Thursday, February 21, 2013

TAARIFA YA HABARI KUTOKA STANDARD RADIO


Source:SR/Beatrice & Mary

Ed: BM

Date: 18 February 2013.

SINGIDA

Mkazi wa kijiji cha Munghamu kata ya Kinyeto tarafa ya Ilongero Mkoani Singida, Bw. Abbas Mussa ameachiwa huru baada ya kesi ya ubakaji iliyokuwa inamkabili kukosa ushahidi.

Akitoa hukumu hiyo Hakimu wa Mahakama ya Hakimu mkazi Singida Bi. Flora Ndale amesema amemuachia kutokana na ushahidi wa kesi hiyo kuwa hafifu

Imedaiwa kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 30, mwaka 2011 majira ya saa tatu na nusu usiku na kwamba alimbaka Bi. Zainabu Ramadhan wakati akitoka mnadani kwenye shughuli zake za kujitafutia riziki

Amesema kuwa alikutana na mshtakiwa Abbas na alipopishana naye kama hatua mbili nyuma alimpiga ngwara na kuanguka chini, akakabwa kooni na kisha kuingiliwa kimwili kwa nguvu na mshtakiwa.

Imeelezwa mahakamani hapo kuwa, mlalamikaji baada ya kuachiwa aligundua kiasi cha shilingi laki moja na nusu zimepotea na alipiga yowe kuomba msaada kwa majirani wa eneo hilo la tukio, ambao walimkamata hadi alipofikishwa mahakamani


Source:SR/Pascal Buyaga

Ed: BM

Date: 18 February 2013.

 

 

MUSOMA

Watu wawili wamekufa baada ya kuzamishwa katika Ziwa Victoria wilayani Butiama mkoani Mara, na watu wanaosadikiwa kuwa wavuvi haramu waliwagonga mtumbwi na hatimaye mtumbwi wao kuzama

Kamanda wa polisi, Kamishna Msaidizi Absalom Mwakyoma amewataja watu waliozamishwa majini kuwa ni Mwenge Rwansa, mkazi wa kijiji cha Kiemba na King Magessa mkazi wa kijiji cha Kabegi kata ya Nyakatende.

Taarifa za awali za jeshi la polisi zinaeleza kuwa watu hao walikuwa katika msako wa kuwatafuta na kuwakamata wavuvi haramu wanaovua samaki katika Ziwa Victoria kwa kutumia sumu.

Mwakyoma amesema watuhumiwa walifanikiwa kutoroka kwa kutumia mtumbwi wao ambao haujajulikana na miili ya marehemu imepatikana February 16 majira ya saa 5 asubuhi na taratibu za mazishi zinafanyika.

Aidha uchunguzi wa kina umeanza ili kubaini watuhumiwa waliotenda kosa hilo ili wakamatwe na kufikishwa mahakamani


 

 Source:SR/Matinde

Ed: BM

Date: 18 February 2013.

 

MWANZA

Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka jiji la Mwanza Bw. Robert Masunya amewataka wakazi wa jiji la mwanza kuhifadhi maji kutokana na tatizo la umeme.

Wito huo umetolewa mapema leo wakati akizungumza na Standard radio ofisini kwake. Bw. Masunya amesema kuwa tatizo la umeme limekuwa likiathiri mitambo ya MWAUWASA katika kusukuma maji ambapo umeme umekuwa ukikatika si chini ya saa 6 hali inayopelekea wakazi hao kukosa maji

Meneja Uhusiano huyo amesema kuwa oparesheni ya kusitisha huduma ya maji kwa wateja ambao hawalipii bili zao inaendelea pamoja na kuwataka wakazi kutoa taarifa pindi mwananchi atakapobainiwa kuwa ni mwizi wa maji.

 Amewaomba wakazi wa jiji la Mwanza kuwa na utaratibu wa kuhifadhi maji ili yasaidie pindi umeme unakapokatika.

 

 


 

Source:SR/SAADA

Ed: BM

Date: 18 February 2013.

 

 

SINGIDA

Mkurugenzi wa manispaa ya Singida Bw. Mathias Mwangu amewataka watu wanaofunga vitambaa vya matangazo barabarani kuviondoa pindi muda wake unapomalizika.

Bw.Mwangu amesema hayo leo wakati akizungumza na Standard Radio. Ofisini kwake.

Amesema kuwa elimu inatakiwa kutolewa kwa wananchi au wadau wanaohusika na matangazo ili kutoka vitambaa au mabango ambayo muda wake umekwisha.

Aidha, Mkurugenzi huyo wa manispaa ya Singida Bw. Mwangu, amesema elimu itolewe kuhusu athari za kuacha matangazo yaliyopitwa na wakati na baadaye hatua za kisheria zitachukuliwa kwa atakayekiuka agizo hilo.

Source:SAPA

Ed: BM

Date: 18 February 2013.

 

 

BAMAKO

Vikosi vya jeshi la Ufaransa kwa kushirikiana na vile vya Mali jana vimeurejesha mji wa Bourem ambao umekuwa ukitumiwa na wapiganaji wa Kiislam nchini Mali kupanga mashambulizi dhidi ya vikosi hivyo.

Mji wa Bourem upo umbali wa kilomita themanini kaskazini mwa mji wa Gao katika njia panda ya barabara ziendazo katika miji ya Timbuktu na Kidal, miji ambayo inadhibitiwa na majeshi ya Ufaransa na Mali.

Serikali ya Ufaransa imesema inatarajia kuondoa wanajeshi wake wapatao elfu nne nchini Mali mwezi March, na kukabidhi jukumu la ulinzi kwa jeshi la Mali na lile la Afrika AFISMA linaloungwa mkono na umoja wa mataifa.

 

 


 

Source: AFP

Ed: BM

Date: 18 February 2013.

 

 

TUNIS

Waziri mkuu wa Tunisia Bw. Hamadi Jebali leo ameanza mazungumzo na viongozi wa vyama vya siasa ili kuunda serikali mpya, licha ya upinzani mkubwa kutoka chama chake cha Kiislam cha Ennahda.

Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuanza mazungumzo hayo, amevitaka vyama vya siasa nchini humo kufikia makubaliano ili kumaliza ghasia zilizotokea nchini humo tangu February sita baada ya mauaji ya kiongozi wa upinzani Chokri Belaid.

Hata hivyo mwenyekiti wa Chama cha Ennahda Rached Ghannnouchi amepinga chama chake kuwa katika serikali ya Umoja wa kitaifa.

Waziri mkuu wa Tunisia Bw. Jebali ametishia kujiuzulu kama atashindwa kuungwa mkono ili kuunda serikali mpya.

 


 

Source: AFP

Ed: BM

Date: 18 February 2013.

 

CAIRO

Maelfu ya raia wa Misri wameandamana jana katika mji wa Port Said wakidai haki itendeke baada ya mauaji ya raia wengi yaliyotekelezwa na polisi.

Habari zinasema waandamanaji hao wamelazimisha shule na maduka kufungwa, na kuziba reli.

Waandamanaji wanataka haki itendeke kufuatia mauaji ya raia arobaini baada ya kutokea mapigano na polisi mwezi January baada ya mahakama moja kuwahukumu kifo mashabiki ishirini na moja wa mpira wa miguu, kufuatia vurugu zilizotokea katika mpira wa miguu mwaka jana.

Mwezi February mwaka jana, watu sabini na nne mashabiki wa timu ya Al-Ahly walikufa katika vurugu zilizotokea katika mji wa Port Said.


 

Source:AFP

Ed: BM

Date: 18 February 2013.

 

 

CARACAS

Rais Hugo Chavez wa Venezuela ametangaza kupitia mtandao wa Twitter mapema leo kuwa amerejea nchini mwake baada ya kuwa nchini Cuba alikokuwa akipatiwa matibabu ya saratani.

Katika ujumbe kwa wananchi wa Venezuela, rais Chavez amesema amerejea tena nchini mwake na kwamba anamshukuru Mungu na kuwashukuru raia wa nchi hiyo.

Amesema ataendelea kupata matibabu ya ugonjwa wa saratani akiwa nchini Venezuela. 


 

Source :SR:BANDOLA

Ed.

Date 17February 2013

 

SINGIDA

Vijana wametakiwa kusoma kwa bidiii na kutambua kuwa elimu ni hazina isiyofutika tofauti na vitu vingine katika jamii

Kauli hiyo imetolewa na mlezi wa ukwata mkoani Singida Mwl Edward Samwel wakati wa hafla ya kuwakaribisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika chuo cha ufundi VETA ambao ni wanachama wa umoja wa kikristu wa wanafunzi Tanzania (UKWATA)

Amesema vijana wanapaswa kutumia muda huu kwa kufanya maandalizi mazuri ya maisha yao kwa kusoma kwa bidii, kwa kutambua kuwa hivi sasa dunia iko katika utandawazi.

Amesema iwapo vijana hawatajituma kwa kipindi cha ujana wao ni dhahiri hawataweza kuzalisha baada ya nguvu zao kupungua hali ambayo inaweza  kusababisha  familia  kuwa katika mazingira magumu.

Aidha Bw. Samwel ametoa wito kwa vijana kuepuka utumiaji wa madawa ya kulevya ambayo yanaweza kusababisha kutotimiza malengo yao.


 

Source:SR/FS

Ed: BM

Date: 18 February 2013.

 

 

IRAMBA

Mbuzi mmoja  amezaa kiumbe kinachofanana na binadamu katika kijiji cha Kinampanda wilaya ya Iramba mkoani Singida.

 

Wamiliki wa mbuzi huyo Bw.  Iddi Mssoliya na mkewe Bi. Rehema Danford wamesema tukio hilo limetokea Februari 15 mwaka huu, na kwamba kiumbe hicho cha ajabu kilikuwa na ngozi kama ya binadamu.

 

Akiongeana standard Radio nyumbani kwake jana, Bi. Rehema amesema baada ya kubaini tukio hilo alienda kwa afisa ughani katika eneo hilo, ambaye amesema kuwa hiyo ni hali ya kawaida katika suala la ukuaji wa viumbe katika mfumo wa uzazi.

 

Aidha, Afisa kilimo na mifugo huyo Bw. Aron Kilazagaye ametoa wito kwa wananchi kutokuwa na imani potofu kutokana na tukio hilo, bali watambue hiyo ni hali ya kawaida inayoweza kutokea hata katika mfumo wa uzazi wa binadamu.


 

Source: St  Im(madeni)

Ed:

Date: February 18, 2013

 

SINGIDA

Idara za elimu nchini zimetakiwa kuwa na kitabu cha madeni kama mkakati wa kupunguza tatizo la walimu kutumia muda mrefu kufuatilia madeni katika halmashauri zao.

Akiongea na wakuu wa idara za elimu mkoani Singida, Naibu waziri ofisi ya waziri mkuu tawala za mikoa na serikali za mitaa Bw Kassim Majaliwa, amesema hatua hiyo itapunguza malalamiko ambayo yanajitokeza mara kwa mara, kuhusu upotevu wa nyaraka za walimu wanaodai malipo mbalimbali.

Aidha amesema kuwa iwapo utaratibu huo utafutwa itakuwa rahisi kwa idara hiyo kuwasilisha majina na kiasi wanachodai walimu ili waweze kupata stahili zao

 

Kwa upande mwingine amewataka wakurugenzi na maofisa wa idara ya elimu kutoa ufafanuzi wa stahili zao, ili kuepusha malalamiko ambayo yamekuwa yakijitokeza wakati walimu wanapowasilisha madai yao.

 

Source: St  Im(madeni)

Ed:

Date: February 18, 2013

DODOMA
Serikali imedhamiria kusambaza huduma bora za mfuko wa Afya ya Jamii CHF katika mikoa yote nchini, ili watanzania wote hasa wa kipato cha chini  waweze kufaidika na huduma za afya

Naibu Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Agrey Mwanri, ametoa kauli hiyo jana wakati wa uzinduzi wa mfumo mpya wa menejimenti ya taarifa za bima (IMIS) kwa ajili ya mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa

Amesema huduma bora za afya ni haki ya kila Mtanzania, hivyo kuzinduliwa kwa CHF iliyoboreshwa, serikali imedhamiria kusambaza huduma hizo nchi nzima kwa kushirikiana na wadau wengine, ili Watanzania wengi zaidi waweze kufaidika

Meneja wa Mradi wa Health Promotion and System Strengthening Project (HPSS), Manfred Stoermer, amesema CHF iliyoboreshwa, inatumia mfumo mpya wa menejimenti ya taarifa za bima unaotumia teknolojia ya kisasa zaidi.

Naye Mkuu wa kitengo cha mawasiliano na mahusiano cha Vodacom, Joseline Kamuhanda, amesema Vodacom Tanzania inasaidia mradi kama mdau muhimu, kwenye masuala ya mawasiliano.


Source: St  Im(madeni)

Ed:

Date: February 18, 2013

 

SINGIDA

 

Wakristo nchini wametakiwa kufuata mafundisho na kutafuta uzima wa milele na sio pesa, maombezi na mafanikio tu.

Mchungaji Danieli Mwangungulu kutoka Dar es salam amesema hayo wakati akihubiri jana katika kanisa la T.A.G lililopo eneo la Gineri mjini Singida

 

Mchugaji Mwangungulu amesema waumini wamekuwa na mazoea ya kutamani miujiza, uponyaji, na mafanikio, kuliko neno la mungu jambo ambalo limezorotesha imani za waumini walio wengi.

 

Aidha mchungaji Daniel amesema hatua hiyo inaweza kusababisha waumini kupokea imani potofu na kusahau njia ya uzima.

Kwa upande mwingine amewakumbusha kutafuta uzima wa milele kuliko kuwapa ajira watumishi matapeli wanaojali maslahi yao jambo ambalo linatishia imani ya kikristo kwa sasa.


 

Source: St  Im(elimu)

Ed:

Date: February 18, 2013

 

SINGIDA

Kaimu mkuu wa mkoa wa Singida Bw Manju Msambya amesema tatizo la lugha ya kufundishia hasa kwa shule za sekondari, ni moja ya sababu zinazosababisha wanafunzi kufanya vibaya katika mitihani yao.

 

Akiongea katika  mkutano wa Naibu waziri ofisi ya waziri mkuu  tawala za mikoa na  serikali za mitaa Bw Kassim Majaliwa, ambao umeshirikisha wakuu wa idara  za elimu mkoani Singida kwa lengo la kuweka mikakati ya kuboresha elimu, Bw Msambya amesema wakati umefika wa kuangalia lugha ipi ya kufundishia

 

Insert Musambya

Cue in shule ya msingi

Cue out  kwa kutumia kishwahili

 

Aidha amesema inasikitisha kuona viongozi wa kitaifa wakitoa hotuba kwa lugha ya kiingereza wakati ziara za wageni mbalimbali wanapokuja hapa nchini, huku wageni hao wakitumia lugha za mataifa yao kama sehemu ya kudumisha utamaduni wao.


Source: 24 news (madeni)

Ed:

Date: February 18, 2013

 

MOGADISHU

Serikali ya somalia imetangaza donge la dola elfu 50 za Kimarekani  kwa  raia atakayefanikisha  kukamatwa kwa mtu anayehusika na mauaji ya waandishi wa habari nchini humo

 

Hatua hiyo imetangazwa na waziri mkuu wa nchi hiyo Bw Abdi Farah Shirdon ambaye amesema serikali yake inasikitishwa na mauji hayo  na kwamba ina nia ya dhati kuhakikisha waandishi wa habari wanalindwa nchini humo.

 

Chama cha waandishi wa habari pia kimeunga mkono tangazo hilo la serikali na kuongeza kuwa kitasaidia kuharakisha kukakamatwa kwa watu wanaovamia waandishi wa habari.

Zaidi ya waandishi wa habari 18 wameuawa nchini Somalia kwa mwaka uliopita pekee.


 

Source: 24 news (madeni)

Ed:

Date: February 18, 2013

 

KABUL

Waislamu wa Kishia jana wameandamana katika miji mbalimbali ya Pakistan wakiishinikiza serikali ya nchi hiyo kuwatia mbaroni waliosababisha milipuko huko Quetta na kupelekea watu 81 kuuawa na zaidi ya 200 kujeruhiwa.

Shambulio hilo la kigaidi linahesabiwa kuwa ni la pili kwa ukubwa dhidi ya Waislamu wa Kishia katika historia ya nchi hiyo.

Familia za watu waliouawa katika tukio hilo, wamegoma kuwazika watu wao ili kulalamikia vitendo vya kigaidi wanavyofanyiwa huku serikali ikishindwa kudhibiti vitendo hivyo.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch nalo limelaani mauaji hayo ya kigaidi na kumtaka waziri mkuu wa Pakistan kuwafuatilia waliofanya vitendo hivyo vya kigaidi na kuwafungulia mashtaka.

Source:AFP

Ed: BM

Date: 18 February 2013.

NEW YORK

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Bw. Ban Ki-moon anatarajia kuhudhuria katika utiaji saini wa mkataba wa amani ya mashariki mwa jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo utakaofanyika wiki ijayo mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.

Msemaji wa Katibu mkuu wa umoja wa mataifa, Martin Nersiki amesema Katibu mkuu wa umoja wa mataifa tayari ameshapata mwaliko na anatarajia kuhudhuria tarehe 24 February mjini Addis Ababa.

Amesema pia kuwa marais wote walioalikwa kuhudhuria utiaji saini wa mkataba huo wameahidi kuhudhuria na wengine kuahidi kutuma wawakilishi.

Nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Uganda, Uganda, Burundi, Angola, Congo, Afrika kusini na Tanzania zinatarajia kusaini mkataba wa muundo, baada ya kukataa kusaini wakati wa mkutano wa Umoja wa Afrika uliofanyika Addis Ababa mwezi uliopita.

Vikosi vya kulinda amani katika Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo vitakuwa na jukumu la kupambana na makundi yenye silaha ambayo yamekuwa yakifanya uhalifu katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo kwa miaka kumi na tano iliyopita. 

 

No comments: