Saturday, December 15, 2012

SINGIDA KUTOKOMEZA JANGWA


Mkuu wa wilaya ya SIngida akipanda mti katika siku maalumu ya upandaji miti katika manspaa ya Singida katika kampeni maalumu ya kutokomeza jangwa. picha na Ediltruda Chami
 
Na. Edilitruda Chami na Elizabeth Martin.

Mkuu  wa wilaya ya Singida Bi. Queen Mlozi amesema kuwa ni vyema kila mwananchi wa mkoa wa Singida kushiriki katika shughuli za upandaji miti ili kuondokana na hali ya ukame unaosababisha hali ngumu ya maisha mkoani Singida.

Wito huo ameutoa  leo katika Uzinduzi wa awamu ya pili wa kampeni ya vita dhidi ya jangwa na miaka hamsini na moja ya uhuru katika kijiji cha Kitope kata ya Mandewa mkoani Singida.

Katika uzinduzi huo jumla ya miti 400 aina ya miti maji inayotoa  sabuni na mbao,  imepandwa ikiwa kama ishara ya mwendelezo wa tukio hilo ambapo miti hiyo huchanua kila baada ya miaka mitatu

Katika hotuba yake Bi. Mlozi amewataka wananchi kushiriki katika upandaji wa miti pamoja na ufugaji wa nyuki, sambamba na kuwa mstari wa mbele katika kuzuia uharibifu wa mazingira kwani wananchi wa mkoa wa Singida wanaongoza kwa kuchoma mkaa na kusafirisha nje ya mkoa na kwamba atakayekamatwa akichoma mkaa sheria itachukua mkondo wake.

Mtoto huyu ni miongoni mwa watoto wa kijiji cha Kitope kata ya mandewa mjini singida akiunga mkono juhudi za serikali za kupanda miti katika eneo lao ambalo ni jangwa

Hata hivyo wananchi waliohudhuria katika uzinduzi huo wameshukuru uongozi wa manispaa ya Singida kwa mkakati huo wa upandaji miti walioanzisha kwani wanaamini kwa kufanya hivyo, Singida itaonekana kjani na sivyo kama watu walivyojijengea kuwa Singida ni kame na kuwa mstari wa mbele kutimiza kauli mbiu ya ” kata mti panda mti”.

Kampeni hiyo imezinduliwa chini ya mradi wa taasisi binafsi ijulikanayo kwa jina la Anti Desert. Kampeni ya upandaji miti ngazi ya Manispaa ya Singida inatarajiwa kufanyika tarehe 4 Januari mwaka 2013, katika shule ya msingi Unyinga mjini Singida.  Awamu ya kwanza ya kampeni hiyo ilifanyika mwaka 2006.

 

 

No comments: