Sunday, December 30, 2012

GARI LA MAFUTA LANUSURIKA KUUNGUA


 Na Boniface Mpagape.
SINGIDA.

Tela la lori la mafuta ya petroli  lilolokuwa likitoka Dar es salaam kwenda wilayani Ngara mkoani Kagera limeanguka alfajiri 28/12/2012 katika eneo la kisaki manispaa ya Singida na kunusurika kuungua

Akielezea chanzo cha ajali hiyo dereva wa gari hilo Bw. Abdulrahman Shaban amesema lori alIlokuwa akiendesha aina ya  Mercedes Benz lenye namba za usajili T 776 ARL lenye tela namba T 123 ASQ, alikutana na lori jingine lililokuwa limewasha taa kali zilizomsababisha  kutoona mbele na kuacha njia kabla ya kuanguka 

 Amemtaja mmiliki wa lori hilo kuwa ni  Bw. Suleiman Hilal Mohamed maarufu kwa jina la Medi mkazi wa Kabanga wilaya ya Ngara.

Kamanda wa polisi mkoa wa Singida Bw. Linus Sinzumwa amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kwamba raia wamethibitiwa vyema kuzuia uporaji wa mafuta ambao ungeweza kusababisha mlipuko wa moto na vifo. 
Kikosi cha askari polisi kwa kushirikiana na kikosi cha zimamoto na uokoaji mkoani Singida wamefanikiwa kuzuia wananchi waliokuwa wakitaka kuchota mafuta ya petrol yaliyomwagika. 


Mrakibu mwandamizi wa kikosi cha zimamoto na uokoaji mkoani Singida Bw. Kevin Mapunda, amesema raia wengi baada ya kupata taarifa za kutokea kwa ajali hiyo, walikusanyika kwa lengo la kujinufaisha kwa kupora mafuta pasipo kuhofia kutokea ajali nyingine ya mlipuko wa moto.  

Tukio la kupinduka kwa lori la mafuta liliwahi kusababisha watu 44 kujeruhiwa vibaya kwa moto wakati wakipora mafuta  katika wilaya ya Manyoni mkoani Singida  miaka ya nyuma. 

 

 

 

 

 

No comments: