Thursday, August 23, 2012

MASHIRIKA YA KIJAMII -SINGIDA



Na. Halima Jamal
Singida
SERIKALI wilayani Singida, imeahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGos) ikiwemo shirika la World vision, ili kuharakisha upatikanaji wa maendeleo endelevu kwa wakazi wa wilaya hiyo.
Ahadi hiyo imetolewa juzi na mkuu wa wilaya ya singida, Queen Mlozi, wakati akifungua warsha ya siku tatu iliyohusu kuwasilisha mpango wa STF/EMLAP unaotekelezwa na shirika la World vision.
Alisema mlango wa ofisi yake upo wazi wakati wote kwa mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau mbali mbali wa maendeleo, katika kushirikiana kutatua kero zinazowakabili wananchi.
“Mimi naomba tufanye kazi kama timu moja, wimbo wetu uwe moja, nao ni kuwaletea wananchi wetu maendeleo ya kweli.  Kwa njia hii, tutaharakisha kuboresha maisha ya  wananchi  kiuchumi na kijamii",lifafanua Mlozi.
  Dc huyo alifafanua zaidi kwa kusema, serikali kwa upande wake, haina uwezo wa kutosha kufanya kila kitu kwa maendeleo ya wananchi, kwa hiyo ushirikiano wa NGos na wadau wengine, ni muhimu mno.
Katika hatua nyingine, Mlozi alitumia fursa hiyo kulipongeza shirika la World vision kwa juhudi zake za makusudi  kuanzisha miradi mbali mbali wilayani Singida na hasa katika tarafa ya Mtinko.
“Wananchi wa wilaya ya Singida, tunapaswa kutunza na kuilinda miradi hii iliyoanzishwa na World vision, iweze kudumu kwa muda mrefu.  Kwa njia hii, tutakuwa tunawatia moyo wenzetu wa World vision kuendelea kuleta neema ya miradi zaidi wilayani kwetu”,alisema.
Awali mratibu wa World vision Mtinko ADP,Edwin Maleko, alisema kwa mwaka huu, wametumia zaidi ya shilingi milioni 107.8 kugharamia utekelezaji wa mradi wa afya katika tarafa ya Mtinko.
Alitaja baadhi ya shughuli walizotekeleza kuwa ni kutoa mafunzo kwa vitendo kwa vikundi 51 vya lishe kuhusu njia sahihi za ulishaji wa watoto wadogo na wachanga na kugharamia kilniki tembezi 22 kwa vijiji vya Minyenye na Mughanga.
Maleko alitaja shughuli zingine kuwa ni kukarabati mtando wa maji unaohudumia vijiji vya Mtinko,Nduu,Malolo na Kijota na kuwezesha michezo ya mpira wa miguu,pete na kikapu baina ya vijana wa vijiji 19 ,kwa lengo la kutoa ujumbe unaohusu VVU na UKIMWI.
MWISHO.

No comments: