Friday, February 1, 2013

UJENZI WA HOSPITALI YA RUFAA SINGIDA WASIMAMA



Jumla ya shilingi bilioni mia moja na hamsini zinahitajika ili kukamilisha ujenzi wa hospitali ya rufaa inayojengwa katika eneo la Mandewa, Manispaa ya Singida.

Mganga mkuu wa mkoa wa Singida, Dk. Suleiman Muttani amesema hayo wakati akisoma risala katika hafla fupi ya kukabidhi msaada wa viti ishirini vya magurudumu kwa ajili ya wagonjwa, ambavyo vimekabidhiwa leo na Mbunge wa Singida mjini Bw. Mohamed Dewji katika hospitali hiyo.

Dk. Muttani amesema wanatarajia kujenga jengo litakalokuwa kitovu cha utafiti, ushauri wa magonjwa yasiyoambukiza. Amesema jengo hilo lipo aktika awamu ya tatu ya ujenzi wa hospitali hiyo na litagharimu shilingi bilioni nane nukta moja hadi litakapokamilika.

Amesema kwa sasa mkoa unatafuta fedha na kuzungumza na serikali ambapo mashirika ya hifadhi za jamii yanatarajiwa kutoa udhamini ingawa suala hilo bado halijafanikiwa.
Mbunge wa Singida mjini Bw. Mohamed Dewji ameipongeza serikali kwa hatua ya ujenzi iliyofikiwa, na ameahidi kuweka msukumo zaidi ili mashirika ya hifadhi ya jamii hapa nchini yaweze kutoa udhamini wa ujenzi wa baadhi ya majengo katika hospitali hiyo.

No comments: