Monday, February 25, 2013

TAARIFA YA HABARI KUTOKA STANDARD RADIO


SINGIDA

Jamii imetakiwa kuweka wazi matukio yanayojitokeza kwa viongozi wao wa ulinzi na usalama, ili kufichua wahalifu katika kukabiliana na uhalifu nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo na Kiongozi wa Ulinzi Kata ya Mandewa Bw. Athuman Soteri wakati akizungumza na Standard Radio ofisini kwake.

Amesema ushirikiano miongoni mwa wananchi na viongozi ni jambo la muhimu katika harakati za kukabiliana na uhalifu na matukio mbalimbali nchini.

Amesema kamati ya ulinzi ya kata ya Mandewa imejipanga kufanya doria kila mara kwa kushirikiana na wananchi wa maeneo husika, na tayari wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa na kuwapeleka kwenye vyombo vya dola.

Amesema polisi kata hufika kila siku ya jumanne kutoa elimu kwa viongozi wa ulinzi na kutoa wito kwa viongozi wa vijiji kuandikisha vijana, ili wapewe mafunzo yatakayowawezesha kukabiliana na uhalifu.

Aidha amesema kamati hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile uchache wa askari, wananchi kutokuwa wazi kuelezea matukio yanapotokea, uhaba wa vitendea kazi kama, Virungu, Filimbi pamoja na Tochi ambavyo vinakwamisha utekelezaji wa zoezi hilo.

Ametoa wito kwa serikali kuwasikiliza na kuwa tayari kutoa misaada pale watakapohitaji ili kutekeleza jukumu lao katika jamii.

 


Source SR: Beatrice

Ed:BM

Date: February 25,2013

 

SINGIDA

Mahakama kuu kanda ya Kati mkoani Singida, leo imeahirisha kesi ya mauaji ya Kassim Juma anayekabiliwa na shtaka la kuua kwa kukusudia.

Kesi hiyo, imeahirishwa na Jaji wa mahakama kuu Kanda ya kati, Laurence Kaduri baada ya mshtakiwa kusomewa shtaka linalomkabili na kukana.

Imeelezwa mahakamani hapo kuwa mwezi Juni mwaka 2011, mshtakiwa Kassim Juma alimuua Martin Shilla maeneo ya Shelui wilaya ya Iramba mkoani Singida

Siku ya tukio mshtakiwa akiwa na nyundo mkononi, alimpiga marehemu Martin Shilla kwa nyundo kichwani hali iliyopelekea kuanguka pale pale.

Watu walioshuhudia tukio hilo walimchukua na kumpeleka hospitali ya wilaya ya Iramba mjini Kiomboi ambako alifariki wakati akipatiwa matibabu.

Mshtakiwa alikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi na katika kufanyiwa mahojiano na afisa wa polisi, alikana shtaka hilo na kesi hiyo imeahirishwa hadi kikao kijacho itakaposomwa tena.


 

Ed:BM

Date: February 25,2013

 

IRINGA

Mkuu wa mkoa wa Iringa Dk Christine Ishengoma jana amezindua jengo la upasuaji wa macho katika hospitali ya mkoa huo.

Jingo hilo lenye uwezo wa kuhudumia wagonjwa elfu moja na mia nne na arobaini limekarabatitiwa kwa zaidi ya million sabini zilizotolewa na shirika la kimataifa la kupambana na upovu duniani.

Katika hotuba ya mkuu wa mkoa huo, iliyosomwa kwa niaba yake na mkuu wa wilaya  ya Iringa Dk, Retisia Warioba amewataka watumishi wa hospitali hiyo kulitunza jingo hilo.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka wizara ya afya Dk Salaha Maongezi amesema Tanzania inakabiliwa na changamoto ya vifaa tiba vya macho uchache wa wataalamu wa macho na mwamko mdogo wa wananchi kuhusu ugonjwa wa macho.

Mbali na ukarabati huo, pia shirika hilo limenunua vifaa vya matibabu ikiwemo miwani yenye thamani ya shilingi milioni thelathini.


 

Source SR: Saada

Ed:BM

Date: February 25,2013

 

SINGIDA

Waumini wa dini ya Kiislam mkoani Singida, wametakiwa kushirikiana ili kudumisha amani na upendo nchini.

Sheikh Mkuu wa mkoa wa Singida, Al Haji Issa Simba wakati akizungumza na standard radio ofisini kwake. Amesema matukio yanayotokea yanatokana na kutokuwepo ushirikiano mzuri kutoka madhehebu ya Kikristo na Kiislam.

Amewaomba waumini wa dini ya Kiislam kufuata maadili mema ya dini hiyo na kuachana na mambo maovu na badala yake kufuata mambo mema yatakayowaletea thawabu maishani.

Aidha, Bw. Simba amewashukuru waumini wa dini ya Kiislam mkoani Singida kwa utulivu walionao kutokana na kuzingatia maadili ya dini yao.

 

 

 


 

Source SR:  (kilimo na ujenzi)

Ed

Date: February 25,2013

ZANZIBAR

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ametahadharisha kuwa huenda kuna watu wenye nia mbaya, ambao wameamua kuyatumia matukio ya kuuawa na kujeruhiwa viongozi wa kidini, kujenga chuki baada ya kuona Wazanzibari hivi sasa ni wamoja.

Maalim Seif alisema hayo juzi usiku alipokuwa akihutubia katika hafla ya Maulid ya Kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) mjini Kiuyu, Wilaya ya Wete Kaskazini Pemba.

Alisema inasikitisha kuona wapo viongozi wenye nia chafu dhidi ya Zanzibar, wenye tabia ya kutoa kauli za kujenga chuki na fitna miongoni mwa Wazanzibari chini ya kivuli cha matukio hayo.

Seif aliongeza kuwa, kinachoonekana kuna ajenda imetayarishwa ya kutaka kulazimisha chuki za kidini Zanzibar, licha ya kuwa kisiwa hicho kina historia ya dahari ya watu kuvumiliana na kuishi kwa pamoja.

Aliwataka wananchi wote wa Zanzibar hivi sasa wawe macho na ajenda zinazolengwa kuwavuruga, na waendelee kuishi kwa mshikamano na umoja kama ambavyo wamekuwa wakiishi.

Seif aliongeza kuwa, vitendo vya kuuawa na kujeruhiwa viongozi wa kidini Zanzibar ni mambo magen, na kwa miaka mingi nchi hiyo imekuwa ni mfano bora wa uvumilivu wa kiitikadi za kidini, licha ya kuwa asilimia 98 ya wananchi wake ni Waislamu.

Alieleza kwamba wingi wa Waislamu Zanzibar haukuifanya ifunge milango kwa watu wa imani nyingine, na kwa wakati wote wamekuwa wakiabudu kwa mujibu wa imani zao bila ya bugudha yoyote.

 

 

Source :

Ed: BM

Date: February 25,2013

 

MOROGORO

Shirika la kimataifa la Reading International la nchini Uingereza linatarajia kujenga maktaba arobaini katika shule za sekondari za kata nchini

Hilo limebainishwa na mwakilishi wa shirika hilo, Bw. George Muthabi wakati wa ufunguzi wa maktaba katika shule ya Nelson Mandela wilayani Morogoro.

Amesema mradi huo umeanza kuwanufaisha wanafunzi katika mikoa ya Morogoro, Lindi, Pwani, Dar es salaam na Mtwara

Kwa upande wake mkuu wa shule ya Nelson Mandela Gaudensi Muowa amesema kuwepo kwa maktaba hiyo kutasaidia wanafunzi kupenda kujisomea

Kwa upande wao baadhi ya wanafunzi waliozungumza na waandishi wa habari, wamesema kuwa maktaba hiyo itawasaidia kujisomea kwa umakini na kufanya vizuri katika masomo yao.

No comments: