Tuesday, March 19, 2013

MSTAKABALI WA NISHATI TANZANIA-MDAHALO

Ajenda ya Maendeleo Baada-ya-2015 na Mustakabali wa Nishati Tunaoutaka kwa Wote
Tanzania, Norway na Umoja wa Mataifa washirikiana mjadala wa ajenda ya nishati
 
Dar es Salaam, Machi 18 Wakati mwaka 2015 unakaribia kwa kasi, bado kuna kazi kubwa ya kufanya kuharakisha kufikiwa kwa Malengo ya Milenia. Wakati huo huo, tunatakiwa tuanze kufikiria nini kitafuata baada ya mwaka 2015. Mjadala huu tayari umeshaanza, kama ilivyoonekana wakati wa “Rio+20”, na serikali katika miaka inayokuja zitajadili na kuamua ajenda ya maendeleo baada-ya-2015.
 
Katika kuchangia majadiliano haya, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa na Ubalozi wa Norway nchini Tanzania wamewezesha, na kwa pamoja wanakuwa wenyeji wa mchakato wa mjadala wa wazi wa kanda Afrika ukihusisha makundi mbalimbali yenye maslahi ikiwamo serikali, asasi za kiraia, sekta binafsi, wasomi na vijana, kuelewa changamoto na fursa zao, na jinsi ya kuingiza masuala ya nishati kwenye ajenda ya maendeleo baada-ya-2015. Ripoti kutoka kwenye mashauriano haya itatoa mchango mzuri kwenye mkutano unaopangwa kufanyika katika ngazi ya kimataifa.
 
Nishati ni suala muhimu katika juhudi za kimataifa kushawishi mabadiliko ya dhana kuelekea kwenye kuondoa umaskini, shughuli za kiuchumi zinazojali mazingira na hatimaye maendeleo endelevu. Kwa namna mbalimbali, mjadala wa kimataifa kuhusu nishati na maendeleo endelevu tayari umeshaanza. Miaka mitano iliyopita imeshuhudia kuongezeka kwa shauku kuhusu masuala ya nishati, ikianza na tamko la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuutaja mwaka 2012 kama “Mwaka wa Kimataifa wa Nishati Endelevu kwa Wote”. Kwa kutambua umuhimu na uharaka wa changamoto za nishati, viongozi katika serikali, biashara na asasi za kiraia wanahitaji kujenga uelewa kimataifa juu ya umuhimu wa nishati kwa maendeleo endelevu.
 
Katika mchakato wa kuhusisha wadau kuhusu hayo yaliyoelezwa, mkutano wa majadiliamo umepangwa kufanyika tarehe 19 Machi 2013 kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam. Watoa mada  wakuu mbalimbali akiwemo Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa; Mkurugenzi wa Nishati, Mazingira na Mabadiliko ya Tabia Nchi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika na Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Norway wamealikwa. Mkutano huu utafunguliwa na Waziri wa Nishati na Madini Mheshimiwa Prof. Sospeter Muhongo.
 
Masuala muhimu yatakayojadiliwa wakati wa mkutano ni pamoja na : Upatikanaji wa Nishati kwa Wote; Kuongezeka kwa Ufanisi na matumizi endelevu ya  Nishati.
Wadau wote wa nishati wanakaribishwa katika mkutano huu.
 
Kwa Taarifa Zaidi Wasiliana na:                       
Mr Styden Rwebangila, Government stydenr@yahoo.com
Ms. Stella Vuzo, United Nations Information Officer at stella.vuzo@unic.org,    
Mr Geir Yngve Hermansen, Norwegian Embassy geir.yngve.hermansen@mfa.no
 

No comments: