Friday, February 15, 2013

TAARIFA YA HABARI KUTOKA STANDARD


Source:SR/Lyatuu

Ed: BM

Date: 15 February 2013.

 

SINGIDA

Walimu wa shule ya msingi Unyakumi manispaa ya Singida wameiomba serikali kutimiza mahitaji yao ili kuboresha kiwango cha taaluma

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Bw. Joachim Msechu amesema hayo wakati akizungumza na Standard radio shuleni hapo.

Amesema kiwango cha elimu kinaendelea kushuka kutokana na walimu kukumbwa na changamoto nyingi

Mwalimu Msechu ametaja changamoto hizo kuwa ni ukosefu wa nyumba za walimu, kucheleweshewa mishahara, na kulipwa mshahara mdogo

Aidha, amesema utoro wa wanafunzi katika shule ya Unyakumi umekithiri, kutokana na wazazi kukosa ushirikiano na walimu hali inayosababisha kudidimia kwa sekta ya elimu.

Bw Msechu ametoa wito kwa serikali kuhakikisha mahitaji ya walimu ikiwemo ujenzi wa nyumba za walimu vinapatikana ili kuinua kiwango cha elimu

 


Ed: BM

Date: 15 February 2013.

 

DAR ES SALAAM

Menejimenti ya Benki ya NMB imesema imegundua kuwepo kwa taasisi inayojitambulisha kama Tanzania Loans Society ikidai kuwa mshirika wa benki hiyo katika kutoa huduma za kibenki.

Taasisi hiyo imedaiwa kuwa, kwa kutumia mtandao wake wa intaneti imekuwa ikijinadi kutoa mikopo ambayo fedha zake zimeidhinishwa na NMB kupitia kwa mameneja wa matawi.

Aidha, Tanzania Loan Society pia inadaiwa kueleza kwamba fomu za maombi ya mkopo na malipo ya usajili vinaweza kulipwa kwa kutumia namba ya simu ya mkononi

Menejimenti ya NMB imezidi kuwatahadharisha wateja wake na umma kwa ujumla kwamba, haina ushirika ama makubaliano yoyote na taasisi hiyo katika shughuli zake

NMB imesema kuwa hutoa mikopo kupitia matawi yake tu, na kwamba hakuna namna yoyote ambayo inaweza kusababisha gharama za maombi ya mikopo au mikopo kutolewa kupitia simu za mkononi.


 

Source:Tanzania daima

Ed: BM

Date: 15 February 2013.

 

DAR ES SALAAM

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imetoa ajira mpya kwa walimu wa shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu nchini.

Waziri wa wizara ya elimu Dk. Shukuru Kawambwa, amesema utoaji wa ajira hizo umefuata tathmini zilizofanyika ili kubaini maeneo yenye upungufu wa walimu, ili kuweza kupeleka walimu kwa wingi katika maeneo hayo

Waziri Kawambwa amesema kwa sasa taifa lina upungufu wa walimu wa masomo ya Sayansi na Hesabu,  na mwaka huu wameajiri walimu elfu mbili na thelathini na saba.

Kwa mujibu wa Waziri Kawambwa, wameajiri walimu zaidi ya elfu kumi na tatu wa ngazi ya cheti ambapo walimu hao wamepangwa katika shule za msingi zilizopo kwenye halmashauri, na 41 wamepangwa katika shule za mazoezi zilizo chini yake.

Amesema kwa upande wa wahitimu wa elimu ya shahada na stashahada, wameajiri walimu zaidi ya elfu kumi na mbili kufundisha shule za sekondari zilizoko chini ya halmashauri, 59 wamepangwa kuwa wakufunzi wa vyuo vya ualimu, huku walimu 21 wamepangwa kufundisha shule za sekondari za mazoezi.

 

Ed: BM

Date: 15 February 2013.

GEITA

Jeshi la polisi mkoani Geita linamshikilia Mchungaji wa Kanisa la PAGT, Isaya Rutta , mkazi wa Kijiji cha Katoro, Wilaya ya Geita, kwa tuhuma za kuchinja ng’ombe mmoja na mbuzi wawili na kusababisha vurugu kati ya waislamu na Wakristo.

Vurugu hizo zimetokea juzi na kusababisha kifo cha mtu mmoja ambaye ni mchungaji wa kanisa moja wilayani Geita na watu wengine 10 kujeruhiwa

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Paulo Kasabango, amesema mtuhumiwa amekamatwa juzi katika kijiji hicho ambapo inadaiwa kuchinja mifugo bila ya kuhusisha daktari wa mifugo kwa lengo la kuthibitishwa kama nyama hiyo ni salama kuliwa na binadamu

Kasabango amesema kuwa mbali na kukamatwa kwa kosa hilo, pia anadaiwa kufanya makosa ya kuchinja eneo ambalo si rasmi kwa mujibu wa sheria ya kifungu namba 17 ya mwaka 2003.

Amesema kuwa mtuhumiwa mwingine Ramadhani Pastory, ambaye kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi, anadaiwa kumuua Mchungaji Mathayo Kachila wa Kanisa la PAGT Buseresere na kwamba atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo wakati wowote akipata nafuu.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Magalula Saidi Magalula, amekemea kitendo walichofanya baadhi ya wananchi, kujichukulia sheria mkononi na kuhatarisha amani.

 

 

 

 

Source:Tanzania daima

Ed: BM

Date: 15 February 2013.

 

DAR ES SALAAM

Jeshi la Polisi na askari wa ulinzi wa Mamlaka ya Bandari (TPA), wamefanikiwa kuwakamata maafisa wa serikali na wamiliki wa bandari kavu kwa tuhuma za wizi wa madini aina ya tantalite yaliyoonesha yametoka Tanzania.

Maafisa hao saba na wengine watatu ambao hawajakamatwa, wamefunguliwa jalada la kesi ya wizi wa mali isafirishwayo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amewataja maafisa hao kuwa ni mfanyakazi wa wizara yake, Godson Mnkeni, mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Mohamed Mbupu, ambaye alitoa hati ya mzigo kusafirishwa, mmiliki wa kampuni na wakala wa kusafirisha mizigo GFC, Francis Mutalemwa na msaidizi wake, Christopher Andrew.

Wengine waliokamatwa ni mmiliki wa Kampuni ya bandari kavu ya Rudi Holding ambaye ni raia wa Ufaransa, Gren Baniaux, mmiliki wa Kampuni ya PMM, Judith Mhina na mtendaji wake, Edward Bachwa, ambao wanahojiwa ili kubaini nani anahusika.

Dk. Mwakyembe amewataja watuhumiwa ambao hawajakamatwa kuwa ni Ofisa wa Usalama wa Taifa ambaye alikuwepo wakati wa tukio la wizi huo, Hamisi Haji, Mmiliki wa Kampuni ya Damco ambaye jina lake halijapatikana pamoja na raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), aliyefahamika kwa jina moja la Christian.

Aidha, Dk. Mwakyembe amesema kuwa atawataja maafisa wote wanaowakingia kifua watu waliokamatwa kwa tuhuma mbalimbali bandarini.

No comments: