapo wabarabaigi na wamang’ati walikuwa wakigombea maeneo hayo.

Mkuu wa wilaya ya Mbulu Anatori Choya amedhibitisha kutokea mapigano hayo ambapo majeruhi wamepelekwa hospitali kwa matibabu na ulinzi umeimarishwa.

Aidha, ameongeza kuwa chanzo cha ugomvi huo ni kutokana na baadhi ya maeneo kukosa mvua na kusababisha kuwepo na ukame jambo lililopelekea wafugaji hao kugombea eneo dogo la kulishia, ambalo lina malisho mazuri na kusababisha kila mtu kutaka kulishia eneo hilo.


 

Source:SR/Irimina & Simtovu

Ed: BM

Date: 11 February 2013.

 

 

SINGIDA

 

Mratibu wa mafunzo ya wanawake jamii, ameiomba serikali kuelimisha vijana juu ya elimu ya ujasiliamali ili kupunguza ongezeko la vijana wa mitaani.

 

Mratibu huyo Bi. Amina Abubakar Msaghaa wakati akizungumza na Standard radio ofisini kwake leo. Amesema mradi wa ushonaji umeanza tangu mwaka 2009, ukiwa na lengo la kupunguza ongezeko la vijana wasio na kazi, kuwaelimisha na kuwapatia ajira.

 

Hadi kufikia mwaka huu, mradi huo una jumla ya wanafunzi mia mbili sabini na mbili walio kwenye mafunzo, wengine kumi wameshindwa kuendelea na mafunzo kutokana na matatizo ya kijamii.

 

Aidha, amesema mafunzo hayo hutolewa kwa walemavu, wajane, yatima na vijana wasiokuwa na uwezo wa kulipia gharama za mafunzo husoma bure. Amesema mchango unaotozwa kama ada ni mdogo ambao unamwezesha kila mtu kumudu gharama.

 

Ametoa wito kwa serikali isaidie kuwaelimisha vijana kuhusu mafunzo hayo na kuishukuru serikali kwa kuwapa jengo la kutolea mafunzo, pamoja na shirika la viwanda vidogo vidogo nchini SIDO kwa kutoa vifaa vya kusindika vyakula.


Source:SR/

Ed: BM

Date: Feb 11/02/2013.

SINGIDA

Wakazi watatu wa kijiji cha Ughaugha (B) Manispaa ya Singida, wamenusurika kufa baada ya kushambuliwa kwa majembe na kundi la watu 12 kwa kile kinachodaiwa kuwa ni ugomvi wa mashamba

Miongoni mwa wakulima waliovamiwa hivi karibuni wakiwa shambani, ni  pamoja John Leonard ambaye amewaambia waandishi wa habari kuwa siku ya tukio wakiwa shambani, ghafla walivamiwa na kundi la watu  na  kushambuliwa

Aidha amesema katika tukio hilo inaonekana yeye alikuwa mlengwa kwani watu hao walianza kumkata kwa hengo kwenye paji lake la uso, na kusababisha aanguke chini na kupoteza fahamu.

Watu hao wamelazwa katika wodi namba tatu katika hospitali ya mkoa Singida, na hali zao zinaendelea vizuri.

Uvamizi huo unadaiwa kuwa umechangiwa kwa kiasi kikubwa na ugomvi wa kugombea shamba kati ya John na Dk. Damas Simbu, anayefanyia kazi jijini Dar-es-salaam.

 


Source:AFP

Ed: BM

Date: 11 February 2013.

 

BAMAKO

Mlipuko mkubwa umetokea  leo asubuhi katika mji wa Gao uliopo kaskazini mwa Mali, saa chache baada ya mwanamgambo wa kiislam kushambulia kwa risasi vikosi vya jeshi vya Ufaransa na Mali.


Vikosi vya Mali vimeliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kuwa sauti ya mlipuko umesikika kutoka kaskazini mwa mji wa Gao, katika kizuizi cha barabara   ambako mashambulizi ya kujitoa muhanga yalitokea mwishoni mwa wiki.

 
Source:AFP

Ed: BM

Date: 11 February 2013.

 

JUBA

Jeshi la Sudan kusini limesema watu ishirini na nne wamekufa katika mapigano yanayoendelea katika mpaka wa nchi ya Sudan na Sudan kusini.

Msemaji wa jeshi la Sudan kusini Philip Aguer amesema vikosi vya jeshi vimewaua wapiganaji saba wanaoungwa mkono na Sudan baada ya kuvuka mpaka unaotenganisha nchi hizo.

Jeshi la Sudan kusini limeteka roli la jeshi la Sudan kaskazini lililokuwa likitumiwa na wapiganaji katika mji wa Obed kwenye jimbo la Upper Nile kaska\zini mashariki mwa nchi hiyo.

Katika shambulio jingine katika mpaka huo, waasi wa Sudan’s People’s Liberation Movement SPLM wanawatuhumu wanamgambo wanaoungwa mkono na Sudan kusini kwa kushambulia kijiji na kuua watu kumi na saba.

 
Source:AFP

Ed: BM

Date: 11 February 2013.

 
BEIJING

Serikali ya China imetangaza kuwa watu wawili wamepatikana na ugonjwa wa mafua ya ndege katika mji wa kusini magharibi wa Guiyang.

Shirika la habari la China, Xinhua limesema wagonjwa hao waliopata maambukizi ya mafua ya ndege wana hali mbaya. Dalili za watu hao kuugua ugonjwa wa mafua ya ndege aina ya H5N1 zilizanza kuonekana tarehe mbili na tatu mwezi huu.

Watu waliokuwa karibu na wagonjwa hao, pia wamafanyiwa uchunguzi, ingawa hajapatikana aliyepata maambukizi ya ugonjwa huo.  Kwa mujibu wa Shirika la afya duniani WHO, ugonjwa wa mafua ya ndege umeshaua watu mia tatu sitini na tano ulimwenguni, tangu ulipogundulika mwaka 2003.
 
China ni miongoni mwa nchi zilizo katika hatari zaidi ya maambukizi ya mafua ya ndege kutokana na kuwa na miradi mingi ya ufugaji wa kuku katika maneneo ya vijijini karibu na maeneo wanayoishi watu. 

 

No comments: