Tuesday, August 7, 2012

WAISLAMU SINGIDA WALAANI WAPINGA SENSA



Na. HALIMA JAMAL
SINGIDA

Waislamu mkoani Singida wameungana  kwa pamoja kulaani kitendo cha baadhi ya watu wanaojiita wanaharakati wa dini hiyo kupinga zoezi la uhesabuji wa sensa.

Hayo yamezungumzwa kwa masikitiko na viongozi wa dini ya kiislamu mkoani Singida wakati wakiongea na mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone juu ya kuhimiza waumini wa dini zote kushiriki katika zoezi la Sensa 2012.

Waumini hao wamelaani kitendo hicho kutokana na baadhi ya watu wanaojiita ni wanaharakati kusambaza ujumbe wa maneno kuwataka waislamu kutoshiriki katika zoezi la kuhesabiwa kwa madai ya kuwa zoezi hilo linataka kupoteza kizazi cha waislamu.

Ujumbe huo uliosambazwa kwa njia ya baadhi ya vyombo vya habari, ujumbe mfupi wa maneno (sms) katika simu za mkononi na mitandao kwa kuandika maneno ya uchochezi, unawataka waislamu wasishiriki kabisa

''tunakuhakikishia mkuu wa mkoa kuwa hao wanaoandika ujumbe huo kuwa ni wachochezi tu wa amani ya Tanzania na sisi waislamu wa mkoa wako tunakwambia kuwa jambo hilo kwa upande wetu halipo kwani hata vitabu vya dini vinasema kuwa kila unapofanya jambo lolote unatakiwa kuwa na idadi ya watu na hata ukiwa kiongozi makini unatakiwa kujua unaongoza waumini wangapi''alisema shehe Issa Nasoro.

Shehe Issa Nasoro alisema kuwa waislamu wanaongozwa na viongozi wa dini hiyo na si hao wanaojiita wanaharakati wa dini hiyo na hivyo basi wala ujumbe huo usiwapotoshe watu na kuanza kuichukia dini hiyo kutokana na baadhi ya watu wasioitakia mema Tanzania.

Aidha mkuu wa mkoa wa Singida Dk Kone alisema kuwa yeyote atakayepinga au kuvuruga zoezi hilo kutokana na utofauti wa dini au kabila atakamatwa na kushitakiwa.

Kone ametoa wito kwa viongozi hao wa dini kuhimiza waumini wao kujitokeza kuhesabiwa ili kuwezesha kuleta maendeleo katika nchi yetu.

Aidha zoezi hilo linatarajia kuanza tar26 august mwaka huu na kumalizika tar 31mwaka huu

MWISHO.

No comments: