Friday, March 1, 2013

MH. PINDA KUZINDUA UTUNDIKAJI MIZINGA YA NYUKI KITAIFA MKOANI SINGIDA

Na. Boniface Mpagape     

Serikali kupitia wizara ya maliasili na Utalii imeanzisha siku ya utundikaji mizinga kitaifa mwaka huu, kwa lengo la kuongeza msukumo katika sekta hiyo yenye uwezo wa kuondoa umaskini.

 

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa mkoa wa Singida Dk. Parseko Kone kwa vyombo vya habari leo, imesema uzinduzi wa mkakati huo kitaifa utafanyika Machi 4, wilayani Manyoni mkoani Singida na Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bw. Mizengo Peter Pinda anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

 

Dk. Kone amesema hii ni heshima kubwa kwa mkoa wa Singida na wananchi wake na ni heshima kwa wafuga nyuki wote wa mkoa wa Singida.

 

Amesema ufugaji nyuki ni njia sahihi ya kutumia raslimali za misitu katika kujiongezea kipato, badala ya kuharibu mazingira kwa kukata miti ili kuchoma mkaa kwani ufugaji huo unatunza miti kwa sababu ni chanzo kikuu cha asali.

 

Amewataka wananchi wa mkoa wa Singida kutumia fursa hiyo kwa kuongeza idadi ya mizinga katika mashamba yao, na wale ambao hawajaanza waanze leo. Mkuu wa mkoa wa Singida ametoa ushauri kujiwekea lengo la kutundika mizinga angalau mitano kila mwaka.

 

Aidha, amewaomba wananchi wote siku ya tarehe 4 Machi mwaka huu, kujitokeza kwa wingi katika hifadhi ya nyuki ya Aghondi wilayani Manyoni, ili kushuhudia uzinduzi na kujifunza mbinu mbali mbali za kisasa za ufugaji nyuki.

 

Kauli mbiu ya siku ya taifa ya utundikaji mizinga mwaka huu, ni Fuga nyuki uongeze kipato, tundika mizinga.

No comments: