Monday, March 25, 2013

HABARI KUTOKA STANDARD RADIO FM 90.1 MHz

Source:SR/E. Lyatuu.

Ed: BM

Date: March 25, 2013.

 

SINGIDA

Jamii katika manispaa ya Singida, imetakiwa kutoona vijana ni mzigo badala yake ione kuwa vijana ni suluhisho la kuleta mabadiliko ya kimaendeleo katika nchi, ili kuondokana na umaskini kwa kuwa vijana ni nguzo ya taifa.

 

Bw. Fidelis Yunde Mratibu na mwanzilishi wa shirika la harakati za vijana katika kuleta maendeleo, Youth Movement for Change YMC amesema hayo, wakati akizungumza na standard radio ofisini kwake, kuhusiana na fursa za vijana katika jamii, mapema leo.

 

Bw. Yunde amesema jamii inapaswa kuwapa vijana hamasa kwa kuwahamasisha, kuwapa nafasi mbali mbali za uongozi kwa kuamini wanaweza, kama vile uongozi katika siasa, kwani wao ni mabalozi wazuri katika vita dhidi ya umaskini.

 

Aidha, amewataka vijana kuunda vikundi mbali mbali kama vile vya kiutamaduni, ujasiriamali, ili kujua jinsi ya kubuni, kuanzisha na kuboresha biashara kwa kupata elimu kuhusu maendeleo ya vijana, na kuchukua hatua kubadili vijiwe vyao kuwa vijiwe vya kazi ili kuleta maendeleo. Amesema vijana wajitume kwa kujishughulisha katika fursa zilizopo kama vile kilimo kwanza, pia viongozi wawekeze zaidi kwa vijana kwa kutoa nafasi za uongozi.

 


Source:Tanzania Daima

Ed: BM

Date: March 25, 2013.

DAR ES SALAAM

Meneja wa wafanyakazi wa ndani ya ndege wa Kampuni ya FastJet, Emma Donavan anayedaiwa kutoa lugha ya matusi kwa mfanyakazi mwenzake, leo amefikishwa mahakamani.

Donavan amefikishwa mahakamani baada ya polisi kukamilisha kazi ya kumhoji sambamba na mashahidi wengine na kisha jalada lake kufikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini DPP, ambaye naye baada kumaliza kulipitia alilirudisha polisi, ili taratibu za kwenda mahakamani ziendelee.

Meneja huyo anakabiliwa na tuhuma za kutoa lugha ya matusi kwa mfanyakazi mwenzake, Samson Itembe. Wiki iliyopita, Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, Deusdedit Kato, alisema walimaliza kumhoji Emma na jalada kupelekwa kwa DPP.

Habari kutoka Kituo cha Polisi cha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu JK Nyerere -Terminal One -  zinasema polisi wamekuwa wakikukusanya ushahidi kutoka kwa wafanyakazi wengine kabla ya jalada kupelekwa kwa DPP.

Meneja huyo ambaye ni raia wa Uingereza alikamatwa wiki iliyopita baada ya kusakwa kwa siku kadhaa.

Source:SR/Bandola.

Ed: BM

Date: March 25, 2013.

 

SINGIDA

Chama Cha Mapinduzi CCM kimewaomba wamiliki halali wa eneo la Nkonkilangi Shelui  katika wilaya ya Iramba mkoani Singida, kuwaruhusu wachimbaji wadogo wadogo wasio na leseni kuendelea kuchimba ili kujipatia riziki.

 

Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Singida Bw. Mgana Msindai wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho mkoani humu.

 

Bw. Msindai amesema kuwa wachimbaji wadogo wadogo wasio na leseni ndiyo walioomba CCM  Mkoa iwasaidie waruhusiwe kuendelea kuchimba na kwenye kikao cha kamati ya siasa mkoa, kilikubaliana chama kisaidie kuwaokoa wananchi wa Nkonkilangi waendelee kujipata riziki zao.

Aidha Bw. Msindai amesema hayo kufuatia mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima  Shehe Semtana aliyeandika kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM mkoani Singida, Bw. Mgana Msindai anatuhumiwa  kupora machimbo ya madini ya wachimbaji wadogo wadogo katika kijiji cha Nkonkilangi na kumkabidhi Bw John Bina bila ridhaa ya wanakijiji.

 

 

Source:SR/Saada

Ed: BM

Date: March 25, 2013.

SINGIDA

Kamishna msaidizi wa madini kanda ya Kati Bw. Manase Mbasha, amewataka wachimbaji wadogo wadogo wa madini kukata leseni, kulingana na maeneo waliyo na uwezo nayo, na kuacha kutegemea wafadhili na wawekezaji.

Bw. Mbasha amesema hayo leo, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kutokana na umhimu wa wachimbaji kukata leseni kulingana na maeneo waliyo na uwezo nayo, na kuacha kuomba leseni ya kumiliki maeneo makubwa ambayo hawana uwezo wa kuyafanyia kazi.

Aidha, Bw. Mbasha ametaja maeneo yenye wachimbaji wadogo wadogo mkoani Singida kuwa ni, Misigiri, Mpambaa, Msangachuki, Londoni, Sekenke, na Nkonkilangi.

Amesema ofisi yake inakaribia kutoa leseni kwa wachimbaji wa madini ya shaba, chumvi, zilikoni, na madini ya chuma.


Source:SR/Saada

Ed: BM

Date: March 25, 2013.

 

DAR ES SALAAM

Rais wa China Xi Jinping leo amehutubia dunia kutokea nchini Tanzania kuelezea sera ya serikali ya China kwa Bara la Afrika.

Hotuba hiyo imetolewa mara baada ya kuzindua na kukabidhi rasmi kituo cha mikutano cha kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es salaam kilichojengwa kwa msaada wa serikali ya China kwa lengo la kumuenzi Mwalimu Nyerere.

Rais huyo wa China amesaini mikataba kumi na saba na rais Jakaya Kikwete, na baadaye ametembelea makaburi ya wataalam wa kichina yaliyopo katika kijiji cha Majohe-Ukonga, ambapo ametoa heshima zake kwa wachina waliofariki wakati wakijenga reli ya TAZARA.

Rais Xi Jinping ameondoka nchini leo jioni kuelekea nchini Afrika kusini kuhudhuria mkutano wa tano wa wakuu wa nchi za BRICS ambazo ni Brazil, India, China na Afrika kusini.

No comments: